Moto aliouwasha Rais John Magufuli wiki iliyopita kwa kutaka ufanyike uchunguzi wa kina juu ya umiliki halisi wa kampuni ya Airtel umegeuka bomu linaloelekea kuwalipukia vigogo wanaoheshimika kwa kiasi kikubwa hapa nchini, uchunguzi wa JAMHURI umebaini.
Tayari Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Wizara ya Fedha, Msajili wa Hazina na vyombo vingine vimeunda timu maalum kuchunguza mchakato, waliokuwa wajumbe wa Bodi na mawaziri waliohusika kwa njia moja au nyingine katika mchakato wa kuhamisha hisa za TTCL kwenye kampuni ya Airtel, ambazo zimepotelea kusikojulikana.
Aliyekuwa Waziri mwenye dhamana na Mawasiliano, Prof. Mark Mwandosya, Mwenyekiti wa Bodi, Jaji Joseph walioba na majina mengine makubwa yanatajwa kuwa uchunguzi ulioanza unaopaswa kukamilika ndani ya wiki moja hautawaacha salama.
Uhalali wa Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) kumiliki hisa zote ndani ya kampuni ya Airtel Tanzania, joto lake likizidi kupanda siku hadi siku baada na kauli ya Rais Magufuli na aliyekuwa Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano kipindi hicho, Prof. Mark Mwandosya, amejitokeza kuanika kila anachokifahamu katika sakata hili.
Prof. Mwandosya ambaye amekuwa Waziri katika kipindi chote cha Awamu ya Tatu (1995-2005) chini ya Rais Benjamin Mkapa pamoja na kuendelea kuwa Waziri Serikali ya Awamu ya Nne (2005-2015), ameliambia Gazeti la JAMHURI, katika mahojiano maalum kwamba taratibu zote za kuhamisha hisa za Airtel zilifuatwa kwa mujibu sheria na yeye hakuwa na uamuzi bali ‘mshika kibendera’.
“Naomba ukumbuke mambo matatu; jambo la kwanza ni ubinafsishaji, hii ilikuwa ni sera ya nchi, kwa hiyo hilo huwezi ukalihoji, maana limekubalika na chama tawala, limekubalika na serikali pamoja na washirika wetu wa maendeleo na TTCL ilikuwa moja kati ya mashirika 400 ambayo yalitakiwa kubinafsishwa.
“Sasa unaweza kuanza kuhoji huko, kwamba ilikuwa ni sera mbovu, hata watu wengi sasa wanaacha mambo ya msingi na kwenda kwenye utekelezaji na kuhoji utekelezaji. Kwa hiyo ukienda kwenye msingi basi uende kwenye misingi na ukikiua msingi unakuwa nje ya msingi wa kutekeleza sera, linakuwa ni jambo kubwa sana.
“Watu wanasahau mwaka 1993, tuliunda chombo maalum cha kisheria PSRC. Chombo hicho kilipewa madaraka kamili, uhuru na uwezo wa kufanya kazi yake bila kuingiliwa na wizara ama mtu yeyote yule. Sheria hiyo ipo mnaweza kwenda kuisoma, kwa hiyo tulikuwa na chombo maalum cha kutekeleza sera ya serikali.
“Jambo la tatu, watu wanasema sasa kuna uhusiano gani na wizara zilizohusika? Nadhani ni vema mkajua kwamba baada ya kuipa madaraka makubwa PSRC iliyokuwa chini ya Ofisi ya Rais, PSRC ilikuwa ikifanya kazi yake inapeleka mapendekezo kwa serikali ili kupata baraka. Sasa PSRC haiingii Baraza la Mawaziri, hivyo mawaziri wa sekta ndiyo wanapeleka mapendekezo hayo ya kisekta kwenye Baraza la Mawaziri. Baada ya pale yanakuwa ni maamuzi ya Baraza.
“Kwa hiyo kwa kweli yote yaliyofanyika yalikuwa utekelezaji wa maamuzi ya Baraza la Mawaziri. Sasa unaweza ukasema, baada ya pale Waziri alikuja [na] msimamo huu, Waziri Prof. Mwandosya, hana mamlaka ya kutaifisha ama kuuza mali za serikali. Nilikuwa ni msemaji tu [wa] hiyo sekta, kwa maana ya kile kilichokubaliwa ndani ya Baraza la Mawaziri,” anasema Prof. Mwandosya.
Kwa mujibu wa taarifa ya mwaka ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu hesabu zilizokaguliwa za serikali kuu na mashirika ya umma kwa mwaka wa fedha ulioishia Juni 30, 2013, kulikwa na mgogoro wa hisa kwa muda mrefu.
“TTCL ilianzishwa kwa Sheria ya Kampuni ya Simu Tanzania Na. 20 ya mwaka 1993 na kusajiliwa chini ya Sheria ya Makampuni Na. 212, Desemba 1993 baada ya kuvunjwa kwa lililokuwa Shirika la Posta na Simu Tanzania mwaka 1993.
“Hadi hivi sasa hisa za TTCL zinamilikiwa na Serikali na Bharti Airtel Tanzania B.V kwa uwiano wa asilimia 65 na asilimia 35 sawia na hivi sasa kuna mazungumzo kati ya Serikali na Bharti Airtel juu ya Serikali kununua hisa asilimia 35 za Bharti Airtel ili imiliki asilimia 100 za TTCL,” inasomeka sehemu ya taarifa hiyo.
TTCL ikisema mchakato wa kuirudisha Airtel mikononi mwake utakuwa ni vita kubwa, kampuni ya Bharti Airtel inayomiliki hisa nyingi za kampuni hiyo ya simu za mkononi, imejitokeza na kusema, “Uwekezaji wetu ulifuata na kuzingatia sheria na taratibu kabla haujapata baraka zote za Serikali ya Tanzania,” ameongeza Prof. Mwandosya.