Mwishoni mwa wiki, gazeti la Serikali la Daily News limekariri kundi la wanafunzi wakitoa kilio kueleza masikitiko yao kuwa wameshindwa kupata mikopo kutoka Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB), na hivyo kuna wasiwasi kuwa hawataingia vyuoni mwaka huu. Kundi kubwa la wanafunzi waliohojiwa ni la watoto kutoka familia masikini.

Wakuu wa vyuo mbalimbali vya Serikali na binafsi, wametangaza rasmi kuwa mtoto yeyote asiyeweza kulipa angalau nusu ya ada ya mwaka, basi asitie mguu chuoni kwao. Haya yamesemwa na viongozi wa vyuo kama Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Chuo Kikuu cha Dodoma na Chuo Kikuu cha Tumaini. Hiyo inayoitwa nusu ada, tunavyofahamu sisi ni karibu Sh 1,000,000.

 

Serikali yetu ingepitia majalada yake na kuona ni familia ngapi za Watanzania ambazo zimeuza pamba, kahawa, tangawizi, katani, mahindi, mchele, viazi, njegere, maharage, ulezi, mtama, alizeti, pareto, korosho au senene zikaingiza pato la wastani wa Sh 1,000,000 kwa mwaka.

 

Bodi ya Mikopo imesema imeshakopesha wanafunzi wapatao 29,000, hivyo hawana uwezekano wa kupata fedha za kutosha kulipia kila mwanafunzi wa taifa hili. Bajeti waliyopewa kwa ajili ya kukopesha wanafunzi ni Sh bilioni 345, hivyo kiasi hiki hakitoshi kulipia kila muhitaji. Wimbo unaoelezwa ni kwamba bajeti ni ndogo.

 

Sisi tunasema tatizo la nchi yetu si fedha, bali ni ubutu wa sera na viongozi wetu katika kukusanya mapato na kupanga matumizi. Tunatoa kipaumbele katika masuala yasiyo ya msingi. Haiwezekani Serikali imiliki magari yenye thamani ya Sh trilioni 5, karibu nusu ya bajeti yote ya Serikali, lakini asitokee kiongozi hata mmoja tu mwenye akili na moyo wenye nyama akasema tupunguze magari tugharamie elimu.

 

Leo zikitengwa Sh trilioni moja tu, ambazo si kwa kwenda kukinga bakuli, bali kwa kunadisha magari ya starehe ya Serikali, ni wazi wanafunzi wote watasoma shule raha mstarehe. Nchi yetu ni ya tatu barani Afrika kwa kuuza dhahabu nyingi nje ya nchi baada ya Afrika Kusini na Ghana. Tumegundua gesi yenye thamani ya Sh trilioni 680 hadi sasa na bado kuna dalili kuwa itagunduliwa gesi nyingi zaidi na mafuta.

 

Hatutaki kukubaliana na maneno ya Meya wa Dar es Salaam, Didas Masaburi, aliyesema baadhi ya viongozi wanafikiria kwa kutumia makalio, isipokuwa yamesheheni ukweli. Haiwezekani viongozi wetu wasioteshwe jinsi ya kuongeza bajeti ya kukopesha wanafunzi kufikia angalau Sh bilioni 800, lakini wapate fedha lukuki kwa ajili ya uchaguzi na fitina.

 

Tunasema kama Serikali itaendeleza sera hii ya ubaguzi katika elimu, wakati watoto kutoka familia masikini wataishia kidato cha nne na wa matajiri watasoma hadi vyuo vikuu, tutakuwa tunaigawa nchi hii. Waliokosa elimu siku wakiamua kuwageukia waliokaa ofisini na viyoyozi kwa kodi zetu, nchi hii itapungua. Hapatatosha.

 

Tunasema sera hii ni mbaya, Serikali itafute fedha kwa kila hali watoto wote wakopesheke na nchi hii irejee katika usawa tuliokuwa nao mara tu baada ya kupata Uhuru mwaka 1961.