Tajiri mwenye ukwasi wa kutisha anayeishi jijini Dar es Salaam, anaonekana kuwa wa kwanza kumjaribu Rais John Pombe Magufuli, aliyesema hajaribiwi, uchunguzi wa JAMHURI umebaini.

Hali hii imetokana na tajiri huyo kuamua kulitumia Jeshi la Polisi kutekeleza matakwa yake, na hata baada ya Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, kuingilia, tajiri huyo ameendelea kuwa ‘ngangari.’

Mwekezaji wa kampuni ya Petrofuel amewasilisha malalamiko Ofisi ya Makamu wa Rais akieleza kunyanyaswa na tajiri huyo ‘anayelituma’ Jeshi la Polisi kufanya atakacho, lakini hadi sasa pamoja na Polisi kumwomba radhi mwekezaji, bado wameendelea kutekeleza matakwa ya tajiri huyo.

Maelekezo ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, yako njiapanda kwani polisi waliosema wangeyafanya kwenye mkutano huo na baadaye katika mkutano kati ya polisi na wadau, hadi sasa hakuna kilichotekelezwa. 

Kamishna wa Kanda Maalumu ya Polisi Dar es Salaam, Simon Sirro, sasa amegeuka jiwe la chumvi kwa kukaidi ahadi aliyoitoa mbele ya Waziri Mkuu, kuwa angeiomba radhi Kampuni ya M/S Petrofuel (T) Ltd na kuwaadhibu askari waliohusika kutumwa na mfanyabiashara, lakini hadi sasa hajatimiza lolote tangu mwaka jana.

Sirro anadaiwa kutoa amri kwa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) kuvamia, kumwondoa na kuharibu mali za mwekezaji kwa faida ya mfanyabiashara mwenye tambo nyingi hapa nchini kuwa yeye ‘anaimudu’ Serikali.

Habari za uhakika lilizozipata Gazeti la JAMHURI zinaonesha kuwa Sirro alitoa kauli kuwa angeomba radhi kwa niaba ya Jeshi la Polisi katika kikao kilichofanyika mjini Dodoma, Septemba mwaka jana, kati ya Waziri Mkuu, Kampuni ya Petrofuel, mtu anayetuhumiwa kulitumia Jeshi la Polisi kutimiza matakwa yake na Jeshi la Polisi lililowakilishwa na Sirro walipokutana.

Kikao hicho kiliitishwa baada ya JAMHURI kuchapisha taarifa za kuonesha kuwa Jeshi la Polisi nchini limetumika kinyume cha taratibu kufanikisha malengo ya mfanyabiashara binafsi, hali inayoendelea kuikosesha Serikali wastani wa Sh bilioni 3 kila mwezi kama kodi.

Serikali ya Awamu ya Tano ikiwa inahaha kuongeza mapato, kampuni ya Petrofuel inayolipa kodi ya wastani wa Sh bilioni 3 hadi Sh bilioni 4 kwa mwezi, imefungiwa ofisi zake kutokana na mgogoro wa ardhi usioihusu.

Kwa hatua hiyo, Serikali kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), itapoteza kodi hiyo iliyokuwa ikilipwa na kampuni ya Petrofuel (T) Limited.

Petrofuel (T) Limited ni mpangaji katika kiwanja kinachodaiwa kumilikiwa na kampuni ya Educational Books Publishers Limited, kiwanja namba 12B, sehemu ya E.P Lot 20, kilichoko Barabara ya Nyerere jijini Dar es Salaam.

Kampuni ya Educational Books Publishers inamilikiwa na mfanyabiashara Mohamed Suleiman Mohamed (Osama), anayetajwa kuwa na vitegauchumi kadhaa jijini na anayedaiwa kuwa na ushawishi mkubwa kwa maafisa wa Serikali.

Osama ameingia kwenye mvutano wa umiliki wa kiwanja hicho na mfanyabiashara Hasham Kassam, ambaye anadai kuwa ni mmiliki halali wa kiwanja hicho chenye hati Na. 186074/21. Kassam ndiye aliyeingia mkataba wa kukodisha eneo hilo kwa kampuni ya Petrofuel.

