Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Bashiru Ally, amepata jaribio kubwa kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, uchunguzi wa JAMHURI umebaini.
“Siku moja baada ya kuingia ofisini, alijifungia ofisini kwake akasema ana shughuli nyingi hivyo asingeweza kumwona mtu yeyote. Ghafla, akaja mzee mmoja. Akamweleza msaidizi wake tukio la kusikitisha. Tukio lenyewe lilikuwa kama sinema vile.
“Huyu mzee alimwambia msaidizi wa Bashiru huku akitokwa machozi kuwa watu wenye nguvu ya fedha wamechukua kiwanja chake. Msaidizi baada ya kusikia uzito wa suala lenyewe, aliamua kwenda kumwomba Katibu Mkuu amsikilize huyu mzee japo kwa dakika moja.
“Dk. Bashiru aliona lazima suala hili ni zito kama msaidizi amediriki kuja kumweleza kuwa ni la kipekee hivyo amsikilize huyu mzee. Mzee aliruhusiwa kuingia. Aliingia ofisini kwa Katibu Mkuu analia. Alipoingia, akamweleza hivi: ‘Mheshimiwa Katibu Mkuu nimenyang’anywa kiwanja changu kilichopimwa.
“‘Wamekuja watu wenye nguvu ya fedha, wametengeneza nyaraka hizi feki zinazoonyesha kuwa nimefariki dunia, wakatangaza kuwa nimefariki dunia, wakabadili umiliki wakati nipo hai. Kila nikienda ofisi ya ardhi Kinondoni, wananikamata na kunipeleka polisi, kisha jioni wananiachia.
“‘Nimezungushwa na kwa kuwa mtandao wako ni mkubwa, Wizara ya Ardhi sasa imeniambia niende kudai haki yangu mahakamani. Ninachofahamu huko sitapata kitu, wamejipanga wana mtandao mpana. Najiuliza kama wananiona machoni mimi niliyesingiziwa kuwa nimekufa, huko mahakamani ndiyo nitapata nini?’
“Baada ya maelezo hayo, Dk. Bashiru alimpakia kwenye gari huyo Ndugu Msae akaenda naye Wizara ya Ardhi, akamwona Kamishna wa Ardhi, wakamweleza suala lote, lakini hadi hivi sasa ninavyozungumza na wewe, kule wizarani ni danadala.
“Dk. Bashiru hakuridhika. Amelipeleka suala hili TAKUKURU, lakini nao wamelipuuza kwani unakaribia mwaka sasa hakuna kinachoendelea. Huyo bwana aliyeghushi nyaraka anatamba kuwa serikali na TAKUKURU viko mfukoni mwake, hivyo anasema hata hiyo kasi ya Rais John Magufuli ni nguvu ya soda, ameingia madarakani amewakuta, na ataondoka atawaacha maafisa wanaoshughulika na masuala ya ardhi,” amesema mtoa habari wetu kutoka ndani ya CCM.
Mtoa habari ameliambia JAMHURI kuwa Dk. Bashiru analifuatilia kwa karibu suala hili, kwani linachafua sura ya nchi na kuigeuza kuwa taifa la manyang’au ila ana wasiwasi iwapo atafanikiwa kutokana na nguvu ya fedha waliyonayo washirika waliofanikisha njama hizi za hatari.
Kilichotokea katika kiwanja
Maajabu hayaishi Tanzania. Mkazi wa Dar es Salaam, Henry Msae, ametegenezewa nyaraka za kughushi kuonyesha amefariki dunia na umiliki wa kiwanja chake ukahamishiwa kwa mtu mwingine, licha ya kwamba yu hai anaendelea na shughuli zake.
Mbali na kusingiziwa kifo, vilevile ametengenezewa nyaraka feki za ndoa, na baada ya ‘kifo’ chake familia yake ‘feki’ ya mke na watoto watatu, ikamteua ‘mke’ awe msimamizi wa mirathi. Yote hayo yamefanyika kwa ustadi mkubwa kufanikisha uuzaji wa kiwanja chake kwa njia ya utapeli.
Mchezo huo unatajwa kufanywa kwa kushirikisha baadhi ya watumishi wa serikali wasio waaminifu, lakini sasa mambo yamegeuka.
