Kampuni za bilionea raia wa Marekani, Dan Friedkin, zilizonaswa kwenye kashfa ya ukwepaji kodi, zimeweka Sh bilioni 50 kwenye akaunti maalumu ya Serikali ya Tanzania.

Habari za uhakika zinaonyesha kuwa pamoja na kulipa kiasi hicho, kuna fedha nyingine nyingi zilizoingizwa kwenye akaunti hiyo kama sehemu ya malipo kutokana na ukwepaji kodi mbalimbali.

Kashfa ya ukwepaji kodi nchini Tanzania imeitikisa Friedkin kwenye masoko ya hisa, hata kwenye mpango wake wa kutaka kuinunua Klabu ya soka ya As Roma ya nchini Italia kwa dola bilioni 1 za Marekani (takriban Sh trilioni 2.2).

Malipo hayo ni utekelezaji wa ahadi iliyotolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni za Friedkin, Jean-Claude McManaman, kwenda kwa Kikosi Kazi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu kinachochunguza kashfa ya ukwepaji kodi.

Katika barua hiyo ya Novemba 8, mwaka huu [angalia kielelezo uk.1), McManaman alisema Sh bilioni 5 zinawekwa kwenye akaunti hiyo wakati ambao bado mjadala wa uchunguzi kuhusu kiwango halisi cha kodi wanachodaiwa Friedkin ukiendelea.

Anaihakikishia serikali kuwa kampuni za Friedkin zitaendelea kutii sheria za nchi, na kwamba kukubali kwao kuweka kwenye akaunti kiasi hicho cha fedha kunathibitisha dhamira hiyo.

Kwenye barua anaeleza matumaini yake ya kuona wakurugenzi waliopokwa hati za kusafiria wanarejeshewa na wanaondolewa zuio la kusafiri nje ya Tanzania.

Msemaji wa kampuni za Friedkin, McManaman, mara zote amegoma kuzungumza na JAMHURI hata baada ya kuandikiwa maswali.

Wakurugenzi wanaokadiriwa kuwa sita walipokwa hati hizo kama sehemu ya mkakati wa kuhakikisha kuwa hawakimbii wakati huu ambao serikali inafanya uchunguzi wa tuhuma za ukwepaji kodi kwa kampuni hiyo na nyingine nchini.

Mbinu za ukwepaji kodi unavyofanywa na kampuni za bilionea Mmarekani, Friedkin, zimefichuka baada ya kubainika kuwa kwa miaka zaidi ya 30 serikali imekoseshwa mabilioni ya shilingi kupitia udanganyifu kwenye mishahara, uuzaji na ununuzi wa mali zikiwamo hoteli.

Nchini Tanzania, baadhi ya kampuni za Friedkin ni Tanzania Game Tracker Safaris Ltd (uwindaji wa kitalii), Wengert Windrose Safaris (Tanzania) Ltd (uwindaji wa kitalii), Ker & Downey Safaris (Tanzania) Ltd (utalii wa picha), Northern Air Ltd (usafiri wa anga), Mwiba Holding Ltd (ranchi ya wanyamapori na utalii) na The Friedkin Conservation Fund (uhifadhi na maendeleo ya jamii).

Kikosi Kazi kilichoundwa na Ofisi ya Waziri Mkuu kimebaini mwanya wa ukwepaji kodi ambao ni kupitia malipo ya mishahara na marupurupu manono wanayolipana wawekezaji hao.

Kwa kutumia akaunti zilizofunguliwa nje ya nchi (offshore accounts), Friedkin wanatuhumiwa kutumia kigezo cha kuajiri wataalamu wa kigeni ili kukwepa kodi. Mwaka 2008 fedha zilizowekwa kwenye akaunti hizo ni dola 963,879 za Marekani. Kwa kiwango cha sasa cha kubadilishia fedha cha wastani wa dola moja ya Marekani kwa Sh 2,300; hiyo ina maana mwaka huo fedha zilizohamishwa kwa mbinu hiyo ni Sh bilioni 2.216. 