 

Mkutano wa Waziri Mkuu

aada ya Waziri Mkuu Majaliwa kufanya kikao na wadau hao walio katika mgogoro kwa nia ya kuumaliza kiutawala na Serikali kuendelea kupata kodi stahiki, imebainika kuwa juhudi za Waziri Mkuu zimegonga mwamba kwani yote waliyokubaliana katika kikao cha pamoja hakuna kilichotekelezwa.

Kama sehemu ya ufuatiliaji, Oktoba 12, 2016, Sirro aliitisha kikao ofisini kwake Dar es Salaam kuhusiana na suala hilo. Kikao hicho kilihudhuriwa na Sirro mwenyewe, Naibu Kamishna wa Polsi, Hezron Gimbi; Gilles Mroto, wakili wa Educational Book Publishers, Wilson Ogunde; mmiliki wa Educational Book Publishers, Mohamed Suleiman Mohamed (Osama); Wakili wa Petrofuel, Dk. Masumbuko Roman Lamwai; na Makamu wa Rais wa Petrofuel, Mshamsham D. Mfuru.

Sirro ndiye aliyeongoza kikao hicho. Alitoa mrejesho kwa wajumbe wa kikao kuwa nia ya kukutana kwao kulitokana na kuondolewa kwa nguvu kwa Kampuni ya Petrofuel (T) Ltd na ISA (T) Limited katika ofisi zao eneo lililotajwa hapo juu kwa kutumia Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU).

Katika mkutano huo, Sirro alikiambia kikao kuwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, aliitisha kikao Dodoma na kutolea uamuzi malalamiko yaliyopokewa na ofisi yake kupitia Ofisi za Makamu wa Rais, hivyo aliitisha mkutano kuwafikishia taarifa ya uamuzi uliofikiwa mjini Dodoma.

“Sirro alikiambia kikao kuwa Manispaa ya Temeke imethibitisha katika mkutano wa Dodoma kuwa ardhi (kiwanja) kinachogombaniwa ni mali ya Educational Book Publishers kwani wamekuwa wakilipa kodi,” amesema mmoja wa watu waliohudhuria mkutano huo.

Katika barua ya Mwanasheria wa Petrofuel, Dk. Lamwai, kwenda kwa Sirro ya Oktoba 18, 2016, yenye Kumb No. PETRO/2016/14, Dk. Lamwai anamkumbusha Sirro kutekeleza ahadi yake ikiwamo kuiomba radhi Kampuni ya Petrofuel na kuwarejesha katika jengo walikotolewa.

“Kamishna Sirro alisema wazi kuwa kuhusishwa kwa polisi katika kuwaondoa [Petrofuel] kwa amri ya Naibu Kamishna wa Temeke, hakukuwa sahihi na bila hati yoyote ya Mahakama.

“Kamishna Sirro alisema kuwa kuondolewa kulikofanyika Juni 24 [2016], kulikuwa kinyume cha sheria. Aliomba radhi kwa niaba ya FFU na Jeshi la Polisi. Aliahidi pia kuchukua hatua za kinidhamu kwa waliohusika.

“Kamishna Sirro alisema pia kuwa amewasiliana na Mahakama; na hakukuwa na amri yoyote kutoka mahakamani iliyoruhusu kuwaondoa [Petrofuel],” inasema sehemu ya barua ya Lamwai inayonukuu kumbukumbu za kikao cha Oktoba 12, 2016.

Pia kwa mujibu wa barua hiyo, Kamishna Sirro alisema polisi hawana jinsi ya kuwarejesha Petrofuel kwenye ofisi zao, kwani kesi ipo mahakamani na kwamba suala la uharibifu wa mali na kutishiwa maisha kwa mke wa Mkurugenzi wa Petrofuel ilikuwa inashughulikiwa na Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP).

Kamishna Sirro pia aliwashauri Petrofuel na Educational Book Publishers kukaa na kushauriana jinsi ya kuondoa mafuta yaliyopo kwenye matangi na ni hatari kwa mazingira na wakazi waliopo maeneo jirani.

Dk. Lamwai anahoji ilikuwaje Sirro akaitisha mkutano haraka haraka baada ya kutoka Dodoma na hata baada ya kujulishwa kuwa wakurugenzi wa Petrofuel ambao ndiyo wenye uamuzi hawakuwapo, aliamua kuendelea na mkutano, suala linalothibitisha kuwa aliitisha mkutano kuwasafisha Educational Book Publishers na Jeshi la Polisi.

