Dhamira ya Rais John Magufuli, katika kuijenga Tanzania mpya, inaonekana. Anatambua nafasi ya utalii katika uchumi wa nchi yetu.
“Ukitaka kujenga nchi yenye uchumi wa kisasa, huwezi kujenga bila kuwa na ndege na ukitaka watalii lazima uwe na ndege. Tunataka watalii wanaokuja nchini kuja moja kwa moja bila kushuka nchi nyingine ili kuongeza mapato yetu na kukuza utalii”. Haya ni maneno ya Rais Magufuli, wakati akipokea ndege mbili zilizonunuliwa mwaka jana chini ya uongozi wake.
Mwaka mmoja uliopita, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Profesa Benno Ndulu, alisema sekta ya Utalii ndiyo inayoongoza kwa kuliingizia Taifa mapato ya kigeni, ikiwa imeipita sekta ya dhahabu.
Akasema Utalii unaliingizia Taifa dola bilioni 2, dhahabu (dola bilioni 1.7), bidhaa za viwandani (dola bilioni 1.3) na huduma za usafirishaji mizigo ni dola milioni 800. Takwimu hizi ni za mwaka 2015. Sidhani kama kuna mabadiliko makubwa kwenye hizo takwimu.
Mwaka jana, Wizara ya Maliasili na Utalii ilisema Utalii ulikuwa ukiongoza kwenye pato la Taifa kwa kuchangia asilimia 17.5. Kwa maneno mengine, Utalii ndiyo roho ya nchi inayotumainiwa katika kupata fedha za kigeni.
Utalii wa Tanzania ni tofauti na ule unaopatikana katika mataifa mengine kama vile Misri. Huko, mapiramidi na mabaki ya miili ya watawala wa kale na maisha yao ndivyo vinavyoongoza kuwavuta watalii.
Hapa kwetu utalii wetu umejikita zaidi kwenye vivutio vinavyotokana na wanyamapori na ndege, fukwe na mandhari asilia. Mabaki ya majengo ya kale na vivutio vingine ni nyongeza tu kwenye mlolongo huu wa kuwavutia watalii.
Kwa muhtasari, hii unatosha kabisa kutuonesha ni kwa namna gani suala la uhifadhi lisivyostahili kupuuzwa. Mahitaji ya fedha za kigeni ni jambo muhimu mno katika ustawi wa Taifa letu. Malengo na ahadi zilizotolewa na Serikali ya Awamu ya Tano vinaweza visitimie endapo suala la uhifadhi litakosa utashi wa kisiasa.
Uzuri wa nchi yetu tulioushuhudia miaka michache iliyopita, na ambao bado tunaendelea kuufaidi katika maeneo kadhaa ya nchi yetu, ni matokeo ya kazi ya kutukuka iliyofanywa na mababu na mabibi zetu; na baadaye ikaendelezwa na waasisi wa Taifa letu.
Septemba, 1961 Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, aliyasema haya kuhusu uhifadhi:
“Kudumisha uhai wa wanyamapori wetu ni suala linalotuhusu sana sisi sote katika Afrika. Viumbe hawa wa porini pamoja na mapori wanamoishi siyo tu kwamba ni muhimu kama mambo ya kustaajabisha na kuvutia, bali pia kwamba ni sehemu muhimu ya maliasili yetu na ustawi wa maisha yetu katika siku za baadaye.
Kwa kukubali dhamana ya kuhifadhi wanyama wetu tunatoa tamko la dhati kuwa tutafanya kila tuwezalo kuhakikisha kuwa wajukuu na watoto wetu wataweza kufaidi utajiri na thamani ya urithi huu.
Kuhifadhi wanyamapori na mapori waishimo kunahitaji utaalamu maalumu, watumishi waliofunzwa pamoja na fedha. Tunatazamia kupata ushirikiano kutoka kwa mataifa mengine katika kutekeleza jukumu hili muhimu. Kufanikiwa au kushindwa kwa jukumu hilo kutaathiri siyo tu Bara la Afrika pekee, bali ulimwengu mzima.”
Mwalimu Nyerere na wenzake walitambua na kulinda rasilimali hii adhimu. Matokeo yake, leo Utalii unachangia asilimia 17.5 kwenye pato la Taifa.
Mungu alipoumba wanyama na ndege alikuwa na makusudi yake. Ukiacha faida za kiafya; ndege na wanyama ni samani katika bustani hii – dunia. Kuharibu malengo haya ya Mungu ni dhambi. Leo tunapoamua kukaa kimya ilhali tukitazama miti ikimalizwa kwa biashara haramu ya mkaa, tusilalamike tunaposhuhudia joto na ukame. Tusilalamike kukumbwa na baa la njaa! Kwa dhambi hii ya kuharibu mazingira, tunastahili adhabu inayotokana na uharibifu huu wa mazingira.
Rais Magufuli ameonesha dhamira ya dhati ya kuukuza utalii, ndiyo maana ameona aanze na usafiri wa ndege. Muda si mrefu, ndege nyingine mbili – mali ya Serikali zitawasili nchini. Tumeambiwa kuwa ndege moja itakuwa na uwezo wa kubeba abiria 160 na nyingine abiria 242. Hii ni hatua kubwa mno.
