Miongoni mwa habari tulizozipa umuhimu wa juu hivi karibuni ni ile inayohusu matumizi mabaya ya fedha yanayofanywa na Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlala ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA).
Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) amebaini kuwa kwa mwaka uliopita, bodi hiyo iliketi vikao 20 badala ya vikao vinne vya lazima na viwili vya kazi za ukaguzi na uandaaji wa bajeti. Kwa kawaida vikao haipaswi kuzidi sita kwa kipindi cha mwaka mmoja wa fedha.
Vikao hivyo 20 vimegharimu fedha za walipa kodi Sh bilioni 1.1. Hiki ni kiwango kikubwa mno cha fedha ambacho hakipaswi kuachwa hivi hivi bila majibu au kuwawajibisha wahusika wakiongozwa na mwenyekiti wa bodi hiyo.
Tunatambua kuwa ripoti ya CAG inaweza kuwa na upungufu, lakini katika hili hatudhani kama kweli CAG alikuwa dhaifu kiasi cha kukosea idadi ya vikao.
Kumekuwapo malalamiko ya muda mrefu kuwa tangu bodi hii iteuliwe, imekuwa ikitaka kufanya kazi za menejimenti. Imekuwa na vikao, si vingi tu, bali virefu kuliko ilivyo kawaida. Katika hali ya kawaida, yeyote mwenye akili anaweza kujiuliza, iweje bodi iketi kwa siku 10 mfululizo? Kuna mambo gani ya ajabu, makubwa na ya kutisha ya kuifanya isiketi vikao 6, isiketi vikao 12, isiketi vikao 18 lakini iamue kuketi vikao 20?
Tunahoji haya maswali tukitambua kuwa fedha za NCAA ni fedha za umma, kwa hiyo wanaoteuliwa kuongoza bodi ya wakurugenzi hawaendi kuongoza kwa kutoa fedha zao mifukoni, bali wanatumia fedha zinazopaswa kuwanufaisha Watanzania wenye mahitaji ya kweli.
Huko nyuma tuliwahi kuandika habari nyingi zilizohusu ufisadi ndani ya bodi za NCAA na tukadhani kuwa kwa hofu na kwa uadilifu bodi hii ya sasa ingekuwa makini, hivyo kutenda kazi zake kwa weledi. Matokeo yamekuwa kinyume.
Haya ya Ngorongoro bila shaka yako kwenye taasisi, idara na mashirika mengi ya umma. Hiki kilichofanywa na Bodi ya NCAA bila shaka kipo kwenye bodi nyingine nyingi.
Tunatoa mwito kwa mamlaka husika kutoa majibu ya hatua stahiki zinazochukuliwa kwa watafunaji wote wa aina hii ya Ngorongoro. Kunyamazia matendo ya aina hii ni kwenda kinyume cha dhamira njema ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kuhakikisha fedha za umma zinatumika kwa njia zilizo sahihi. Bodi zisiwe vyanzo vya kuyaua mashirika ya umma. Kwa hili la Ngorongoro wananchi wanasubiri majibu.