Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam

BODI ya Kahawa imezindua mradi wa mgahawa unaotembea maeneo mbalimbali yenye mikusanyiko ya watu ili kuweza kutoa huduma ya unywaji wa Kahawa.

Akizungumza na waandishi wa habari kwenye maonesho ya wakulima na wafugaji (Nanenane) yanayofanyika kitaifa katika viwanja vya Nanenane Nzuguni jijini Dodoma Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Kahawa, Primus Kimaryo amesema wamebuni mradi huo unaotembea ili kuwaweza vijana kujipatia kipato kupitia zao hilo la Kahawa.

Kimaryo amesema mradi huo unawalenga vijana ambapo watapata mradi huo kwa mkopo nafuu na baada ya miaka mitatu muhusika anapaswa kurejesha gharama hizo za mkopo na mgahawa unakuwa ni mali yake.

Amesema vijana mbalimbali wameshaonesha nia ya kutaka kuwa na mgahawa huo.

“Lengo la mkakati huu ni kuongeza unywaji wa Kahawa kutoka asilimia 7-8 ambao ni unywaji wa sasa kwenda asilimia 15. Pia msukumo mkubwa ni kuona namna gani vijana wanaweza kupata ajira kupitia zao la Kahawa kwani kijana kupata ardhi au kukodisha mgahawa ni changamoto,” amesema.

Amefafanua kuwa, mpaka hivi sasa gharama za mkopo huo ni Shilingi milioni 30 huku akisema wanaanza kwa kutengeneza migahawa 100 ambayo pia itatengenezwa kwa awamu.

Amesema kabla kupata mradi huo vijana wote wataokidhi vigezo vya kupata mkopo huo waapatiwa mafunzo ya uendeshaji wa migahawa hiyo ili iweze kuleta tija iliyokusudiwa.

Please follow and like us:
Pin Share