Na WAF, Bungeni Dodoma.
Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel amesema, Bima ya afya kwa wote itakuwa suluhu ya kudumu kwa wananchi wote ikiwemo watoto wasio na wazazi na wasiojiweza ambao awali walikuwa wakilipiwa na wahisani kupitia “Toto Afya Kadi”.
Dkt. Molel amebainisha hayo leo Septemba 8, 2023 wakati akijibu swali la Mhe. Abdul-Haffar Idrissa Juma Mbunge wa Mtoni katika Bunge la 12, kikao cha tisa, Jijini Dodoma
Dkt Mollel amesema ni kweli kuwa, mfumo wa kulipia watoto kupitia “Toto Afya Kadi” umebadilika na kwa sasa unafanyika kupitia utaratibu wa shule na vifurushi vya bima ya afya vya najali, wekeza na Timiza na kueleza suluhu ya kudumu ni kuingia kwenye Bima ya afya kwa wote itayotoa fursa kwa wananchi wote kupata matibabu bora katika vituo vyote.
“Suluhisho la kudumu ni kukamilika kwa Muswada wa sheria wa Bima ya Afya kwa wote ambao tunaamini utawezesha watoto wengi zaidi wasio na walio na changamoto za kiafya kulipiwa Toto Afya Kadi” amesema.
Aidha, Dkt. Mollel amesema, Serikali imeendelea kutoa elimu mashuleni ili kutambua uwepo wa Bima ya afya kwa watoto, huku akitoa wito kwa waheshimiwa Wabunge kuendelea kutoa elimu kwa wananchi katika ngazi zote ikiwemo wazazi juu ya vifurushi vyenye matibabu kwa watoto na umuhimu wa Bima ya Afya kwa wote.
Pia Dkt. Mollel amesema, Serikali ina utaratibu wa kutoa matibabu bure kwa watu wasio na uwezo wa kumudu gharama za matibabu kupitia barua ya kiongozi katika eneo lake analoishi inayothibitisha hali yake ili apewe matibabu.