ARUSHA
Na Hyasinti Mchau
Binti wa Arusha, Rawan Dakik (20), ameweka rekodi ya kuwa Mtanzania wa kwanza mwanamke kupanda Mlima Everest.
Mlima huo uliopo nchini Nepal, barani Asia, ndio mrefu kuliko yote duniani, kilele chake kikiwa mita 8,849.
Rawan, amerejea nchini wikiendi iliyopita na kupata mapokezi makubwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), yaliyoongozwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja.
“Nina furaha kubwa kwa mafanikio haya. Ni sifa kwa taifa letu pia. Kwa hakika mafanikio yangu yametokana na wazazi kunipa ujasiri mkubwa hata kama walifahamu kuwa nitakumbana na changamoto za hapa na pale,” anasema Rawan akizungumza na JAMHURI.
Binti huyo amewasili kwa ndege ya Shirika la Ndege ya Qatar, na miongoni mwa waliokuwapo kwenye mapokezi hayo ni Mtanzania wa kwanza kupanda mlima huo, Wilfred Moshi, aliyepanda mwaka 2012.
Ateuliwa kuwa Balozi wa Utalii
Rawan ameteuliwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii kuwa Balozi wa Utalii, akiahidi kumwalika binti huyo bungeni jijini Dodoma.
“Mbali na kumwalika bungeni, pia atapewa nafasi ya kutambuliwa na taasisi za utalii watakakompa maelezo zaidi juu ya vivutio vilivyopo nchini,” anasema Naibu Waziri Mary.
Waziri huyo amemzawadia Rawan picha maalumu inayoonyesha wanyama na mandhari mojawapo ya hifadhi za Tanzania.
“Sisi kama Watanzania tunamshukuru Mungu tumempokea mtoto wetu akiwa mwenye nguvu na afya. Niwapongeze wazazi wa Rawan kwa kumsaidia binti yao kufikia malengo yake, kwani tumeambiwa ameanza kupanda milima akiwa na umri wa miaka 12 tu,” anasema.
Anasema Rawan amekuwa akipanda milima mbalimbali Afrika ukiwamo Mlima Kilimanjaro.
“Tunastahili kumpongeza binti yetu huyu kwa kuipa heshima nchi yetu kwa kuitangaza kimataifa. Tumemuona mara zote akipeperusha bendera ya taifa, hivyo hata ambao walikuwa hawaijui Tanzania sasa wameijua,” anasema Mary.
Mwenyewe ataka vipaji vitambuliwe
Akizungumza kwenye mapokezi hayo, Rawan ametaka vipaji vya vijana nchini vitambuliwe, vithaminiwe, viheshimiwe, vitangazwe na viendelezwe, kwani mafanikio ya vipaji hivyo yataleta heshima kwa taifa.
“Katika safari ya kupanda Mlima Everest, nimepitia changamoto nyingi za hatari. Kilichonipa nguvu ni ahadi yangu ya kubeba wajibu wa kulipa taifa langu heshima.
“Nimefanikiwa kufika kwenye kilele cha Mlima Everest nikiwa msichana wa kwanza mdogo zaidi kwa umri kutoka barani Afrika,” anasema Rawan.
Anamshukuru Mungu kwa kumuwezesha kuweka historia hiyo huku akiwashukuru Watanzania kwa maombi na salamu za heri, akisema zilimtia moyo na kumfanya ajiamini zaidi hatimaye kufikisha bendera ya taifa katika kilele cha mlima huo.
Rawan ameyatoa mafanikio yake hayo kama zawadi kwa Watanzania.
“Pia ni zawadi kwa Rais wetu, mama yetu, Samia Suluhu Hassan,” anasema Rawan.
Anasema ameweza kupanda Mlima Everest baada ya kupata uzoefu kwa kupanda Mlima Kilimanjaro kwenye malango matatu tofauti; Marangu, Machame na ya mzunguko wa kilele cha Kibo kwa upande wa kaskazini.
Ameushukuru ujumbe wa serikali ulioongozwa na Naibu Waziri Masanja, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongella na Mbunge wa Arusha Mjini, Mrisho Gambo kwa mapokezi waliyompatia, pia Kamishna wa Uhusiano wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), Paschal Shelutete.
Kupanda mlima wa saba mwakani
Baba yake Rawan, Karim Dakik, mmiliki wa Kampuni ya Alpha Group Ltd ya jijini Arusha, anasema Rawan ameshapanda vilele vya milima sita kati ya saba alivyopanga kupanda ambapo anatarajia kupanda Mlima Denali uliopo Alaska, Marekani.
“Atapanda mlima huo wakati wa likizo ya masomo Juni mwakani na kutimiza ndoto zake.
“Furaha yetu kubwa zaidi ilikuwa Mei 23, mwaka huu. Saa 9:35 alfajiri kwa saa za Afrika Mashariki. Rawan alipofika kilele cha Mlima Everest akiwa salama na kuiweka bendera ya Tanzania ambayo ilipepea kuisalimia Tanzania,” anasema Dakik na kuongeza:
“Tupo na bendera hiyo iliyopepea kwenye mlima huo mrefu zaidi duniani ikituma salamu kwa nchi yetu ya Tanzania na wananchi wake kutokea juu ya kilele hicho ikisema; kazi iendelee,” anasema Dakik.
Anasema ni furaha kumwona binti yao akitumika kuitangaza Tanzania duniani, hasa kwenye masuala ya utalii, upendo na amani.
“Siku ya mwisho ya kufika kileleni ilikuwa yenye hofu kubwa, kwani alipoteza mawasiliano na tulipokuwa tunaangalia mtandaoni, tuliona kulikuwa na upepo mkali ambao ulikuwa unachana mahema juu ya mlima. Tukaanza kumwomba Mungu, lakini baada ya saa 22 tulipata ujumbe wake kuwa yuko salama na ameshashuka mita 8,000. Tukamshukuru Mungu,” anasema Dakik.
Mongella: Rawan kuhamasisha vijana
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mongella, amempongeza Rawan kwa kuwa msichana wa kwanza kutoka Afrika kufika kilele cha Everest.
“Tutamtumia Rawan kuhamasisha vijana wengine, awajaze ujasiri waweze kupanda milima wakianza na ya kwetu; Meru na Kilimanjaro,” anasema Mongella.
Anasema hata yeye amehamasika na mwaka huu atawaalika viongozi na rafiki zake wapande Mlima Kilimanjaro.
TANAPA wajivunia Rawan
Meneja Uhusiano wa TANAPA, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi, Shelutete amesema wanajivunia kuwa sehemu ya mafanikio ya Rawan na kwamba kufika kwake kilele cha Everest kumeutangaza zaidi Mlima Kilimanjaro kimataifa.
“Rawan amefanya mazoezi kwenye Mlima Kilimanjaro, na nyakati zote alipokuwa akihojiwa amekuwa akieleza hivyo, jambo ambalo linatupa matumaini makubwa kuwa ujumbe huo umewafikia watu wengi wa mataifa mbalimbali, hivyo wale wenye nia ya kupanda Mlima Everest watakuja kufanya mazoezi kwenye Mlima Kilimanjaro ambao ni mlima mrefu kuliko yote barani Afrika,” amesema Shelutete.