JAMHURI haizungumzii uhalali wa nani mmiliki wa kiwanja kwani kuna kesi mahakamani juu ya suala hili na Mahakama ndiyo itakayothibitisha kati ya Hasham Kassam, aliyewapangisha Petrofuel na anayo hati anayoilipia kodi kila mwaka na Tanzania Book Publishers wenye hati ya kiwanja hicho hicho pia, huku nao wakionekana wanailipia ada zote kila mwaka.

Hata hivyo, Lamwai anahoji Sirro amepata wapi mamlaka ya kutangaza ni nani mmiliki halali wa kiwanja kati ya Educational Book Publishers na M/S Hasham Kassam and Sons Ltd – ambao wote wanadai kuwa wanalipa kodi na kesi ipo mahakamani wakitafuta uhalali wa suala hili.

Pia anasema askari anayefahamika kwa jina la Tirumanywa Josephat kutoka ofisini kwa Sirro, alikwenda ofisi za Petrofuel asubuhi kabla FFU hawajafika na watuhumiwa kuwatolea vitu nje, na akasema kuwa mmiliki halali wa kiwanja hicho ni Educational Book Publishers, hali wanayohoji alilenga nini.

Anasema Sirro kudai kuwa polisi hawawezi kuliingilia suala hili si sahihi, kwani kama waliweza kuisaidia Educational Book Publishers kutoa vitu vya Petrofuel ofisini bila kibali cha Mahakama, ni maslahi yapi walikuwa nayo na nini kinawashinda sasa kuirejesha ofisini kampuni hiyo baada ya kubaini kuwa walitenda kosa.

Katika barua hiyo, Lamwai anaeleza maneno yanayoashiria kuwa “Osama” amewatia mfukoni baadhi ya viongozi wa Serikali anaposema: “Educational Book Publishers hawakutaka kurejesha hati za kusafiria za wafanyakazi wa Petrofuel, na walilazimishwa kufanya hivyo baada ya kuhusisha Ubalozi wa India na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ya Tanzania.

“Ukali na majivuno aliyoonesha ndugu Mohamed Suleiman Mohamed dhidi ya maafisa wa Polisi waliokuwa wanasimamia kurejeshwa kwa paspoti alizokuwa anazishikilia, ni wazi inaashiria kuwa haogopi sheria na ana viongozi wa juu wanaomuunga mkono. Kiuhalisia, anaonekana anawadhibiti baadhi ya maofisa wa umma,” anasema Lamwai.

Anasema hakutaja hatua zipi angewachukulia watu zaidi ya 150 walioshiriki kazi haramu ya kuondoa mali za Petrofuel kwenye ofisi walizopanga kihalali na kampuni ya Yono Auction Mart, mawakili Wilson Ogunde na Dk. Lugemeleza Nshalla, walioshiriki shughuli hiyo aliyoiita ya dhuluma.

Dk. Lamwai anahitimisha kwa kusema: “Mkutano huu ulitufanya tuamini kuwa Kamishna Sirro alihusika kwa karibu katika mchakato wote na amesisitiza mtazamo wake mbele ya waliotenda kosa kuwapa imani kuwa hawataguswa na Petrofuel itabaki katika mchakato wa kisheria kwa miaka kadhaa,” anasema katika barua hiyo iliyotolewa nakala kwa Ofisi ya Makamu wa Rais Tanzania, Waziri Mkuu, Katibu Mkuu Kiongozi, Waziri wa Mambo ya Ndani na Waziri wa Sheria na Katiba.

Wengine waliopewa nakala ya barua hii ni Mkuu wa Jeshi la Polisi, Mkurugenzi wa Upelelezi, Mkurugenzi wa Mashtaka na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

 

Sirro azungumza

JAMHURI imemtafuta Kamishna Sirro kuzungumzia utekelezaji wa ahadi aliyoitoa kutokana na mkutano kati yake na Waziri Mkuu, ambapo amesema kuwa suala hilo limekwisha muda mrefu, hivyo haina maana kulizungumzia tena.

Amesema hawezi kuiomba radhi Kampuni ya Petrofuel,  kutokana na kwamba yeye ni Kamishna wa Polisi na kwa mamlaka yake haiwezekani kufanya hivyo.

