DAR ES SALAAM

Na Andrew Peter

Baada ya kuishuhudia Taifa Stars ikipokea kipigo cha mabao 2-0 kutoka kwa Algeria katika mchezo wa Kundi ‘F’ kusaka kufuzu fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2023, Ivory Coast, macho na masikio ya mashabiki sasa yamegeukia katika Ligi Kuu Tanzania Bara kutaka kuona iwapo Coastal Union itatibua rekodi ya Yanga ya kutangaza ubingwa bila kufungwa katika mchezo wa kwanza kati ya miwili watakayokutana ya kuamua ubingwa hivi karibuni.

Yanga itaikaribisha Coastal Union kesho kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, wakijua ni ushindi pekee utakaowapa ubingwa wa Ligi Kuu kwa mara ya kwanza baada ya kusubiri kwa miaka minne. 

Pia wawili hao watakutana tena Julai 2, jijini Arusha katika mechi ya fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) itakayochezwa kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid.

Bingwa wa Ligi Kuu mbali na kupokea kombe jipya, pia kwa mara ya kwanza ataweka kibindoni fedha taslimu Sh milioni 600 wakati mshindi wa pili ataondoka na Sh milioni 300, huku atakayeshika nafasi ya tatu atachukua Sh milioni 250 na timu ya nne itaondoka na Sh milioni 200.

Wakati timu inayoshika nafasi ya tano itapata Sh milioni 65; ya sita Sh milioni 60; ya saba Sh milioni 55; ya nane Sh milioni 50; ya tisa Sh milioni 45 na ya kumi Sh milioni 40.

Watakaoshika nafasi ya 11 wataondoka na Sh milioni 35; ya 12 Sh milioni 30; ya 13 Sh milioni 25 na nafasi ya 14 ya kucheza mechi ya mtoano ataondoka na Sh milioni 20.

Hata timu mbili zinazoshuka daraja hazitaachwa bure kwani nazo zitaondoka na kifuta jasho cha Sh milioni 10 kila moja, wakati timu yenye nidhamu itaondoka na zawadi ya Sh milioni 20.

Pongezi nyingi ziwaendee wadhamini wa Ligi Kuu, Kampuni ya Azam Media Limited na Benki ya NBC.

Ukiangalia mgawo wa fedha ambazo klabu zitapata ni ishara kwamba thamani ya ligi imepanda, hivyo viongozi wa klabu hawapaswi kubweteka kwa fedha hizo, bali kuhakikisha wanatafuta wadhamini wengine ili kuzipa nguvu ya kiuchumi klabu zao.

Viongozi wa klabu wakiwa makini katika kutafuta fedha za wadhamini hakuna shaka kwamba watafanikisha lile lengo la leseni za klabu linalopigiwa kelele na CAF na TFF wanaozitaka timu zote kuwa na viwanja vyao vya mazoezi, pia kuwa na timu za vijana za uhakika kwa lengo la kukuza vipaji.

Mbali ya yote, pia udhamini wa aina hii ni fursa kubwa katika kuboresha maisha ya wachezaji wanaocheza Ligi Kuu hivyo kuongeza ushindani ndani ya uwanja na kupunguza yale matatizo ya wachezaji kuuza mechi.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Azam Media Limited, Tido Muhando, wakati wa kutia saini mkataba wa udhamini wa ligi kupitia haki za matangazo ya televisheni alisema: “Miaka minane iliyopita imetufanya kufahamu uendeshaji wa timu. Tumeona changamoto nyingi wanazopitia, tumeona maisha ya wachezaji na tumekuwa sehemu ya maisha hayo ndiyo maana tumeguswa kwa kiasi kikubwa katika mkataba huu.”

Hakuna ubishi ni lazima viongozi wa klabu wafanye jitihada za makusudi kuhakikisha maisha na masilahi ya wachezaji wanaocheza Ligi Kuu yanakuwa mazuri na bora, kwa kuanzia mishahara yao na bonasi wanazotoa kwa timu.

Hii itawezekana iwapo wachezaji wanaocheza katika klabu kubwa watakubali kuungana na wenzao na kupigania masilahi yao kwa pamoja, kwani bila ya kufanya hivyo ni viongozi pekee watakaonufaika na fedha hizi za udhamini.

Msimu unaelekea mwishoni, wachezaji wanapaswa kuingia katika majadiliano na viongozi wa klabu, hasa Bodi ya Ligi na TFF kupigania kuwapo kima cha chini cha mshahara cha wachezaji wanaocheza Ligi Kuu.

TFF na Bodi ya Ligi wanapaswa kupitisha sheria kabisa endapo klabu itashindwa kulipa mishahara yao japo ya kima hicho cha chini, basi itashushwa daraja au haitapaswa kupanda kucheza Ligi Kuu.

Mafanikio ya uwekezaji mkubwa wa Ligi Kuu yanayoendelea kuonekana hayatakuwa na maana endapo maisha ya wachezaji, hasa wa Kitanzania yataendelea kuwa duni.

0655 413 101