Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Tanga
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Mashaka Biteko, ameipongeza Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), kwa usimamizi thabiti wa huduma za nishati na maji nchini ambao ameeleza kuwa umechangia kuleta na kuimarisha utulivu kwenye sekta ya nishati na taifa kwa ujumla.
Biteko alitoa pongezi hizo juzi wakati akifungua kikao cha nne cha Baraza la Pili la Wafanyakazi wa EWURA kinachofanyika jijini Tanga.
“EWURA mnafanya kazi kubwa ya kudhibiti upatikanaji wa huduma za uhakika za umeme na mafuta nchini kwa ufanisi mkubwa, mmeleta utulivu kwenye sekta ya nishati nchini, mmerahisiha mazingira ya uwekezaji kwenye CNG, vituo vya mafuta vijijini na kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji kwenye nishati safi ya kupikia, nawapongeza sana.” alisema Biteko.
Dkt Biteko alisisitiza EWURA kuendelea kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia, kuendelea kuweka mazingira wezeshi ya kiudhibiti kuhusu ajenda ya misheni 300 ya umeme na kuwasimamia watoa huduma wanaodhibitiwa kuhakikisha wanakuwa na mikataba ya huduma kwa mteja inayotekelezeka.
Aidha, aliitaka EWURA kuhakikisha inaendelea kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara ya mafuta nchini, na kushirikisha wadau na watoa huduma wanaodhibitiwa kwenye maamuzi ya kiudhibiti ili utekelezaji wake uwe na tija.
Katika hatua nyingine, alitoa rai kwa EWURA kufanya tafiti za kina kuhusu huduma zinazodhibitiwa ili kubaini maeneo yanayohitaji kutiliwa mkazo, kufanya kazi kwa weledi na kufuata sheria ikiwamo kupokea hoja za wanaokosoa utendaji wa taasisi ili kuisaidia kujitathmini na kuboresha zaidi utendaji wake.





