📌 Asema pamoja na dunia kuhamia kwenye nishati jadidifu, makaa ya mawe yatasaidia Afrika kuwa na umeme wa kutosha
📌 Aeleza mafanikio sekta ya nishati Tanzania katika Jukwaa la Mawaziri Wiki ya Nishati India
📌 Tanzania yapongezwa kwa miradi ya kikanda ya umeme
Na Mwandishi Wetu
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema kuwa pamoja na dunia sasa kuweka mkazo ikiwemo ya kifedha kwenye uzalishaji umeme kwa kutumia nishati jadidifu kama vile jua, maji na upepo, nchi za Afrika zinapaswa kutumia vyanzo ilivyonavyo kama vile makaa ya mawe ili kuweza kuwa na umeme wa kutosha.
Dkt.Biteko amesema hayo juzi, New Delhi, India wakati akishiriki katika mjadala wa Mawaziri wa Sekta ya Nishati kutoka India, Qatar, Uingereza na Tanzania wenye mada iliyosema Mpango Mpya wa Dunia wa Biashara ya Nishati ikiwa ni sehemu ya Mkutano wa Wiki ya Nishati India.
![](https://www.jamhurimedia.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/1a.jpg)
Dkt.Biteko ametolea mfano kuwa Tanzania ina madini ya makaa ya mawe ya kutosha pamoja na urani ambayo yanafaa kuzalisha umeme hata hivyo kumekuwa na changamoto ya kupata ufadhili wa kuyaendeleza kwa ajili ya kuzalisha umeme kwa vile yanatajwa kusababisha uchafuzi wa mazingira akieleza kuwa makaa ya mawe yanaweza kutumika kuzalisha umeme kwa kutumia teknolojia ya kisasa yenye kuondoa sumu ya kaboni.
Amesema kuwa takribani watu milioni 600 barani Afrika hawajafikiwa na huduma ya umeme hivyo kwa kuzalisha umeme kwa kutumia vyanzo mbalimbali ikiwemo makaa ya mawe itawezesha lengo la kufikishia umeme watu hao kwa haraka.
“ Afrika inachangia uchafuzi wa mazingira kwa kiasi kidogo kwa sababu ni bara maskini lakini inatajwa kuwa na mchango sawa na mataifa mengine, mabadiliko ya matumizi ya nishati hayakwepeki, nchi ziruhusiwe kuwa na uendelezaji endelevu wa rasilimali zake kwa ajili ya kuwa na usalama wa nishati.” amesisitiza Dkt. Biteko.
Ameongeza “ Lazima tuangalie ukweli na hali halisi mfano Qatar au India hali yao ya upatikanaji umeme ni tofauti na Tanzania, hatutaweza kutumia njia ya aina moja kwa ajili ya kutatua changamoto za masuala ya umeme kati ya nchi zilizoendelea na zinazoendelea ni lazima kutumia njia tofauti,”
![](https://www.jamhurimedia.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/0-21.jpg)
Ameangazia lengo la Mkutano wa Nishati wa Wakuu wa Nchi Afrika (Mission 300) uliofanyika nchini Tanzania hivi karibuni wa kufikisha nishati ya umeme kwa watu milioni 300 barani humo ifikapo mwaka 2030 na kusisitiza kuwa pia Afrika inahitaji fedha na miundombinu ya kusafirisha umeme pamoja na vyanzo mseto vya uzalishaji umeme ili kufikisha lengo la kuwapatia umeme wananchi wake kwa asilimia 100.
Pamoja na hayo, Dkt. Biteko amebainisha mafanikio ya sekta ya nishati nchini Tanzania na kusema kuwa kuna umeme wa kutosha huku ziada ikiwa ni megawati 750 na kwamba imejenga miundombinu ya kusafirisha na kuunganisha umeme na nchi jirani kama vile Kenya, Burundi na Rwanda ili kuwezesha biashara ya umeme.
Waziri anayeshughulikia masuala ya nishati kutoka Uingereza, Mhe. Ed Milliband ameipongeza Tanzania kwa mafanikio yake katika uzalishaji na usambazaji umeme kwa wananchi na hasa miradi ya umeme kwenda katika nchi jirani.
Kwa upande wake, Waziri wa Petroli na Gesi kutoka nchini India, Mhe. Hardeep Singh Puri amesema kuwa
Mkutano huo wa Nishati India unalenga kuwakutanisha pamoja viongozi wa sekta ya nishati, watunga sera na wavumbuzi kutoka maeneo mbalimbali duniani ili kujadili changamoto zilizopo katika sekta hiyo na kutafuta suluhushi kwa mustakabali endelevu wa upatikanaji wa nishati.
Aidha, utaangazia teknolojia za kisasa, mipango kabambe ya kupunguza uzalishaji kaboni na fursa za uwekezaji zinazoendana na malengo ya nishati kimataifa.
![](https://www.jamhurimedia.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/1.jpg)