Awali katika sakata hilo, Ofisi ya Msajili wa Hati ni kama vile ilikuwa ikiwakingia kifua wahusika walioghushi nyaraka, kwa kutaka suala hilo likaamuliwe mahakamani, wakitupilia mbali ushauri wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Daniel Chongolo ambaye iliitaka ofisi ya Msajili wa Hati imrejeshee mhusika kiwanja chake kwa kuwa nyaraka zote zilizotumika kufanikisha mchakato wa mauzo na hatimaye ubadilishaji wa miliki ya hati husika umefanywa kwa kurejea nyaraka za kughushi.
Kiwanja kinachohusika katika sakata hilo ni namba 140, kitalu 23 Bunju, jijini Dar es Salaam, kinachomilikiwa na Henry Paschal Msae, tangu mwaka 2003, lakini baada ya mchakato wa kutengeneza nyaraka feki kuwa mmiliki huyo amefariki dunia, familia feki imeketi na kuteua msimamizi wa mirathi ambaye ni mkewe ‘feki’.
Mchakato wa kuanza kubadili umiliki huo kupitia nyaraka feki ulianza kwa kupata taarifa ya polisi ya kupoteza mali/nyaraka (loss report) kutoka Kituo cha Polisi Kawe, jijini Dar es Salaam.
Nyaraka hizo feki zilitumika hatimaye kubadilisha umiliki wa kiwanja hicho mara kadhaa. Kwanza kilibadilishwa kutoka kwa mmiliki halali kwenda kwa mkewe ‘feki’ ambaye naye alikiuza kwenda kwa mtu mwingine, ambaye naye pia alikiuza kwa mwingine, aliyejenga jengo ndani ya kiwanja hicho.
Kauli ya ‘marehemu’
Katika mazungumzo na Gazeti la JAMHURI, mzee Henry Msae amesema haki yake ilikwishaporwa, lakini anamshukuru Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Bashiru Ally, ambaye baada ya kufika ofisini kwake kumweleza shida yake, alichukua hatua madhubuti ikiwa ni pamoja na kuwaona baadhi ya viongozi wa Wizara ya Ardhi, pamoja na kusaidia kutoa taarifa ofisi za Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), makao makuu Dar es Salaam.
“Namshukuru sana Katibu Mkuu wa CCM. Awali, nilikuwa nafuatilia sana suala hili, lakini vitisho vilikuwa vingi. Ilikuwa kila nikifika pale wilayani Kinondoni, nafikiri hawa matapeli walikuwa na mtumishi mmoja pale anawapa taarifa kuwa nimefika. Kila nikifika, mara baada ya muda wanafika askari polisi na kunichukua, wananipeleka Central (Police), nashinda hapo kutwa nzima, wananiachia… hivi vilikuwa vitisho, na ushahidi kwamba mtandao wa uporaji ardhi za watu ni mkubwa Dar es Salaam na unahusisha baadhi ya watendaji serikalini,” amesema.
Msae amekiri kubambikiwa taarifa kwamba amefariki dunia, nyaraka zikiwa zimeandaliwa na kubwa zaidi, akabambikiwa kwa njia ya nyaraka kuwa anaye mke anayeitwa Esther ambaye amezaa naye watoto watatu, na huyo ndiye aliyeteuliwa kuwa msimamizi wa mirathi.
“Nimeshangaa kuambiwa nimefariki dunia, nina mke ambaye si mke wangu,” amesema.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa CCM ameeleza kusikitishwa na kitendo cha baadhi ya watumishi wa serikali kuhusika katika matukio ya uporaji haki za wananchi.
“Katika hili suala kuna mambo mawili muhimu ya kutekelezwa. Kwanza, kumrudishia mzee huyo umiliki wake wa kiwanja. Pili, kuna jinai imefanyika, suala la kughushi nyaraka, lakini vilevile kuna mazingira ya rushwa, bado naendelea kufuatilia kuona suala hili litaishia wapi,” amesema Dk. Bashiru.
Mchezo ulivyokuwa
Uchunguzi wa JAMHURI umebaini kuwa ‘mmiliki’ wa sasa wa kiwanja hicho ambacho kimebadilishwa kwa misingi ya hati za kughushi tangu awali ni Venance Sabi Mulebya ambaye amejenga nyumba katika kiwanja husika.
Kabla ya Mulebya, kiwanja hicho kwa kutumia nyaraka feki zilizoonyesha kuwa mmiliki wa awali, Msae, aliyemiliki kiwanja hicho kwa hati rasmi tangu Oktoba 24, 2003 hati iliyopaswa kudumu kwa miaka 33 kuanzia muda huo, amefariki dunia. Nyaraka feki zilitumika kuwasilisha maombi ya kwanza ya mabadiliko ya umiliki.
