Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Lindi
Kuanzia Oktoba, 2023 hadi kufikia Mei, 2024 Tanzania ilikumbwa na kadhia ya mvua kubwa zilizotawala zikichangiwa na tukio la asili la hali ya hewa El-Nino pamoja na Kimbunga Hidaya lililoathiri hali ya hewa nchini na kusababisha athari hasi kwa wananchi kukosa makazi, vifo, magonjwa ya milipuko, uharibifu wa miundombinu ya barabara pamoja na madaraja.
Katika eneo la Miundombinu, Barabara za Mkoa wa Lindi ziliathirika kwa kiasi kikubwa kutokana na madhara ya mvua hizo zilizonyesha mfululizo ambapo hata hivyo Serikali inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt Samia Suluhu hassan ikatoa fedha jumla ya Shilingi za kitanzania bilioni 19 kwa ajili ya matengenezo ya dharula na kurejesha mawasiliano kwa haraka.
Akizungumzia Ofisi kwake Mkoani Lindi, Msimamizi wa Kitengo cha Mipango wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Lindi Mhandisi Jastas Mpenihaka amesema kuwa kiasi cha Shilingi bilioni 13 zimetumika kwa ajili ya matengenezo ya dharula kwa kujaza mawe, vifusi na kuweka makalavati ya plastiki katika barabara kuu katika maeneo mbalimbali ya Somanga Mtama, Kipwata, Mikereng’ende, Matandu, Lingaula, Mbanga na Mbwemkuru.
Amesema kiasi cha Shilingi bilioni 6 zimetumika kwa ajili ya matengenezo ya dharula kwa kujaza mawe, vifusi na kuweka makalavati ya plastiki katika baadhi barabara Mkoa kwa barabara ya Nangurukuru – Liwale, Liwale – Nachingwea na Tingi – Kipatimu.
Naye, Msimamizi wa Kitengo cha Miradi ya Maendeleo TANROADS Mkoani Lindi Mhandisi Fred Sanga amesema kuwa mvua za El-Nino pamoja na kimbunga Hidaya ziliathiri maeneo mengi katika barabara za mkoa wa lindi ambapo athari kubwa zaidi ilikuwa katika barabara za mikoa na barabara kuu hususani maeneo ya Somanga-Mtama, Mikereng’ende, Mbwemkulu, na Kipwata.
Amesema, kwa kuwa matengenezo hayo ya dharula yalikuwa ni suluhisho la muda mfupi kwa ajili ya kurejesha mawasiliano; Serikali inaendelea na mkakati kabambe wa suluhisho la kudumu kupitia mdau wa maendeleo Benki ya dunia wa kujenga madaraja katika maeneo yote yaliyo athiriwa na mvua hizo za El-nino na kimbunga Hidaya.
Mhandisi Sanga amebainisha kuwa katika mkakati huo kabambe kupitia Benki ya Dunia, serikali inatarajia kutumia jumla ya Dola milioni 55 sawa na takribani Shilingi za kitanzania bilioni 146 kwa ajili ya ujenzi wa madaraja hayo.
Kwa mwaka wa fedha 2024/25 kwa kauli moja Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania liliidhinisha na kupitisha bajeti ya Wizara ya Ujenzi na bajeti kuu ya Serikali, na wakala ya barabara Mkoa wa Lindi kupitia Wizara ya Ujenzi imetengewa jumla ya Shilingi za kitanzania bilioni 11.340 kwa ajili ya matengenezo na Shilingi bilioni 2.743 kwa ajili ya miradi ya maendeleo kwa barabara za mikoa.