Na Lookman Miraji, JamhuriMedia, Dar es Sakaam

Wasanii kutoka katika kiwanda cha filamu nchini Bongo movie wametoa mitazamo yao kuelekea siku ya tarehe 26 disemba ambapo kutashuhudiwa mfululizo wa mapambano ya ngumi.

Usiku huo uliopewa jina la “Knockout ya mama” unatarajiwa kufanyika huku kukitegemewa kushuhudiwa mfululizo wa mapambano ya ngumi ya kimataifa ambapo mikanda mitano ya kimataifa ya ngumi itashindaniwa.

Akiongoza wasanii katika mkutano na wanahabari, msanii Jimmy Mafufu ameisifu kampuni ya uandaaji mipambano ya ngumi ya Mafia boxing promotion kwa kuandaa tukio hilo kubwa kitaifa huku ikiwa ni sehemu ya muendelezo wa kuunga mkono jitihada za serikali katika kuinua michezo nchini.

Aidha mbali na msanii huyo wasanii wengine wa filamu akiwemo Wema Sepetu, Shamsa ford, Sakina Lyoka na wengine wametoa rai kwa wapenzi wa sanaa na wanamichezo kuungana kwa pamoja katika kushuhudia historia hiyo ambayo itakwenda kubaki katika historia ya mchezo huo kwa muda usiotabirika.

Usiku huo utahusisha jumla ya mabondia 13 wa kitanzania ambao watashuka ulingoni kupigana dhidi ya mabondia kutoka nchi mbalimbali ndani na nnje ya Afrika.

Usiku wa Knockout ya mama unatarajiwa kufanyika Disemba 26 katika ukumbi wa The super dome, masaki, Dar es salaam.