Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam

BODI ya Utalii Tanzania (TTB), imesema imelenga kuhakikisha fursa zote za utalii wa Tanzania kuanzia ngazi ya halmashauri zinatambulika ili kuliingizia Taifa pato.

Hayo yameelezwa mwishoni mwa wiki mkoani Morogoro n Mkurugenzi Mkuu wa TTB, Ephraim Mafuru w wakati akizungumza na wahariri kutoka vyombo mbalimbali vya habari Kwa ajili ya kuelezea mikakati mbalimbali ya bodi hiyo.

Amesema mchango wa utalii katika pato la taifa umezidi kuongezeka ambapo mwaka 2023, Serikali iliingiza Sh. bilioni 3.4 na jumla ya watalii milioni 3.7 walitembelea vituo mbalimbali vilivyopo nchini.

“Mtaona ni jinsi gani utalii wetu unaendelea kukua, hata hivyo TTB tumejipanga kuhakikisha idadi ya watalii inaendelea kuongezeka ikiwemo kwa kutambulisha mazao mapya ya utalii ambayo bado hayafahamiki zaidi,” amesema Mafuru.

Ameyataja mazao ya utalii ambayo wanatarajia yatasaidia kuongeza kipato kuwa ni talii wa Wanyamapori, utalii wa fukwe na meli, utalii wa utamaduni na malikale, utalii wa mikutano na matukio pamoja na utalii wa michezo.

“Tumejua mahitaji ya watalii yanazidi kubadilika na sisi Bodi ya Utalii tumesema ili kuweza kutangaza vivutio vingi lazima tuwe wabunifu. Mfano ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kuna nyumbu zaidi ya milioni 1.8 na pundamilia zaidi ya laki tano ambao wapo katika migration kwa miezi 11 wanakuwa bado wapo katika ardhi ya Tanzania.

“Nimeambiwa kuna zoezi la nyumbu kuzaa kwa pamoja, ambapo ana uwezo wa kusimamisha kukua kwa mimba ili azae mwezi wa pili au wa tatu. Hili ni jambo la kipekee ambalo linapatikana katika Hifadhi hii, kwahiyo bodi ya utalii tumedhamiria ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti tuitangaze hii tofauti ili watalii wa ndani na nje ya nchi waweze kuja kushuhudia jambo hili,” amesema.

Aidha amesema wamejipanga kujenga kituo kikubwa cha mikutano jijini Arusha ambacho kitaitwa Mount Kilimanjaro International Convention Center (MKICC) kitakachokuwa na uwezo wa kubeba wageni 3,000.

Amesema pia wamejipanga kuhamasisha utalii hasa kwa vijana pamoja na kuongeza vyanzo vipya vya mapato.

Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Mikumi, Kamishina Msaidizi wa Uhifadhi Agustine Masesa amesema Agosti, mwaka huu Hifadhi hiyo itaadhimisha miaka 60 tangu kuanzishwa kwake Agosti,mwaka huu.

“Hifadhi hii ndo inaongoza kwa wageni wa ndani na imekuwa pendwa kwa sababu ya miundombinu rafiki hivyo watalii kutoka Dar es Salaam, Iringa, Dodoma Moro na Mbeya hutembelea kwa wingi.

Hata hivyo amesema kuanzishwa kwa Treni Mpya ya Kisasa (SGR) kumechangia kuongezeka kwa idadi ya watalii kutoka jijini Dar es Salaam na Zanzibar.

“Tunamshukuru Rais Samia kwa kuanzisha treni hii, sasa hivi watalii kutoka Dar es Salaam na Zanzibar wamezidi kuongezeka kwasabbau ya uwepo wa treni hiyo ambapo wanaweza kupanda asubuhi wakafika hapa Mikumi na jioni wakaweza kurudi na treni hiyo,” amesema Masesa.