Mwaka 2009 dola 849,109 za Marekani (Sh bilioni 1.952) za mishahara ziliingizwa kwenye akaunti hizo; na mwaka 2010 kiwango hicho kilikuwa dola 578,798 za Marekani (Sh bilioni 1.331). Hii ina maana kwa miaka mitatu pekee kiwango cha fedha kilichohamishwa bila kukatwa Kodi ya Ajira (PAYE) na Kodi ya Uendelezaji Ufundi Stadi (SDL) ni Sh bilioni 5.499 ambazo kwa miaka 33 ni Sh bilioni 181.467.

Akaunti hizo zimefunguliwa katika Visiwa vya Cayman, Cyprus, Mauritius na Uswisi. Kampuni ya Kitanzania (jina tunalo) imekuwa ikishirikiana na kampuni nyingine za kimataifa kufungua akaunti mbalimbali za wafanyakazi wa kampuni za Friedkin. Baadhi ya washirika hao ni CIM Corporate Services iliyopo Mauritius.

Mambo mengine yaliyodaiwa kufanywa na kampuni za Friedkin ni ubaguzi wa mishahara kati ya wafanyakazi wageni na wenyeji bila kujali uwezo wao kitaaluma. Wafanyakazi wageni wanalipwa kiasi kidogo cha fedha hapa nchini, ilhali kiwango kikubwa kikiwekwa kwenye akaunti zao zilizofunguliwa ughaibuni.

Mkurugenzi Mkuu, Jean-Claude McManaman, anapokea mshahara wa Sh milioni 50 kwa mwezi. Mkurugenzi wa Oparesheni wa Mwiba Holdings Limited, Russel Hastings analipwa mshahara wa Sh milioni 49 kwa mwezi. Sehemu kubwa ya mshahara huo haikatwi kodi kwa kuwa huingizwa moja kwa moja kwenye akaunti zilizoko ughaibuni. Ofisa Mkuu wa masuala ya Fedha wa Kerr & Downey Limited, Nick Stubbs mshahara wake ni Sh milioni 43. 

“Jambo la kusikitisha ni kuwa sehemu kubwa ya mishahara hii inalipwa offshore, kwa hiyo haikatwi kodi wala tozo, lakini kwa wafanyakazi Watanzania ambao wanalipwa kidogo, kodi zote wanakatwa,” kimesema chanzo chetu.

Mchanganuo unaonyesha kuwa kati ya mwaka 2013 hadi mwaka huu (2019), Hasting pekee ‘amekwepa’ kodi ya wastani wa Sh milioni 840; na Stubbs ameikosesha serikali Sh milioni 744 kama kodi na tozo kutoka kwenye mshahara wake pekee.

Wakati wageni hao wakilipwa hivyo, kwa Watanzania walio kwenye ngazi ya umeneja mshahara wa kila mmoja ni wastani wa Sh milioni 9 pekee kwa mwezi; na baada ya makato hubaki na wastani wa Sh milioni 5. 

Wafanyakazi wa ngazi ya chini kama vile wahudumu wanalipwa mshahara wa wastani wa Sh 400,000 hadi Sh 800,000 kwa mwezi na wanakatwa kodi zote za PAYE, SDL, WCF na NSSF. Pia imebainika kuwa kwa miaka yote 30 hakuna Mtanzania aliteuliwa kushika nafasi ya juu kwenye menejimenti ya kampuni za Friedkin hapa nchini.

Wawindaji Bingwa (PH) raia wa kigeni wanalipwa dola 12,000 za Marekani (Sh milioni 27.6) kwa mwezi; lakini ‘waswahili’ wanaambulia dola 1,000 za Marekani (Sh milioni 2.3) tu kwa muda kama huo. 

Kwa miaka yote hiyo, wafanyakazi wataalamu kutoka nje walioajiriwa na kampuni za Friedkin wamekuwa wakilipwa sehemu kubwa ya mishahara yao kwenye benki zilizo ughaibuni ili pamoja na mambo mengine, wasilipe kodi na tuzo mbalimbali za kisheria hapa nchini.

Sehemu zinazotajwa kupelekwa fedha hizo ni katika Visiwa vya Bahamas kwenye taasisi za fedha za Adventure Services na AHIL Trust. Hayo yakiendelea, uchunguzi umeanza kwenye akaunti za Friedkin zilizoko Uswisi na Visiwa vya Cayman.