“Yaani mimi Kamishna unataka niiombe radhi kampuni? Haiwezekani. Kwanza jambo lenyewe tayari limekwisha muda mrefu, nashangaa kulianzisha tena,” anasema Sirro. Hakukubali kusema iwapo kuna hatua alizowachukulia waliohusika katika kuharibu mali za Petrofuel kama alivyoahidi kwenye kikao pia.

Kwa upande wake, Dk. Rugemeleza Nshalla kama wakili wa Educational Book Publishers, amesema hawezi kuzungumza chochote kutokana na kwamba suala hilo lina kesi mahakamani na hukumu bado haijatolewa.

Wakili mwingine, Wilson Ogunde, amesema miongoni mwa uamuzi uliofikiwa katika kikao na Kamishna Sirro baadhi ya wafanyakazi wa Petrofuel waliomba kwenda kufunguliwa ofisi kuchukua hati zao za kusafiria.

Anasema baada ya kuchukua hati hizo, walifunga tena ofisi huku kukiwa na askari kutoka Chang’ombe na wa Kituo cha Kati Dar es Salaam.

Anaeleza kuwa katika kikao cha Kamishna Sirro yeye alikuwa mmojawapo, ambapo alieleza msimamo wa Serikali baada ya Petrofuel kupeleka malalamiko katika Ofisi ya Waziri Mkuu na Makamu wa Rais.

“Baada ya kufanyika uchunguzi wa mgogoro huo, Kamanda Sirro alibainisha kuwa baada ya Serikali kupitia nyaraka zote eneo hilo ni la Educational Book Publishers,” anasema Ogunde.

Ogunde anasema kutokana na shauri hilo kuwa mahakamani, Kamishna Sirro alisema mambo mengine yatapatiwa ufumbuzi mahakamani.

Anasema kuwa kuhusu madai ya Jeshi la Polisi kuwa linashirikiana na upande wa Educational Book Publishers kuiondoa kwa nguvu Petrofuel si kweli, kutokana na siku ya tukio Educatioinal Book Publishers kwenda wao wenyewe.

“Polisi walikuja eneo la tukio baada ya kupata taarifa kuwa kuna mgogoro na walifika kwa ajili ya kuwaondoa watu wa Educational Book Publishers,” anasema Ogunde.

Ogunde anasema kuhusu mafuta, hivi karibuni amepokea barua kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma ya Nishati na Maji (EWURA) ambayo inawataka Petrofuel kutoa mafuta yao katika eneo hilo.

Anafafanua kuwa nakala ya barua hiyo inaeleza kuwa Petrofuel walitakiwa kufika eneo hilo Januari 16 mwaka huu, saa nne asubuhi kuondoa mafuta.

“Barua hiyo wamepewa zaidi ya mara nne na EWURA, lakini mpaka sasa wamekaidi kuyatoa hayo mafuta na wamekuwa wakielekezwa kuyaondoa,” anasema Ogunde.    

Anabainisha kuwa kilichopo upande wa Petrofuel; wamepeleka madai yao mahakamani wakidai kuwa kitendo cha kuwatoa kimewasababishia wao kupata harasa na kuomba warudishwe waendelee na shughuli zao.

“Petrofuel wanawataka  Educational Book Publishers wawafidie wakati huohuo nao Educational Book Publishers wanahitaji fidia ya kupotezewa muda kutoka kwa Petrofuel na wenzake kwa kukaa katika eneo hilo na  kufanya biashara zaidi ya miaka tisa bila idhini ya mhusika,” anasema Ogunde.

JAMHURI imewatafuta upande wa Petrofuel, ambao wamesema wao wameathirika kwa kiasi kikubwa na wanasikitika kuwa hawafanyi biashara, na Serikali inaendelea kupoteza kodi kwa makosa ambayo si yao, hivyo wakaomba ikiwa kuna uwezekano Serikali iingilie kati mgogoro huu.

“Sisi tunaheshimu suala kwamba kesi ipo mahakamani. Tunaendelea kupata hasara. Tungekwishaondoa mafuta, ila kuna taratibu za kimahakama ambazo zinatuhitaji kuzitimiza tusipoteze ushahidi na mwisho wa siku kupoteza kesi, hivyo tutayaondoa mafuta kwa maelekezo ya Mahakama na si vinginevyo,” amesema Afisa aliyetaka asitajwe jina gazetini.

