Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), imejionea maendeleo ya miradi mbalimbali iliyopo Dar es Salaam ili kuona juhudi zinazofanywa na timu ya ujenzi chini ya usimamizi wa Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Hamad Abdallah.
Ziara hiyo yenye lengo la kukagua maendeleo ya ujenzi imewajumuisha wajumbe wote wa bodi pamoja na viongozi waandamizi wa NHC.
Bodi ilipata fursa ya kutembelea miradi ya Kawe 711, Morocco Square, Samia Housing na eneo la NHC Urafiki ambayo inajumuisha ujenzi wa nyumba za makazi na biashara. Mwenyekiti wa Bodi, Dk Sophia Kongela, alitoa maelekezo akitaka umuhimu wa kuimarisha utekelezaji wa miradi na kuhakikisha ubora unaendelea kuzingatiwa kwa kila hatua.
“Ni muhimu kwa Bodi yetu kufanya ziara kama hizi ili kujionea moja kwa moja maendeleo ya miradi yetu. Tunajivunia juhudi zinazofanywa na timu yetu ya ujenzi na tunahakikisha kwamba miradi yote inatekelezwa kwa viwango vya kimataifa,” amesema Dk.Kongela.
Viongozi wa NHC waliokuwepo katika ziara hiyo waliweza kutoa maelezo ya kina kuhusu changamoto zinazojitokeza katika ujenzi na hatua ambazo zimechukuliwa ili kuhakikisha miradi inakamilika kwa wakati na kwa ubora unaotarajiwa.
Bodi inaendelea na ziara katika miradi ya Samia, Morocco Square na Eneo la NHC Urafiki kufuatilia utekelezaji wa maelekezo na miongozo yake.
Ziara hii ni sehemu ya juhudi za NHC katika kuhakikisha kuwa inatoa suluhisho la makazi bora kwa wananchi na kusimamia rasilimali za umma kwa ufanisi na uwazi.