Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Mererani
Rais Samia Suluhu Hassan ameombwa kuingilia kati, mgogoro wa kufungwa njia ya mgodi wa bilionea Saniniu Laizer ambao mwaka 2020 ulivunja rekodi ya kutoa madini makubwa zaidi ya Tanzanite tangu kugunduliwa madini hayo miaka zaidi ya 50 iliyopita .
Kutokana na kufungwa njia ya mgodi huo, tangu Desemba 10, 2023 uliosajiliwa ML 543/2015 vijana 580 waliokuwa wanafanyakazi wamekosa ajira huku, pia serikali ikipoteza mapato ikiwepo kodi zaidi ya millioni 500 hadi sasa.
Juni 23 mwaka 2020 Laizer alitangazwa kuvunja rekodi ya upatikanaji madini Mererani, baada ya kupata mawe ya madini makubwa moja likiwa na kilo 9.27 na jingine kilo 5.103 ambayo yalinunuliwa na serikali kwa zaidi y ash 7.8 bilioni.
Mchimbaji huyo, baadae alipata jiwe jingine lenye uzito wa kilo6.33 na kuiuzia serikali kiasi cha sh 4.86 bilioni na katika mauzo ya madini hayo makubwa, serikali iliweza kupata kodi na malipo mengine zaidi y ash 800 milioni.
Hata hivyo, tangu kupatikana madini hayo, mchimbaji huyo, alikuwa akifuatiliwa na wachimbaji wengine na kutafuta njia ambayo ametumia kufikia madini hayo, lakini hata hivyo wamekuwa wakikwama kwani amechimba zaidi ya kilomita 1.5 kufuata mikondo ya madini na sasa waendeshaji wa mgodi wa Kitalu C wamevamia na “kuteka” njia ya mgodi huo na kudai ipo katika eneo lao.
Bilionea Laizer akizungumzia kupokonywa njia ya mgodi wake, amesema bado anaimani kubwa na Serikali itamtendea haki kwani ametumia mabilioni ya fedha kuchimba madini katika njia hiyo na amekuwa akishirikiana na serikali kwa miaka yake yote ya uchimbaji wake.
“Mimi napenda haki, tangu nimeanza kuchimba nimekuwa na Serikali na maafisa wa madini wanajua njia hii ambayo nachimba miaka yote ,hawajawahi kusema nivunja sheria. Kwani tumekuwa nao, kodi nimekuwa naongoza kwa kulipa na kusaidia jamii hadi kujenga shule sasa ambacho kimetokea namshitakia Mungu lakini najua haki yangu ipo siku itapatikana”amesema.
Meneja msaidizi wa mgodi huo, Paulo Jacob amesema njia muhimu ya mgodi huo, ambao ulikuwa unazalisha imefungwa na kampuni ya Franone Minning and Gems Ltd, ambayo imekodishwa na serikali kuendesha eneo la kitalu C.
Jocob amesema wameshangazwa na kufungwa njia ya mgodi huo, ambao ulikuwa umbali za zaidi ya mita 700 chini ya ardhi,kwani hawajawahi kutobozana na mgodi wa KItalu C na hawajawahi kuna na mgogoro kwa miaka zaidi ya mitano.
“Sisi tumeanza kuchimba muda mrefu, lakini ilikuwa Jumapili usiku Desemba 10, mwaka jana, wachimbaji wa Franone walivamia mgodi wetu, baada ya kupitia katika mgodi ya Tanzanite Explores Ltd ambao tunapakana nao”amesema.
Amesema baada ya kuvamia mgodi huo, waliziba njia na wamezua vifaa vyao vya kazi na mashine zote, vifaa ambavyo ni mashine za kuingiza hewa mgodini( moter 6, Gear box 6, blower,Diggers,mfumo wa waya za umeme, nyundo, tindo na vingine kadhaa vikiwa na thamani ya zaidi ya sh 500 milioni.
