Na Mwandishi wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt.Dotto Biteko ameieleza Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kuwa Serikali inafurahishwa na mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) kwa kutoa kipaumbele cha fursa za ajira kwa Watanzania kupitia utekelezaji wa Sera ya kuwawezesha wazawa ( Local Content).

Akizungumza wakati akijibu hoja za wajumbe wa Kamati hiyo ya Bunge iliyotaka kujua namna miradi inavyowanufaisha Watanzania, Naibu Waziri Mkuu Biteko amesema kupitia miradi mbalimbali mikubwa ya kimkakati ya sekta ya nishati ukiwemo wa EACOP, Serikali inahakikisha Watanzania wanapewa kipaumbele cha ajira kupitia sera hiyo, ili kuwawezesha kiuchumi na kufaidika moja kwa moja kupitia miradi hiyo.

“Ni muhimu Watanzania wakafaidika na utekelezaji wa miradi mikubwa ya sekta ya nishati inayotekelezwa hapa nchini linapokuja suala la fursa kupitia miradi hiyo,” amesema Dkt.Biteko.

Ameipongeza Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) kwa kusimamia vyema utekelezaji wa masuala ya ajira kwa wazawa kupitia miradi mikubwa ya sekta ya nishati ukiwemo wa EACOP, ambao utahusika na usafirishaji wa mafuta ghafi kutoka Kabaale, wilaya ya Hoima nchini Uganda hadi pwani ya Chongoleani mkoani Tanga kwa ajili ya kuuzwa katika soko la kimataifa.

Amesema Ewura imekuwa mstari wa mbele kuhakikisha sera ya miongozo ya ushiriki wa wazawa inatekelezwa kwa ufanisi, jambo ambalo linawezesha Watanzania kunufaika na fursa za ajira katika miradi mikubwa.

“Ni jambo la kujivunia kuona miradi mikubwa kama EACOP inavyotoa kipaumbele cha ajira kwa Watanzania kama sehemu ya utekelezaji wa sera hii ili kuwawezesha wazawa kiuchumi,” amesema Naibu Waziri Mkuu.

Amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kushirikisha wadau mbalimbali wa sekta ya nishati ili kuimarisha ushiriki wa wazawa katika miradi inayotekelezwa hapa nchini.

Mradi wa EACOP umekuwa ukitoa fursa mbalimbali za ajira kwa Watanzania katika maeneo mbalimbali ikiwemo kuwapa nafasi wakandarasi wazawa katika utoaji huduma mbalimbali katika mradi huu.

Pia umekuwa ukitoa kipaumbele cha ajira kwa watu wa makundi mbalimbali zikiwemo kazi zinazohitaji utaalamu, huku kipaumbele cha kwanza kwa kazi zisizohitaji ujuzi kikitolewa kwa wazawa wanaoishi jirani na maeneo ya mradi huu unaopita katika mikoa 8 na wilaya 24 hapa nchini.

Mradi huu una jumla ya umbali wa kilomita 1,443 utakaohusisha ufukiaji wa mabomba ardhini kwa ajili ya usafirishaji huo wa mafuta ghafi.

Kati ya kilomita hizo, 1,147 zipo nchini Tanzania na 296 zipo nchini Uganda.

Katika mradi huu, Serikali inamiliki hisa asilimia 15 kupitia Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC).

Wanahisa wengine wa mradi wa EACOP ni Shirika la Mafuta nchini Uganda (UNOC) linalomiliki hisa asilimia 15, Shirika la mafuta nchini China (CNOOC) linalomiliki hisa asilimia nane, huku kampuni ya TotalEnergies ikimiliki asilimia 62.

Mwisho