Na Egbart Rwegasira, JamhuriMedia, Missenyi
Halmashauri ya Wilaya Missenyi mkoani Kagera iko kwenye hatua za mwisho kuanza ujenzi wa soko kubwa litakalounganisha wafanyabiashara wa Afrika Mashariki katika Eneo la Bunazi Kibaoni.
Akiwasilisha taarifa ya upembuzi yakinifu na usanifu wa soko kwa madiwani wa Halmashauri ya Wilaya Missenyi Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Stet International (T) Ltd Bwana Shedrack Wellin Willilo amesema kuwa soko litakalo jengwa litakuwa la kisasa katika ukanda wa Afrika mashariki na limeandaliwa kwa kuzingatia ukuaji wa mji,mahitaji ya biashara za mpakani kwa wafanyabiashara wa ndani na nje ya Nchi.
Ameongeza kuwa ujenzi wa soko utagharimu takribani shilingi bilioni tano na muda wa ujenzi unatarajiwa kuwa miaka miwili ili kukamilisha majengo ya maduka zaidi ya 300 ya yatakayopangiliwa ili kukidhi vigezo vya migahawa,mabenki, baa, maegesho ya magari ,kituo cha daladala na miundombinu mingine inayohitajika
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halimashauri ya Wilaya Missenyi wakili John Paul wanga amesema kuwa kati ya shilingi bilioni tano zinazohitajika kwa ajili ujenzi wa soko hilo tayari wameandaa shilingi bilioni 1.7 kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa mradi
Wakili Wanga ametoa wito kwa jamii nzima ya wilaya ya Misseny kujiandaa kupokea mradi huu ambao utakuwa na manufaa makubwa kiuchumi kwa wananchi pamoja na halmashauri.
Wanga ameongeza kusema anafurahia mshikamano unaooneshwa na balaza la madiwani katika kujadili, kupanga na kusimamia miradi ya maendeleo .
“Nina amini hakuna wilaya inaweza kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo pasipo mshikamano wa viongozi, ninachojivunia hapa Missenyi ni umoja wetu na hili litatuwezesha kuifanya missenye ipige hatua kubwa zaidi kimaendeleo” alisema Wanga.