Amesema licha ya kuandika barua za malalamiko, ofisi za madini hadi Wizara ya Madini bila majibu na Februari 29, mwaka huu, walituma barua nyingine kwa Afisa madini mkazi Mererani, Nchagwa Marwa kutaka kupatikana suluhu ya mgogoro huo hawajawahi kuhojiwa wala kupewa majibu yoyote.
“Hawataki kujibu barua na wanatujibu kwa maneno tukae kumalizana na Franone sasa imekuwa ngumu kupata suluhu ya mgogoro huu”amesema.
Mwenyekiti mtahafu wa chama cha wachimbaji madini Mererani, Jeremiah Sumari amesema anaomba Serikali kutenda haki katika mgogoro huo na kujali maisha ya maelfu ya wakazi wa Mererani ambao sasa wanataabika kutokana na kukosa kazi ya kuchimba madini.
Afisa Madini mkazi Mirerani, Nchagwa Marwa amekiri kupokea barua ya malalamiko ya Bilionea Saniniu Laizer lakini hata hivyo,alisema suala hilo linashughulikiwa na Katibu wa Tume ya Madini.
“Mimi sio msemaji wa jambo hili, naomba mumtafute Katibu Tume ya Madini ndio anaweza kuzungumzia ”amesema.
Baadhi ya wachimbaji wadogo na wakazi wa Mererani, wameomba Rais kuingilia kati kutatua mgogoro huo, kwani sasa mji wa Mererani, unakufa kutokana na vijana zaidi ya 1000 kukosa ajira, kukosekana fedha na hivyo wizi kuibuka.
Wakazi wa Mererani Zaituni Said amesema wanawake na vijana wamekuwa waathirika wakubwa baada ya kufungwa migodi ya wachimbaji wadogo ambayo inazalisha kwa tuhuma kuwa inachimba eneo la kitalu C.
“Tunamuomba mama Samia Rais wetu, aingilie kati kumaliza mgogoro huu, kwani tunajua kuna vigogo wapo nyuma ya mgogoro huu kwa maslahi yao, mji wa Mererani unakufa, wizi, umeongezeka, Wanawake wametelekezewa familia kwa sababu hakuna fedha tena:”amesema.
Kanaeli Minja amesema kwa miaka yote mji wa Mirerani unategemea wachimbaji wadogo lakini tangu migodi yao kufungwa kwa tuhuma za kuchimba eneo la kitalu C, maisha yamekuwa magumu sana Mererani.
“Tunalia na Rais kwani tunajua kuna watu wapo nyuma ya mgogoro huu, mbona hawa ambao wanabebwa hatuelezwi hata kodi ambayo wanalipa serikalini, hakuna mapato yanayojulikana, huyo Laizer ndiye dunia nzima wanajua amevunja rekodi ya kupata madini makubwa hao wanaobebwa madini yao yapo wapi”amesema.
Amesema wanawake wa Mererani ndio waathirika wakubwa na wanajipanga kufanya maandamano ha Amani hadi mgodini ili kulia haki ipatikane kwa wachimbaji wote na wanawake na vijana wanufaike kuliko sasa mji wa Mererani umegeuka magofu, watu wanahama kutokana na hali ngumu ya maisha.
Mchimbaji wa mgodi huo, Erick Sekawa kufungwa kwa njia ya mgodi huo, imeaathiri sana kwani wanashindwa kuendesha familia na wanashangazwa na ukimya wa Wizara ya madini kwani tangu tukio kutokea hadi sasa hawajawahi kwenda katika mgodi huo kupima na kujua ukweli.
“Tunajua ni “mchezo mchafu” lakini tunaumia sisi vijana tunashindwa kusomesha watoto, maisha yamekuwa magumu sana”amesema.
Wachimbaji Saimon Siriya na Sinyoki Laizer, wameiomba Serikali kuingilia kati mgogoro huo ili kuokoa maisha ya maelfu ya watu, kuliko kutetea mgodi mmoja ambao haunufaishi wananchi wengi.
“Tunaomba Serikali ije kukaa na wachimbaji wadogo, kutatua migogoro Mererani imekuwa shamba la bibi sisi, wakazi wa Mererani hatunufaiki na madini kwa sasa”amesema.