Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam

BODI ya Mkonge Tanzania (TSB), imesema kuwa imekuwa ikiwaunganisha wakulima wa zao hilo na masoko ili wapate soko la bei nzuri.

Hayo yamesemwa na Mkuu sehemu ya Maendeleo ya Mkonge kutoka TSB, Saimon Kibasa katika maonesho ya Wakulima na Wafugaji (Nanenane), ambayo yanafanyika Kitaifa viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma.

Amesema kuwa Wizara ya Kilimo imeweka mpango wa kuweka vituo vya usindikaji wa zao la Mkonge lengo likiwa ni kumsaidia mkulima mdogo ili aweze kusindika na kupata nyuzi, singa ambazo zitakubalika katika soko la ndani na nje ya nchini.

Ameongeza kuwa lengo la kuhamasisha kilimo hicho ni zao ambalo lina soko kubwa na ni zao ambalo linastahimili magonjwa, ukame na ni la uhakika kumpatia mkulima kipato.

“Tanzania wakulima wamegawanyika katika makundi matatu wadogo, wakubwa na wakati…wakulima wakubwa hawana changamoto kama ilivyo wa wakulima hao wadogo. Na wakulima wadogo nao wamegawanyika katika sehemu mbili wanaolima kwenye mashamba yao binafisi na wanaofanya biashara lakini wapo ambao wanalima kilimo cha mkataba kinachoendeshwa katika mashamba matano nchini yakiwamo Ngombezi na Magoma,” amesema.

Amefafanua kuwa katika mashamba hayo yana mikataba kati ya mkulima mdogo na Bodi ambapo inamkodisha mkulima huyo na kazi yake ni kulima na kutunza mkonge.

“Kuna mkataba kati ya vyama vya ushirika vilivyopo katika mashamba hayo na usindikaji. Wote hawa wanasimamiwa na Bodi kwa kushirikiana na ofisi ya msajili wa vyama vya ushirika Mkoa wa Tanga katika maeneo hayo, TSB imekuwa ikiwasimamia wakulima kuhakikisha wanapata bei nzuri kupitia wanunuzi mbalimbali,” amesema.

Ameongeza kuwa lengo la kuhamasisha kilimo hicho ni zao ambalo lina soko kubwa na ni zao ambalo linastahimili magonjwa, ukame na ni la uhakika kumpatia mkulima kipato.