📍NIRC:Nzega, Tabora
Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC) imekabidhi awamu ya tatu ya utekelezaji wa Mradi wa Umwagiliaji wa Skimu ya Idudumo, wenye thamani ya zaidi ya Sh. bilioni 36, kwa Mkandarasi Kampuni ya Mkwawa Logistics and Construction Limited.
Mradi wa Idudumo unalenga kuongeza eneo la umwagiliaji kutoka hekta 300 hadi hekta 1,550 ambao utakapokamilika utanufaisha wakulima zaidi ya 5,000.
Mradi huo unalenga kuongeza uwezo wa bwawa hilo kutoka lita bilioni 2.5 kwa sasa hadi lita bilioni 9, baada ya kukamilika; hatua itakayowezesha kilimo cha uhakika kwa misimu miwili kila mwaka.

Akizungumza wakati wa makabidhiano ya mradi huo, Mhandisi wa Umwagiliaji Mkoa wa Tabora, Mhandisi Martin Mgangaluma amesema Kazi kubwa zinazoendelea ni pamoja na ujenzi wa tuta la bwawa lenye urefu wa mita 1,000, barabara za mashambani, mifereji ya umwagiliaji, maghala ya mazao, nyumba za meneja wa skimu, na mabirika ya mifugo.
“Umwagiliaji ni kilimo cha uhakika, na mradi wa Idudumo utasaidia wakulima wa vijiji vya Idudumo, Mwanzori, Mwagedeli, Kitengwe, na Iduguta kuongeza usalama wa chakula na kipato cha familia zao.”, ameongeza Mgangaluma
Kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Mkuu wa wilaya ya Uyui Mohamed Musa Mtuliakwalu, amesema serikali imedhamiria kuwaondelea umasikini watu wa nzega, kupitia utekelezaji wa Mradi wa Umwagiliaji wa Idudumo.

“Leo tunaenda kuuaga umaskini kupitia utekelezaji wa mradi huu tunao kabidhi kwa mkandarasi, ambaye yupo tayari kwa utekelezaji.Moja ya faida za mradi huu ni kuzalishwa kwa ajira za kudumu, kupitia kilimo cha umwagiliaji na kukua kwa shughuli za biashara”, amesema Mkuu huyo wa wilaya
Kwa upande wake,Mwenyekiti wa kijiji cha Idudumo, Wande Makundula, ameishukuru serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwaletea fedha nyingi za kutekeleza mradi wa Umwagiliaji katika kijiji chao.
“Nipo hapa kushuhudia utiaji saini utekelezaji wa mradi wa umwagiliaji wa Skimu yetu ya Idudumo, awamu ya tatu na sasa wananchi wetu wataweza kwenda kulima zaidi ya mara tatu”, amesema Wandeu,” amesema.