Wanaotajwa kuwa wanahusika kuidhinishaji fedha kutoka ofisi kuu za Friedkin zilizoko Houston Texas, Marekani ni Rais wa kampuni za Friedkin, Dan Friedkin; Mtendaji Mkuu, Marcus Watts; na Mwanasheria Mkuu, Kimberly Jacobson.

Oktoba 25, mwaka huu Kikosi Kazi hicho kilikutana na wawakilishi wa kampuni za Friedkin jijini Arusha. Kwa upande wa Friedkin, waliohudhuria ni Jean-Claude McManaman, Lemmy Bartholomew, Wilfred Mawalla, Elibariki Lucas, Nick Stubbs, Russel Hastings na Alex Rechsteiner. 

Taarifa kutoka kwenye kikao hicho zinasema kampuni za Friedkin zinatuhumiwa kwa makosa ya ukwepaji kodi kupitia malipo ya wakurugenzi; na ukwepaji kodi kwenye mikopo na uhamishaji fedha ndani ya kampuni. 

Makosa mengine ni kuajiri wataalamu kutoka nje ya nchi wanaofanya kazi kama washauri, lakini wakiwa hawana vibali na  wala sifa za kitaaluma; na imebainishwa kuwa baadhi ya wafanyakazi – wamekutwa wakiwa na mishahara zaidi ya mmoja na kwa viwango tofauti. Pia hakuna makato kwa ajili ya mifuko ya hifadhi ya jamii. 

Jingine ni mikataba mingi kwa wataalamu kutoka nje ya nchi, hasa kwa Jean-Claude ambaye amekutwa akiwa na barua ya ajira, lakini ana mkataba mwingine kama mshauri.

Kwenye kikao hicho, Friedkin waliomba wapewe hati zao za kusafiria kwa kile walichodai kuwa baadhi yao wana masuala ya kifamilia huko kwao na wengine wanakwenda katika matibabu na masuala ya kibiashara.

Walikwama kwa maelezo kuwa hilo litawezekana tu endapo watuhumiwa hao watakuwa tayari kuweka kiasi cha fedha kama dhamana.

Friedkin wakawa tayari kutoka Sh milioni 100 na baadaye Sh milioni 200, lakini Kikosi Kazi kikagoma kukubali ofa hiyo. Badala yake, wakaelezwa waweke dhamana ya Sh bilioni 5 kwenye akaunti maalumu ya serikali wakati majadiliano kuhusu kiwango halisi cha kodi kilichokwepwa kikikokotolewa.

Mkurugenzi Mtendaji wa Friedkin Group Company Ker and Downey Tanzania Ltd., Jean-Claude McManaman, anatajwa kukiri baadhi ya tuhuma za ukwepaji kodi.

Wakati wataalamu na wakurugenzi wa Friedkin wakizuiwa kusafiri nje ya nchi, ‘mshauri’ mkuu wa Friedkin Group, Fabia Bausch kutoka Chem Chem Safaris, yeye aliwahi na akafanikiwa kukimbia.

Taarifa za ukwepaji kodi zimewafanya baadhi ya mashabiki na wamiliki wa AS Roma waanze kuhoji uhalali wa bilionea huyo kununua klabu yao.

Mtazamo wao ni kuwa fedha zinakazotumika kununua klabu yao ni sehemu ya matokeo ya ukwepaji kodi uliofanywa kwa nchi maskini yenye mahitaji makubwa ya fedha.

Mapambano dhidi ya rushwa na ukwepaji kodi ni sehemu ya ahadi zilizotolewa na Rais John Magufuli alipozindua Bunge mjini Dodoma mwishoni mwa mwaka 2015.

Tangu wakati huo vita dhidi ya vitendo hivyo imeendeshwa kwenye sekta takriban zote bila kujali mhusika ni nani au analindwa na nani.

Miaka kadhaa iliyopita, kampuni za Friedkin, kwa kuwatumia maseneta nchini Marekani, ziliishitaki Serikali ya Tanzania kwa Rais Barack Obama, zikidai kupokwa vitalu vyake vya uwindaji; jambo ambalo lilipingwa vikali na serikali.

Kwa miaka mingi Friedkin imekuwa na uswahiba na viongozi wengi wakuu wa serikali, hata kufikia hatua ya kutoa ndege zake kwa ajili ya kampeni za ubunge za baadhi ya mawaziri wa wakati huo.