Na Mwamvua Mwinyi,JamhuriMedia,Bagamoyo
Wilaya ya Bagamoyo,mkoani Pwani, inazalisha chumvi tani 90,000 hadi tani Laki moja kwa mwaka.
Kutokana na kiwango hicho cha uzalishaji kwenye sekta ndogo ya madini ya chumvi wilayani humo, Serikali imekusudia kuweka mazingira wezeshi ambapo tayari imeshapata mkandarasi wa kujenga miundombinu ya barabara kwa lengo la kuongeza tija .
Aidha, Serikali imekamilisha taratibu za kupeleka nishati ya umeme ili kuongeza uzalishaji wa madini hayo.
Waziri wa Madini Dkt. Dotto Biteko alieleza hayo ,wakati alipofanya ziara katika viwanda vya kuzalisha chumvi vya Sea Salt na Stanley vilivyopo katika eneo la Saadani wilaya ya Bagamoyo.
Dkt. Biteko alisema, katika kuhakikisha uzalishaji wa madini ya chumvi unaimarika nchini, Serikali inaboresha mazingira kwa ajili ya uzalishaji wa chumvi kwa kuzuia uagizaji wa chumvi ghafi kutoka nje ya nchi, kupunguza tozo na kodi zilizokuwepo kwenye sekta ndogo ya chumvi.
“Kama mnavyofahamu Serikali ilikuwa inatoza zaidi ya tozo 17 ,” kwa sasa imezipunguza na kubaki tozo nane lakini vilevile mrabaha wa chumvi ulikuwa asilimia tatu Serikali imepunguza mpaka asilimia moja,” anasema Dkt. Biteko.
Alifafanua, takwimu za Wizara ya Madini zinaonesha kwamba eneo la Bagamoyo linazalisha kati ya tani elfu 90 hadi tani laki moja za madini ya chumvi kwa mwaka ambapo bado kuna uhitaji wa kuzalisha zaidi kutokana na uwepo wa Pwani ndefu zaidi kuliko nchi nyingine za jirani”anasema Dkt.Biteko.
Dkt. Biteko alitoa wito kwa Halmashauri ya wilaya ya Bagamoyo kutoza tozo rafiki kwenye sekta ya chumvi ili hali zisiwaongezee mzigo mkubwa wazalishaji wa madini hayo.
Awali Mkurugenzi wa Kiwanda cha Stanley, Richard Stanley alieleza kuwa changamoto kubwa inayoikabili Sekta Ndogo ya Madini ya Chumvi katika eneo la Bagamoyo ni ukosefu wa masoko ya bidhaa hiyo, miondombinu ya barabara ambayo kipindi cha masika haipitika kiurahisi pamoja na ukosefu wa nishati ya umeme.
Nae, Ofisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Dar es Salaam na Pwani Mhandisi Ally Maganga alieleza, wanaendelea kutatua changamoto zilizopo ,lengo likiwa kuongeza uzalishaji, kuongeza ajira, kuongeza mapato ya serikali na kuongeza upatikanaji wa fedha za kigeni.