Pamoja na nia njema ya Rais wetu, ndege hizi zinaweza zisiwe na kazi ya kufanya endapo suala la kuhifadhi mapori yetu na viumbe waliomo litapuuzwa au litaachwa liwe la watu wachache wenye mapenzi mema na nchi yetu.
Watalii wanakuja nchini kuwaona wanyamapori, ndege na mazingira ambavyo huko kwao vimeshavurugwa na pengine kutoweka kabisa.
Msafara wa nyumbu, pundamilia na wanyamapori wengine kati ya Hifadhi ya Taifa Serengeti nchini Tanzania na Maasai Mara nchini Kenya, ndiyo msafara pekee wa aina hiyo uliobaki katika sayari hii. Huko Amerika misafara ya aina hiyo ilikuwapo, lakini kwa uharibifu wa mazingira na mauaji ya wanyamapori, ilitoweka. Tuna sababu zote za kulinda rasilimali hii kwa manufaa yetu kama nchi, na kwa walimwengu wote.
Miaka ya karibuni kumeibuka ubinafsi wa hatari sana. Magenge ya watu yamekuwa yakijitokeza kwa kasi ya ajabu kabisa kuhakikisha yanahodhi na hatimaye kuharibu kabisa makazi ya wanyamapori.
Majuzi tu tumemsikia Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Simiyu, akimwomba Rais Magufuli aruhusu ng’ombe waingizwe katika Hifadhi ya Serengeti na mapori mengine. Kwa akili ya Mwenyekiti, ng’ombe wana thamani sana kuliko wanyamapori! Fikiria, huyu ni mwenyekiti wa chama chenye Serikali!
Huyu ni miongoni mwa wanasiasa wenye idadi kubwa mno ya ng’ombe. Nyuma ya pazia wanataka waonekane wanawatetea wafugaji, lakini ukweli ni kuwa wao ndiyo wenye ng’ombe.
Wapenda uhifadhi tunampongeza Rais Magufuli kwa msimamo wake wa kupinga wazo hilo. Msimamo uliooneshwa na Rais Magufuli kwa Mwenyekiti wa Simiyu, uwe ndiyo huo huo kwenye suala zima la uhifadhi nchini kote. Tusikubali rasilimali wanyamapori itoweke kwa tamaa za watu wachache waliokosa uzalendo kwa nchi na hata huruma kwa viumbe hawa tuliopewa na Mwenyezi Mungu.
Rais Magufuli anaweza kuwa na nia nzuri ya kukuza utalii kwa kuagiza ndege na kuweka mazingira mazuri kwa watalii. Pamoja na ukweli huo, anaweza asifanikiwe kama yeye binafsi au Serikali yake watafumbia macho uharibifu mkubwa wa mazingira unaofanywa na wachungaji (wanaoitwa wafugaji), majangili, wachoma mkaa na wakata misitu.
Elimu ya uhifadhi itolewe kuanzia ngazi ya chini kabisa ili vijana wa Tanzania wakuzwe katika misingi ya kutambua, kuheshimu na kulinda mazingira na viumbe waliomo. Kuwafunza uhifadhi watu wazima wenye sharubu ni kazi ngumu kweli kweli.
Sambamba na elimu, mamlaka zinazohusika zipitie sheria zilizopo kwa lengo la kuzifanyia mabadiliko ili kuongeza adhabu kwa watu wanaojihusisha na masuala mbalimbali ya kuharibu uhifadhi, ujangili na kadhalika.
Wanasiasa wanashiriki sana kuua uhifadhi. Kwao, ubinafsi na tamaa za kupata mali vimekuwa chanzo kikuu cha wao kushiriki hujuma mbalimbali kwenye hifadhi na mapori mbalimbali nchini mwetu.
Hatuna budi kuyalinda mazingira ili wanyamapori ambao ndiyo kivutio kikuu waendelee kuwapo. Watalii wanazuru na wataendelea kuzuru nchi yetu kwa kiu ya kuja kuwaona wanyamapori, ndege na mazingira mazuri ya asili. Hakuna mtalii anayekuja nchini kuangalia ng’ombe, mbuzi, kondoo au punda vihongwe katika hifadhi na mapori yetu. Mtalii anakuja kumwona tembo, simba, nyumbu, duma, kiboko na wanyama wengine wakiwa katika mazingira yao ya asili.
Leo Ngorongoro imebaki kuwa makazi ya ng’ombe, mbuzi na kondoo. Kuna hatari kubwa ya watalii kupungua kwa sababu hakuna wanyamapori! Hakuna mtalii mwendawazimu anayeweza kulipa maelfu ya dola kuja kushuhudia mifugo!
Ndiyo maana wanaoitakia mema nchi yetu wanamwomba Rais Magufuli awe mkali katika kusimamia sheria za mazingira. Kasi hii ya uharibifu wa mazingira ikiachwa iendelee kwa miaka mitano, utalii utakuwa kwenye somo la historia! Kasi hii ya mifugo kwenye mapori na hifadhi vikiachwa hivi hivi, tutakuwa tumetenda dhambi kubwa kwa kuipuuza Ilani ya Arusha iliyotolewa na Mwalimu Nyerere mwaka 1961 jijini Arusha.
Hakuna mtalii atakayepanda ndege kuja kushangaa ng’ombe au mbuzi! Hakuna.