Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia

Serikali imepanga kuboresha huduma za afya ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa bima ya afya kwa wote inawafikia Watanzania wote.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya Ummy Mwalimu wakati akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari mbalimbali leo Januari 23,2023 jijini Dar es Salaam.

Waziri Ummy amesema kuwa inayowakumba Watanzania katika kupata huduma za afya ni gharama kuwa juu,hivyo amesisitiza wahariri kuwahamasisha wananchi kuwa na bima ya afya ambayo itawawezesha kupata matibabu kwa urahisi.

Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF),Bernard Konga

“Hivi sasa ukiwauliza Watanzania changamoto kubwa inayowakabili katika kupata huduma za afya watakueleza kuwa ni gharama kubwa za matibabu.

“Kama kweli tunawapenda kweli Watanzania tuwahamasishe na kuwahimiza kuwa na bima ya afya ili waweze kupata matibabu kwa urahisi kabla ya kuugua” amesema Waziri Ummy.

Amesema kuwa Serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imedhamiria kuboresha sekta ya afya kwa kutoamuacha nyuma Mtanzania kwa kuhakikisha kuwa anapata huduma ya afya popote alipo kwa kutumia kadi ya bima ya afya ya NHIF.

“Hatutaki mtu akataliwe kupata huduma kwa ukosefu wa kadi ya bima na ndio maana Serikari imedhamiria kuboresha sekta hiyo hivyo Mswada Bima ya Afya kwa Wote ambao unatarajiwa kupelekwa bungeni Februari mwaka huu na kuanza kutumia Julai mwaka huu utakuwa na manufaa makubwa kwa Watanzania.

“Tuna ushahidi wa kesi za watu wanaouza nyumba zao ili waweze kugharamia matibabu. Kwetu sisi Serikali kupitia Wizara Afya, bima ya afya tunaichukulia kama ukombozi kwa Mtanzania kwa sababu atapata uhakika wa kupata matibabu bila vikwazo.

“Bima ya afya ni kwa ajili ya kumsaidia Mtanzania hususani masikini,kwa sasa Mtanzania masikini akiumwa atauza mali zake alizonazo ili apate matibabu,wapo wanaouza pikipiki,viwanja ili tu kumudu gharama za matibabu” amesema waziri Ummy.

Akizungumzia mchakato huo,Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF),Bernard Konga, ambaye pia mjumbe wa Kikosi Kazi Muswada wa Bima ya Afya kwa wote amesema kuwa chimbuko la kuandaliwa kwa muswada huu ni kutimiza wajibu wa serikai wa kikatiba wa kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma bora za afya bila vikwazo.

“Uhalisia unaonyesha kywa idadi kubwa wananchi (asilimia 85) hawana bima ya afya na hivyo kukosa uhakika wa kupata huduma za afya pindi wanapozihitaji.

“Sheria zilizopo kuweka uhiari wa wananchi katika sekta isiyo rasmi na sekta rasmi ya binasi kujiunga na bima ya afya hatua ambayo inasababisha wengi kujiunga wakiwa tayari na matatizo ya kiafya,” amesema Konga.

Katibu mkuu wa Wizara ya Afya Profesa Abel Mkubi

Amesema kuwa katika kuhakikisha kuwa kila mmoja anakuwa na bima kuna mambo muhimu yanayozingatiwa katika muswada kama kuwa na kaya ya watu 6 ambayo itaundwa na mwanachama mchangiaji, mwenza na wategemezi wasiozidi wanne.

“Kati ya mambo ambayo muhimu yanayozingatiwa katika muswada ni utekelezaji wa ufungamanishwaji utafanyika kwa awamu kwa makundi ya kimkakati.Awamu ya kwanza 2023-2026 makundi yatakayofungamanishwa ni pamoja na wageni wanaoingia nchini na wanafunzi wa vyuo vikuu.

“Awamu ya pili 2026-2028 sekta isiyo rasmi kupitia leseni za biashara, udereva, bima za vyombo vya moto na awamu ya tatu 2029-kuendelea utekelezaji wa bima ya afya kwa wote kwa ulazima,” amesema.

Waziri wa Afya Ummy Mwalimu akiteta jambo na Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania TEF Bw. Deodatus Balile mara baada ya kufungua kikao kazi Cha majadiliano kuhusu rasimu ya Muswaada mpya wa bima