Mohamed Suleiman Mohamed (Osama), alipotafutwa na JAMHURI, alisema kwa ufupi: “Mtafute wakili wangu azungumzie yote hayo.”

JAMHURI imewasiliana na Ofisi ya Waziri Mkuu, ambao waliomba muda kulitolea ufafanuzi suala hili, kwa maelezo kuwa Waziri Mkuu yuko safarini mikoa ya kusini ila watahakikisha Serikali inalishughulikia kwa ukamilifu.

Kampuni ya Petrofuel (T) Limited ilipeleka Mahakama Kuu hati ya kuomba kuzuia kuondolewa katika kiwanja hicho. Suala hilo lilifikishwa Mahakama Kuu. Katika shauri hilo, kampuni hiyo na nyingine ya ISA Limited, zimewashtaki Educational Books Publishers Limited, Wilson Ogunde na Yono Auction Mart and Court Brokers.

Kwa mujibu wa nyaraka za Mahakama, shauri hilo lilisikilizwa na Jaji Lugano Mwandambo katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Julai 21, mwaka jana. Uamuzi wa kutoa au kutotoa hati ya zuio ulitarajiwa kutekelezwa wiki mbili, lakini hadi mwaka huu haujatolewa.

Kampuni hiyo inasema uvamizi na kufunga ofisi zao ulifanywa kwa nguvu na hivyo kusababisha hasara kubwa ya mali na fedha.

“Uamuzi wa kutuondoa katika eneo linalozungumzwa katika shauri hili litatusababishia hasara ya kati ya Sh milioni 200 hadi Sh milioni 400 kwa siku. Waliingia hapa na mashine zinazotumia gesi kukata milango pamoja na makufuli,” inasomeka sehemu ya shauri hilo.

Katika shauri hilo, kampuni ya Petrofuel (T) Limited inasema kuna matangi sita ya mafuta ya dizeli yenye lita 278,000 pamoja na vipuri vya mitambo na magari kwa ajili ya migodi ya madini.

Kampuni hiyo inasema endapo haitaruhusiwa kuokoa mali hizo, itafilisika kutokana na kutopewa fidia na taasisi za kifedha.

“Tunashauri kwamba namna bora ya kushughulikia hayo matangi ya mafuta kunahitajika utaalamu mahsusi ambao hao tunaowashtaki hawana, hivyo matangi hayo yanaweza kulipuka,” inasomeka sehemu ya shauri hilo.

Mmoja wa watumishi wa kampuni ya Petrofuel (T) Limited, ambaye hakupenda kutajwa jina lake gazetini, anasema lilikuja kundi la watu ofisini kwao na kuanza mabishano na mtumishi wa mapokezi, na baadaye Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo alitaka kupatiwa ufafanuzi wa ujio huo, lakini hakujibiwa.

“Mkurugenzi Mtendaji alitaka kupatiwa maelezo ya kina pamoja na kuoneshwa barua zinazowaruhusu kutekeleza agizo hilo, hawakufanya hivyo na badala yake walimsukumia pembeni na kuingia katika ofisi zetu na kuanza kutoa vitu nje, baadaye wakaanza kutoa magari nje kwa kutumia winchi,” anasimulia mmoja wa wafanyakazi wa kampuni hiyo.

Anasema walimpigia simu mwanasheria wa kampuni hiyo baada ya kuwauliza na kubaini kuwa hawakuwa na nyaraka zozote za kuwaruhusu kuiondoa kampuni katika ofisi hizo.

“Baadaye tukampigia Mkuu wa Kituo cha Polisi Chang’ombe, akamtuma mpelelezi wa kituo hicho, ambaye baada ya kuwauliza maswali kuhusu nyaraka zinazowaruhusu kufanya jambo hilo, walianza kuondoka mmoja mmoja.

“Tulishangaa kuvamiwa hapa ofisini, huku wavamizi wetu wakiwa wamesindikizwa na askari polisi wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia…walikuja hapa wakiwa wamesindikizwa na maaskari, tungependa kuona askari wanafuata taratibu za kazi zao, maana alipokuja mpelelezi wa Kituo cha Chang’ombe na kuwahoji walianza kuondoka mmoja mmoja,” anasema mfanyakazi huyo.

Akizungumza na JAMHURI, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, Mroto, alisema anafahamu kuhusu suala hilo, lakini hawezi kulisemea kwa kuwa liko mahakamani.