Na Magrethy Katengu,JamuhuriMedia,Dar es Salaam
Tanzania imefikia , mauzo ya nje Jumuiya ya Nchi za Kusini mwa Afrika yameongezeka kutoka shilingi trilioni 2.607 mwaka 2016 hadi shilingi trilioni 4.422 mwaka 2023, na mauzo nje kwenye Jumuiya ya Ulaya yameongezeka kutoka shilingi trilioni 0.605 mwaka 2016 hadi shilingi trilioni 3.835.65 mwaka 2023, huku bidhaa zilizouzwa kwa wingi ni za kilimo, hususan kahawa, chai, mahindi, ngano, mchele, mbogamboga na bidhaa za viwandani.
Akizungumza leo na Waandishi wa habari Julai 28,2024 jijini Dar es Salaam, Waziri wa Viwanda na Biashara, Selemani Jafo, amesema Serikali imefanya mapitio ya Sera ya Taifa ya Biashara ya mwaka 2003 na kutoa toleo la 2023, lenye lengo la kuweka mfumo mkakati madhubuti unaolenga kuboresha mazingira ya biashara, kuongeza ukuaji wa kiuchumi na kuboresha ustawi wa wananchi na utekelezaji wa sera hiyo utailetea nchi faida nyingi ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa mchango wa sekta ya biashara katika pato la taifa.
Sera hiyo mpya inalenga kuimarisha na kuendeleza biashara ya ndani na nje, pamoja na kuimarisha mtengamano na ushiriki wa nchi katika biashara na nchi zingine rafiki, kikanda na kimataifa.
“Sera hii ni marejeo ya sera ya mwaka 2003 ambayo imefanyiwa marekebisho ili iweze kuendana na mabadiliko ambayo yametokea katika nyanja mbalimbali kikanda na kimataifa,” amesema Dk. Jafo.
Sanjari na hayo ameongeza kuwa sera hiyo itaimarisha mazingira ya ufanyaji biashara, kuvutia uwekezaji, kuongeza shughuli za biashara na ajira, kuongeza kipato cha wananchi, na kuimarika kwa uzalishaji viwandani kutokana na upatikanaji wa masoko ya uhakika hivyo kuchochea jitihada za ujenzi wa uchumi wa viwanda.
“Sera hii inaongozwa na kauli mbiu isemayo ‘Ushindani wa Biashara katika kuchochea kasi ya Mabadiliko ya Kijamii na Kiuchumi yanayoongozwa na Viwanda’. Inatarajiwa kuzinduliwa rasmi Jumanne, Julai 30 na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Mashaka Biteko,” amesema Dk. Jafo.
Dk. Jafo amebainisha kuwa sera hiyo itachangia kuwepo kwa ushindani huru na haki katika biashara, kumlinda mlaji, kuimarika kwa ratibu wa biashara, na kuondokana na mgongano wa kisera, kisheria, na mgawanyo wa majukumu ya kitaasisi katika masuala ya biashara.
“Kuimarika kwa miundombinu ya masoko na biashara; kuimarika na kuongezeka kwa biashara ya nje, na kuongezeka kwa ufanisi katika utendaji wa shughuli za biashara kupitia matumizi ya mifumo ya kibiashara,” amesema ” Waziri Jafo.
Waziri Jafo ametaja baadhi ya mambo yaliyoainishwa katika sera hiyo ni kuimarisha, kukuza na kuendeleza biashara ya ndani na nje, kuimarisha mtengamano na ushiriki wa nchi katika biashara na nchi zingine rafiki, kikanda na kimataifa, na kuimarisha maendeleo na ujenzi wa miundombinu ya masoko na biashara.
Amesema sera hiyo pia melenga kuimarisha usimamizi wa ushindani halali wa kibiashara na kumlinda mlaji, kuendeleza biashara ya huduma, kuwezesha na kuimarisha biashara mtandao kupitia matumizi ya teknolojia, na kuimarisha na upatikanaji wa mikopo na mitaji ya biashara.
Waziri Jafo alieleza mafanikio ya sera ya mwaka 2003 kuwa ni serikali kufanikiwa kushiriki kikamilifu katika majadiliano mbalimbali ya biashara baina ya nchi na nchi, kikanda na kimataifa kwa lengo la kuongeza fursa zaidi za biashara ya bidhaa na huduma kutoka Tanzania ikijumuisha kupata masoko yenye masharti nafuu kwa ajili ya wafanyabiashara wa Tanzania.
“Fursa hizi ni pamoja na zile zinazotokana na soko la Jumuiya ya Afrika Mashariki, Jumuiya ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), AfCFTA, soko la China kwa kuuza bidhaa bila kulipa ushuru wala kikomo kwa asilimia 98 ya bidhaa zote kutoka Tanzania, India, AGOA kwa kuuza zaidi ya bidhaa 6,400 bila ushuru,” amesema Jafo.
Faida nyingine ni kumewezesha mchango wa biashara katika pato la taifa kufikia asilimia 8.3 mwaka 2023, kupitia fursa hizo mauzo kwenda Jumuiya ya Afrika Mashariki yameongezeka kutoka shilingi trilioni 1.12 mwaka 2016 hadi Sh trilioni 3.022 kwa mwaka huo.
Vilevile, mauzo ya nje Jumuiya ya Nchi za Kusini mwa Afrika yameongezeka kutoka shilingi trilioni 2.607 mwaka 2016 hadi shilingi trilioni 4.422 mwaka 2023, na mauzo nje kwenye Jumuiya ya Ulaya yameongezeka kutoka shilingi trilioni 0.605 mwaka 2016 hadi shilingi trilioni 3.835.65 mwaka 2023, huku bidhaa zilizouzwa kwa wingi ni za kilimo, hususan kahawa, chai, mahindi, ngano, mchele, mbogamboga na bidhaa za viwandani.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkazi wa kampuni ya Trade Mark Afrika, Elibariki Shami, aliipongeza Tanzania kwa kufanya maboresho hayo na kusisitiza kuwa ni vema kila taifa liige hatua hiyo ili biashara ziweze kufanyika kwa urahisi.
“Sera hii itarahisisha kufanya biashara katika maeneo mbalimbali ya kikanda kwa sababu nchi nyingi za Afrika zinashindwa kufanya kwa pamoja kwa sababu ya kukinzana katika sera za biashara,” amesema Shami.
Aidha Julai ,30,2024 Naibu Waziri Mkuu ambaye pia ni Waziri wa nishati Dkt Doto Biteko anatarajiwa kuhudhuria katika hafla ya uzinduzi wa sera ya Taifa biashara 2003 toleo la 2023 itakayofanyika katika ukumbia wa Mlimani city Jijini Dar es salaam