Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko leo Oktoba 21, 2024 akiwa nchini Singapore amekutana na kufanya mazungunzo na Mwakilishi wa Heshima wa Tanzania nchini humo, Bw. Teo Siong Seng ambaye pia ni mwenyekiti mwenza wa Kampuni ya Pacific International Lines (Pte) Ltd.

Katika mazungumzo yao, Dkt. Biteko amesema kuwa Serikali inathamini kazi ya uwakilishi inayofanywa na Bw. Seng na kuwa itaendelea kumpa ushirikiano katika kutekeleza jukumu hilo.

Pia, ameikaribisha sekta binafsi kwa ajili ya kuwekeza katika sekta ya nishati ili kuongeza kasi ya uzalishaji, uunganishaji na usambazaji wa nishati nchini Tanzania.

Kwa upande wake, Bw. Seng ameishukuru Serikali kwa kumpa fursa hiyo ya kuiwakilisha Tanzania nchini Singapore huku akiahidi kuendelea na jukumu hilo ikiwa ni pamoja kutangaza utalii.

Dkt. Biteko yuko nchini Singapore kwa ajili ya kushiriki Mkutano wa 17 wa Wiki ya Kimataifa ya Nishati ambao unalenga kuwakutanisha wadau wa sekta hiyo kwa ajili ya kujadili mahitaji ya nishati yanayoongezeka duniani ikiwa ni pamoja na kuharakisha juhudi za kupunguza hewa ya ukaa.