Na Deodatus Balile

Mwezi uliopita nimefanya mapitio ya kitabu kiitwacho “Making Africa Work”. Tafsiri isiyo rasmi ya jina la kitabu hiki ni “Mbinu za Afrika kujikwamua kiuchumi.” Kimeandikwa na Greg Mills, Olusegun Obasanjo (Rais mstaafu wa Nigeria), Jeffrey Herbst na Dickie Davis.

Kimechapishwa na Taasisi ya Brenthurst Foundation ya Johannesburg, Afrika Kusini. Rais (mstaafu) Benjamin Mkapa ameshiriki uzinduzi wa kitabu hiki katika Hoteli ya New Africa, Dar es Salaam. Nilikuwapo.

Katika mapitio ya kitabu hiki, niliandika kwa kina juu ya ongezeko la watu duniani. Nimeeleza kinachotajwa katika kitabu hiki kwamba Tanzania kwa sasa inakadiriwa kuwa na watu milioni 58. Kufikia mwaka 2050 Tanzania itakuwa na watu milioni 138.

Afrika ina watu bilioni 1.2 kwa sasa. Kufikia mwaka 2050 itakuwa na watu bilioni 2.4 na mwaka 2100 Afrika itakuwa na watu bilioni 5.7. Dunia wakati huo itakuwa na watu bilioni 11, hivyo nusu ya watu duniani watakuwa wanaishi Afrika.

 

Sitanii, wakati leo nahitimisha uchambuzi wa kitabu hiki, imenilazimu kurejea mpango tulionao kama taifa. Sera ya Serikali ya Awamu ya Tano ni Tanzania ya Viwanda. Nimeona Tanzania imeeleza mpango wake wa ujenzi wa viwanda. Niaendelea kuusoma na nitauchambua baadaye.

Katika kitabu hicho wameeleza matatizo mengi tunayokabiliana nayo hasa nchi ambazo hazijaendelea. Wameeleza hatari kubwa inayolinyemelea taifa letu ya wingi wa watu. Tanzania kwa mfano kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2012, asimia 84 ya wananchi wake wana umri chini ya miaka 40.

Tanzania haina tofauti na mataifa mengine. Idadi hii ya vijana na watoto wengi ni ‘bomu’, na wakati huo huo ni fursa. Kitabu kinaeleza miradi mbalimbali kama ujenzi wa miundombinu, makazi, uchimbaji madini, sekta ya benki na maeneo mengine mengi. Lakini pia kinaeleza uwekezaji makini.

Sitanii, nimevutiwa na mfano wa nchi ya Morocco. Mwaka 2010, nchi hiyo iliamua kufanya mageuzi ya viwanda. Morocco iliamua kuwekeza katika maeneo sita tu; vifaa vya ndege, magari, viwanda vya nguo na mavazi, uhifadhi wa fedha kimataifa, umeme na kilimo.

 

Kutokana na kubadili sera kuvutia wawekezaji kwa kulegeza masharti, kilomita 30 Kusini mwa Casablanca, kuna kampuni 100 zimewekeza katika viwanda vya vifaa vya ndege na utengenezaji magari. Mfano katika eneo la vifaa vya vipuri vya ndege kampuni kama Matis, Aircelle, Snecma, Sagem, Teuchos, Boeing, Mombardierna Airbas, zimewekeza nchini humo. Kwa sasa kampuni hizo zinafanya biashara ya dola bilioni 1 kwa mwaka sawa na Sh trilioni 2.5.

Kampuni ya kutengeneza magari ya Renault iliyokuwa inaelekea kukata tamaa baada ya awali kuwa imeinunua Fiat, baada ya mabadiliko ya mwaka 2010 ikaanza kuona matunda. Mwaka 2015 viwanda vya magari nchini Morocco vilifanya biashara ya dola bilioni 7, sawa na Sh trilioni 17.5. Kitabu hiki kinaonyesha mwaka 2020 viwanda hivi vitafanya biashara ya dola bilioni 10 sawa na Sh trilioni 25.

Sitanii, Morocco hawa tunaowaomba watusaidie ujenzi wa uwanja wa michezo jijini Dodoma, kati ya mageuzi waliyofanya kuanzia mwaka 2010 ni kuwafutia kodi wawekezaji wenye mtaji wa kuanzia dola 15,000 kwa miaka 5 na kuwataka kuanza kulipa kodi ya asilimia 8.75 ya mapato yao kwa miaka 20 inayofuata.

Sasa hivi, wawekezaji wamefurika na Morocco inaoga fedha. Si hilo, tu Serikali imejenga majengo inawapangisha wawekezaji kwenye ‘business park’, bei ambayo inatoa fedha za ukarabati wa majengo tu, na serikali inafaidi ajira na kodi. Tanzania tunalo la kujifunza katika kitabu hiki. Mzee Mkapa amekisoma na ameshiriki uzinduzi. Naomba tufungue milango. Tufanye mambo kwa utaratibu mpya na tutashuhudia matunda.