Mke feki wa Msae ambaye ndiye aliyetengenezwa kuwa msimamizi wa mirathi, aliwasilisha nyaraka za ushahidi kuwa ‘mumewe’ amefariki dunia, naye ndiye msimamizi wa mirathi, kwa hiyo umiliki wa kiwanja sasa uhamishiwe kwake.
Mke huyo feki nyaraka zinamtambulisha kwa jina la Esther Paschal Lukemo, baadaye ‘mke’ huyo alikiuza kiwanja hicho kwa Seif Nassor Ally wa sanduku la posta 11277, Dar es Salaam ambaye naye aliwasilisha maombi ya ubadilishaji umiliki.
Baada ya hapo, kiwanja hicho kikauzwa kwa Mulebya, na maombi ya mabadiliko ya hati ya umiliki yakawasilishwa tena, uhamisho huo ukapewa kibali ama kuidhinishwa Julai 14, 2017.
Majibizano serikalini
Nyaraka zilizopatikana katika mchakato wa uchunguzi wa Gazeti la JAMHURI zinabainisha kuwa Septemba 19, 2018 iliandikwa barua kutoka Ofisi ya Msajili wa Hati kwenda kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, ikirejea barua kutoka ofisi ya mkurugenzi huyo ya Agosti 28, 2018 yenye Kumb. Na. KMC/77908/24/ES kuhusu kumwondoa mmiliki wa wakati huo (baada ya utapeli kufanyika) katika daftari la usajili na kumrudisha mmiliki wa awali aliyedaiwa kuwa alifariki dunia wakati bado yuko hai.
Barua hiyo ilibainisha kuwa, kumbukumbu zilizomo kwenye daftari la usajili zinaonyesha kuwa kiwanja namba 140, kitalu 23 Bunju, Manispaa ya Kinondoni chenye hati namba 64723 kilisajiliwa kwa mara ya kwanza Desemba 10, 2003 kwa jina la Henry Paschal Msae wa S.L.P 90088, Dar es Salaam, kwa muda wa miaka 33 kutoka Oktoba Mosi, 2003.
Lakini Desemba 7, 2016 Ofisi ya Msajili wa Hati ilipokea maombi ya kutoa hati mpya baada ya hati ya awali iliyoandikishwa kwa jina la Henry Paschal Msae kupotea. Maombi hayo yaliwasilishwa chini ya kifungu namba 38 cha sheria ya usajili sura ya 334. Maombi hayo yaliambatanishwa na ripoti ya polisi (police loss report) kutoka katika Kituo cha Polisi cha Kawe.
Pamoja na maombi hayo, Ofisi ya Msajili wa Hati ilipokea maombi ya kusimamia mirathi ya ‘marehemu’ Henry Paschal Msae yaliyoambatanishwa na barua ya usimamizi wa mirathi kutoka Mahakama ya Mwanzo Magomeni, Wilaya ya Kinondoni. Ofisi ya Msajili wa Hati ilipokea maombi hayo kutoka kwa Esther Paschal Lukemo wa S.L.P 10624 Dar es Salaam, ambaye ndiye mke feki wa Msae.
Hati mpya ilitolewa baada ya kutangazwa kwa siku 30 kwenye Gazeti la Serikali la Februari 10, 2017 na Gazeti la Daily News la Januari 7, 2017, ikifuatiwa na hatua ya kumsajili msimamizi wa mirathi, na mke huyo, Esther Paschal Lukemo alisajiliwa kama msimamizi wa mirathi ya ‘marehemu’ Henry Paschal Msae kwa nyaraka namba 187228.
Aprili 21, 2017 Ofisi ya Msajili wa Hati ilipokea maombi ya uhamisho wa miliki kutoka kwa Esther Paschal Lukemo kwenda kwa Seif Nassor Ally wa S.L.P 11277 Dar es Salaam, na uhamisho wa miliki hiyo ulisajiliwa kwa nyaraka namba 188445.
Agosti 9, 2017 Ofisi ya Msajili wa Hati ilipokea maombi ya uhamisho wa miliki kutoka kwa Seif Nassor Ally wa S.L.P 11277, Dar es Salaam kwenda kwa Venance Sabi Mulebya wa S.L.P 7625, Dar es Salaam, na uhamisho wa miliki hiyo ulisajiliwa kwa nyaraka namba 190563.
