Bilionea na mfanyabiashara wa India aliyetambulika kimataifa, Ratan Tata (86) amefariki dunia Jumatano usiku baada ya kuugua kwa muda mrefu na kulazwa katika hospitali ya breach candy.

Taarifa ya kifo chake imetolewa na Kampuni ya Tata aliyoiongoza kwa zaidi ya miongo miwili.

Tata Group ni moja ya makampuni makubwa zaidi nchini India, yenye mapato ya kila mwaka yanayozidi Dola za Kimarekani Bilioni 100 (£76.5bn).

Mwenyekiti wa sasa wa Tata, Natarajan Chandrasekaran amemuelezea Bilionea huyo kwamba alikuwa ‘kiongozi wa kipekee.’

Taarifa iliyoshtua na kushangaza wengi ni ile ya kuwa Bilionea huyo hakuwahi kuoa wala kuwa na mtoto maishani mwake, aliwahi kufichua kuwa alijaribu kupenda zaidi ya Wanawake wanne ambao alikaribia kuwaoa, lakini hakufanikiwa kwa kile alichodai kuwa ni kazi kuchukua sehemu kubwa ya muda wake pamoja na kufurahia uhuru wa kutokuwa na wasiwasi kuhusu hisia za mtu mwingine au mahangaiko ya mtu mwingine.

Tajiri huyo aliwahi kuhojiwa na kuulizwa kwanini hajaoa ambapo alijibu.

“Msururu mzima wa mambo umenizuia kuoa, muda, kazi kuchukua sehemu kubwa ya muda wangu kwa wakati huo, Nilikaribia kuoa wakati fulani, lakini haikuwezekana.”

“Kuna nyakati nyingi ambazo nilijihisi mpweke kwa sababu ya kutokuwa na mke au familia ingawa wakati fulani nilifurahia uhuru wa kutokuwa na wasiwasi kuhusu hisia za mtu mwingine au mahangaiko ya mtu mwingine”

Serikali ya Maharashtra nchini India imepanga kumfanyia Bilionea huyo mazishi ya kiserikali.

Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi, pamoja na watu wengine mashuhuri wakiwemo Salman Khan, Ajay Devgn waliomboleza kifo cha Bilionea huyo.