Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia, Dodoma

Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi katika mwaka wa fedha,2022-2023,imetenga Sh 4.65 bilioni kwa ajili ya kuboresha na kuongeza uzalishaji katika ranchi za Kongwa na Mzeri.

Mtendaji Mkuu wa Kampuni za Ranchi za Taifa- Narco,Profesa Peter Msofe amesema hayo wilayani Kongwa wakati wa ziara ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi ya kukagua utendaji kazi wa Kampuni ya Narco Kongwa.

Amesema fedha hizo zilitengwa kwa ajili ya kununulia ng’ombe wazazi,vifaa vya shamba na uchimbaji wa visima virefu.

Malengo ya Narco ni kuendeleza Narco,kuzalisha mifugo bora,kuzalisha malisho,kununua mifugo kutoka kwa wananchi na kisha kuinenepesha,kuhifadhi mazingira na Kongwa kuwa ranchi ya mfano,”amesema.

Kwa upande wake Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulega ametoa maagizo matatu kwa  kampuni ya Ranchi za Taifa (Narco) ikiwemo    kuhakikisha malisho ya mifugo yanapatikana  kwa wafugaji.

Akizungumza wakatí iwa ziara yake ya kukagua utendaji kazi wa Narco Kongwa, amesema  ni aibu ng’ombe waliopo katika ranchi mbalimbali kukonda kwa kukosa malisho wakati ranchi hizo zina maeneo makubwa ya kuzalisha malisho.

Kutokana na hali hiyo amemuagiza  Mtendaji Mkuu wa  Narco,Profesa Peter Msofe kuhakikisha malisho yanapatikana katika ranchi zote zilizopo nchini.

Waziri Ulega amesema malisho hayo ni lazima yajitosheleze ikiwa  pamoja na kuwauzia wananchi na kusafirisha nje ya Nchi.

“Majani yanapaswa kuandaliwa,tunataka mfugaji akimka asubuhi ajue anapata wapi malisho,ule ufugaji wa kizamani sitaki na hapa Narco nyinyi mtakuwa shamba darasa kuhakikisha malisho yanapatikana,”amesema Waziri Ulega.

Pia,ameitaka Narco kuhakikisha nyama inayozalishwa katika ranchi za Taifa zinakuwa na ubora wa kukidhi soko la kimataifa.

“Kiasi tunachosafirisha  nje ya Nchi  ni kidogo,ni lazima tuweke mikakati tuuze tani 50,000 hadi 100,000 ifikapo 2024 au 2025 tuna maeneo ya kufanya nyama iwe bora kama hapa Narco Kongwa,”amesema Ulega.

Pia ameitaka Narco kunenepesha mifugo iliyopo katika ranchi mbalimbali nchini.

Waziri Ulega amesema Serikali itaendelea kuwekeza kwa kuboresha ranchi zilizopo nchini kwa kuhakikisha madume yanapatikana ili kupata mbegu bora.