Bondia wa uzani wa Super-feather, John Cooney (28), amefariki dunia baada ya kushindwa na Nathan Howells wa Wales katika pambano lililofanyika Belfast Jumamosi iliyopita.

Cooney, raia wa Ireland, alikumbwa na tatizo la kutokwa na damu kwenye ubongo na kufanyiwa upasuaji wa dharura katika Hospitali ya Royal Victoria, lakini alifariki baada ya wiki moja ya kupigania maisha yake.

Familia yake, kupitia MHD Promotions, ilitoa taarifa ya huzuni, ikimuelezea kama mwana, kaka, na mchumba mpendwa. Cooney alikuwa akitetea taji lake la uzani wa juu wa Celtic, ambalo alilishinda Novemba 2023 dhidi ya Liam Gaynor.

Mwaka 2024, alirejea ulingoni baada ya kuuguza jeraha la mkono na kushinda pambano dhidi ya bondia wa Tanzania, Tampela Maharusi. Kifo chake kimeacha pengo kubwa katika mchezo wa ngumi.