Kutokana na mlolongo huo, bila kujali kuwa nyaraka zilizoambatanishwa kuhalalisha mabadiliko hayo ya umiliki zilikuwa za kughushi, kuanzia cheti cha kifo, hati ya polisi ya kupoteza mali (loss report), na katika mazingira yenye utata ya kughushi nyaraka, Ofisi ya Msajili wa Hati ikapendekeza Henry Paschal Msae apeleke shauri hilo mahakamani na mahakama ndiyo itoe uamuzi juu ya uvamizi wa kiwanja hicho, bila kujali kuwa huyo ndiye mmiliki halali tangu mwanzo, na hajafariki dunia.
“Ndugu mwandishi nahakuhakikishia huo ndiyo mchezo wa siku zote hapo ofisini kwa msajili. Kuna watu wasiokuwa na mshipa wa fahamu. Wanafahamu kuwa huyu mzee akienda mahakamani, huko mahakamani wanao mtandao wao, atashindwa kesi tu. Ndiyo maana bila aibu walishauri aende mahakamani.
“Waziri [William] Lukuvi amejitahidi sana kuondoa mambo haya, ila bado kuna masalia mengi. Ndiyo maana wanamkwamisha majadala ya ardhi yasiwekwe mtandaoni. Kwao hali ilivyo sasa ni faida. Kuna watu wengi wamenyang’anywa viwanja kwa utaratibu huu. Hicho mnachokishuhudia ni kiduchu,” amesema mmoja wa maafisa wa ardhi aliyedai yanamkera yanayofanywa na wenzake.
Ushauri wa Ofisi ya Msajili wa Hati kumtaka Msae aende mahakamani umetolewa na ofisa aliyetambulika kwa jina la Joanitha Kazinja, kwa niaba ya Msajili wa Hati.
Wilaya ya Kinondoni
Ofisi ya Wilaya ya Kinondoni katika juhudi za kusimamia haki, Agosti 27, mwaka jana iliandika barua kutoka kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni yenye kumbukumbu namba KMC/LD/77908/24/ES, kwenda kwa Msajili wa Hati, Wizara ya Ardhi, kuhusu kiwanja hicho namba 140, kitalu 23 Bunju, jijini Dar es Salaam.
Barua inaeleza kwamba ofisi hiyo ya Manispaa ya Kinondoni ilipokea barua kutoka Ofisi ya Katibu Tawala wa Wilaya ya Kinondoni kuhusu mgogoro wa uvamizi wa kiwanja hicho ambapo Henry Paschal Msae analalamika kuvamiwa kiwanja hicho na Venance Sabi Mulebya ambaye anafanya maendelezo katika kiwanja husika.
Kwa mujibu wa kumbukumbu za Manispaa, Mkurugenzi anaeleza kuwa kiwanja husika kilimilikishwa kwa Henry Paschal Msae wa S.L.P 90088, Dar es Salaam kwa barua yenye kumbukumbu namba LD/220807/2 ya Oktoba 24, 2033 kwa muda wa miaka 33 iliyoanza Oktoba Mosi, 2003.
“Aidha, nakufahamisha kwamba baadaye ofisi yetu ilipokea nyaraka za kuomba kuhamisha miliki ya kiwanja hiki kutoka kwa Seif Nassor Ally wa S.L.P 11277, Dar es Salaam akidai kuuziwa kiwanja hicho na Esther Paschal Lukemo ambaye kwa mujibu wa nyaraka za uhamisho wa miliki zilizowasilishwa ofisini kwetu ikiwamo hati (certified true copy) yenye CT.no. 64723 ni msimamizi wa mirathi ya Henry Paschal Msae aliyedaiwa kuwa ni marehemu, hivyo ofisi yetu kutoa kibali cha uhamisho huo Aprili 18, 2017. Baadaye tena Seif Ally wa S.L.P 11277, Dar es Salaam alihamisha miliki ya kiwanja hicho kwenda kwa Venance Sabi Mulebya wa S.L.P 76250, Dar es Salaam na uhamisho huo kupata kibali Julai 14, 2017.
Ofisi yetu baada ya kupokea maelezo kutoka ofisi ya Mkuu wa Wilaya juu ya malalamiko ya Henry Paschal Msae na kufanya uchunguzi wa kina juu ya nyaraka zake ilibaini kwamba nyaraka zilizowasilishwa na Esther Paschal Lukemo ikiwamo hati (certified true copy) yenye CT.No. 64723, fomu za mirathi (I-IV), mkataba wa mauziano, (land form no. 35, land form no. 29, land form no. 30) pamoja na ‘consent of beneficiaries’ vimepatikana kwa njia ya udanganyifu kwa kuwa Henry Paschal Msae hakufariki dunia kama nyaraka hizo zinavyoeleza.
Katika msisitizo, ofisi ya Wilaya Kinondoni ambayo awali ndiyo iliyopokea hati hizo za kughushi, ikaeleza kuwa upatikanaji wa kiwanja hicho ulikuwa wa udanganyifu, kwa hiyo ofisi inapendekeza kiwanja hicho kiondolewe kwenye daftari la usajili wa hati ili mmiliki halali ambaye ni Henry Paschal Msae ambaye yupo hai aweze kurejeshewa miliki yake.
Barua hiyo ya kupigania haki iliyotaka kuporwa ilisainiwa na Geofrey S. Mwamsojo, kwa niaba ya Mkurugenzi Manispaa ya Kinondoni.
Kauli za majirani
Gazeti hili lilizungumza na ‘majirani’ wa Msae ambaye licha ya kujenga jengo dogo ndani ya kiwanja hicho na kumweka mwangalizi, hakuwa anaishi hapo, isipokuwa alikuwa akifika katika nyakati tofauti kukagua eneo lake na kusalimu majirani zake.
Jonas Ndagi, mmoja wa majirani hao maarufu kwa jina la ‘Baba Jojo’ anasema: “Tunafahamu kuwa kiwanja hiki ni cha mzee Msae kwa muda mrefu, mwaka juzi nafikiri tukapata taarifa kuwa amefariki dunia. Tukasikia eneo hili limeuzwa. Hatukujua kinachoendelea.”
Lakini baada ya kusikia taarifa za kifo cha Msae, jirani mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Philipo Nyaki, alijaribu mara kadhaa kupiga simu ya Msae, haikupatikana, naye akaamini huenda ni kweli amefariki dunia.
“Nilipiga hiyo simu yake haikuwa hewani. Tukahisi labda ni kweli amefariki dunia kwa kuwa mara ya mwisho alipokuja kukagua eneo lake afya yake haikuwa nzuri, nafikiri hao matapeli wametumia huo mwanya. Hapo katika eneo lake aliweka mlinzi tunayemjua kwa jina la Baba Agatha, huyu naye tukashangaa ameondoka kwa makubaliano na hao waliodai ni kiwanja chao sasa,” amesema.
Lakini kwa upande wake, jirani Ndagi anasema: “Dalali aliyehusika katika huu mchezo yupo hapo Bunju anaendelea na mambo yake. Hawa watu wachukuliwe hatua za kisheria. Huu ni uonevu.”
Mawazo ya mzee Msae
Kuhusu uamuzi wake endapo mipango ya kurejesha haki yake itafanikiwa, hasa hatima ya jengo la ‘mnunuzi’ lililojengwa ndani ya kiwanja chake, mzee Msae anasema: “Huyo mtu amekuwa na dharau sana juu yangu. Niliwahi kumwita ofisi ya Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa ili tuzungumzie suala hilo akanitukana, akaniita mimi takataka. Mtu wa namna hiyo utaweza kujadiliana naye kweli? Ni bora tu kuvunja hiyo nyumba.”
Amesema waliofanya kitendo hicho dhidi yake walikuwa na dhamira ya wazi ya kumpora mali yake kiasi cha kughushi nyaraka hadi za kifo chake. Ameshauri vyombo vya dola vitumie nafasi yao kisheria kumsaidia ikiwa ni pamoja na kuwachukulia hatua wahusika wote wa sakata hilo.
Tayari mzee Msae amekwisha kuhojiwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuhusu sakata hilo na taarifa za uhakika ambazo JAMHURI limezipata zinabainisha kuwa taasisi hiyo chini ya Mkurugenzi wake Mkuu, Kamishna Diwani Athumani inaendelea na uchunguzi wa suala hilo.
Waziri Lukuvi alifanyia kazi
JAMHURI limewasiliana na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, aliyesema suala hilo amelipata, na analifanyia kazi kwa kina. “Haya mambo yamekuwapo mengi tu. Watu wamedhulumiwa sana miaka ya nyuma. Ndiyo maana tumeamua kuanzisha hati za dijitali. Kwamba mtu aweke hadi ‘finger print’ zake, hivyo kughushi itakuwa haiwezekani tena. Nalifanyia kazi, jibu litapatikana,” amesema.