Baada ya kusoma mengi katika magazeti na kuona kwenye runinga namna lile jengo la ghorofa 16 lilivyoporomoka, mimi, huenda na wengine wengi. tumeingiwa na wasiwasi.
Kwanza ni ile hali ya majonzi ya kufiwa na wananchi 36 baada ya jengo lile kuporomoka. Pili, namna shutuma zilivyokuwa zinatolewa kuelekeza kwa makundi mbalimbali ya watu.
Halafu kukatolewa hali nisiyoielewa pale mamlaka kadhaa zenye dhamana za kuwajibika nazo eti zikawa zinalalamika. Nani basi wa kulaumiwa katika hali ya mkanganyiko namna hiyo?
Katika nchi yetu zipo sheria na kanuni zinazotawala ujenzi katika miji. Zipo mamlaka zinazosimamia sheria na kanuni hizo. Vipo vyombo vinavyodhibiti mienendo yote ya ujenzi. Katika hali kama hiyo, penye utaratibu mzuri wa utendaji kisheria, majanga au matukio ya kuporomoka majengo bila kuwapo matetemeko ya ardhi, kamwe hayatokei.
Hapa Tanzania siku hizi imekuwa kawaida kusikia jengo fulani limeporomoka hata bila kuwapo kwa nguvu za asili kama tetemeko la ardhi. Swali hapa ni kwamba hali ya namna hii inatokea vipi, au inasababishwa na nini?
Labda tujikumbushe baadhi ya matukio ya kukumbukwa jijini Dar es Salaam. Mwaka 2006, maeneo ya Keko, Manispaa ya Temeke, kuna jengo la ghorofa moja liliporomoka na kuua mtu. Jengo lile liliitwa Chang’ombe Village Inn. Mwaka 2008, jengo la ghorofa 10 katika Mtaa wa Mtendeni, Kisutu liliporomoka na kuua mtu. Hili janga limetokea katika Manispaa ya Ilala.
Februari, mwaka huu jengo la ghorofa nne maeneo ya Kijitonyama Mpakani, Manispaa ya Kinondoni, liliporomoka na kuua mtoto mwenye umri wa miaka 10. Jengo lile linasemekana lilisitishwa kuendelezwa ujenzi wake, lakini wanafamilia waliamua kuishi humo.
Sasa Machi 29, mwaka huu, majira ya asubuhi tunaelezwa kuporomoka ghafla kwa hilo jengo la ghorofa 16 katikati ya Jiji la Dar es Salaam, Mtaa wa Indira Gandhi, Manispaa ya Ilala. Hili sasa lilisikika nchi nzima. Limesababisha maafa makubwa. Imedhihirika wananchi 36 walifariki. Mungu awarehemu wote waliofikwa na mauti hayo ya ghafla.
Nimekumbusha matukio hayo yote ili tuone uzito wa tatizo hili Dar es Salaam na nchini kwa jumla. Haya ni matokeo ya kile ninachofikiria kuwa ni KUTOKUWAJIBIKA kwa mamlaka husika katika nchi. Mara baada ya lile ghorofa la Chang’ombe Village Inn kuporomoka, Serikali iliunda Tume kuchunguza na kukagua ujenzi wa maghorofa yote jijini Dar es Salaam.
Namsifu Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa, kwa kuunda tume mara moja kuchunguza kilichotokea na kifanyike nini. Tume hiyo ilikagua majengo 505 jijini Dar es Salaam.
Tumeambiwa matokeo ya uchunguzi ule ni kwamba maghorofa zaidi ya 100 yalibainika kujengwa kinyume cha taratibu za ujenzi! Maghorofa 147 yalikutwa HAYANA NYARAKA ZA UJENZI na maghorofa 22 eti inasemekana WENYEWE HAWAKUPATIKANA na yalikuwa yamejengwa BILA KUZINGATIA SHERIA ZA UJENZI! Hii ni ripoti ya mwaka 2006.
Jamani, hatua gani zilichukuliwa na mamlaka husika kurekebisha uzembe mkubwa namna ile katika Manispaa zote tatu? Hatuambiwi. Huo uzembe katika usimamizi wa sheria na kanuni za ujenzi (great laxity in law enforcement) ndiyo ulioleta maafa mengine yote yaliyofuata jijini Dar es Salaam na maghorofa yakaendelea kuporomoka na kuua watu! Tumefuga uzembe katika usimamizi wa sheria sasa majuto ndiyo mjukuu.
Kwa kadiri ya uelewa wangu, hakuna jengo linaloruhusiwa kusimama bila kibali cha Manispaa. Kamati husika inapitisha michoro, inasimamia na ujenzi wenyewe. Bango kubwa lenye kuonesha mwenye jengo (Proposed Building for ……….) nambari (Plot No.) ya kiwanja kibali cha ujenzi (Building Permit), mkandarasi na kadhalika.
Sasa Tume ya Lowassa inaposema maghorofa 22 hayakuwa na “wenyewe”, inaingia akilini ripoti ya aina hiyo? Kwanini Serikali (Mamlaka husika za Manispaa) WASITAIFISHE MARA MOJA MAGHOROFA hayo na kuwa MALI YA UMMA – nyumba za Serikali? Tuelezwe maghorofa hayo 22 sasa yanafanywaje, au anamiliki nani?
Kule kukaa kimya kwa mamlaka husika kunamaanisha iko namna hapo! Wapo watu wamenufaika hapo. Kwa hali ya namna hiyo, dhana ya rushwa katika mamlaka husika haiepukiki. Kama ile ripoti ya Lowassa ingefanyiwa kazi nadhani hata ghorofa la Kijitonyama, lile la Mtendeni na la Mtaa wa Indira Gandhi yasingejengwa; na kwa hiyo yasingeporomoka; na ndiyo kusema yasingeua watu.
Katika kila Manispaa kuna Mipango Miji, kuna wahandisi na kuna kamati maalumu za ujenzi. Wote hao hakuna angalau aliyekuwa na ule msukumo wa uwajibikaji akaonesha kwamba ukaguzi wa majengo ni moja ya wajibu wao? Sipendi kuamini kuwa mamlaka zote hizo zimewekwa mifukoni mwa wenye fedha ili wafumbie macho ukiukwaji huo wa sheria za ujenzi.
Siku moja nilitembelea ofisi ya chama tawala kumsalimia rafiki yangu. Mezani nilikuta kijitabu kidogo cha vikaragosi. Mimi nilivutiwa na kichwa cha kile kitabu, kiliandikwa “KIONGOZI ASIYEWAJIBIKA, TUFANYEJE”? Baada ya kusalimiana naye, na baada ya kusoma kidogo yaliyomo nilimtania namna hii, “My learned brother, who is such a leader?” Huyu bwana kitaalamu ni mwanasheria, na hawa wenzetu wanasheria wanapenda kutambulika kama wasomi ndiyo maana huitana ‘learned brother’.
Lakini nilichukua kijitabu kile na nikawa najiuliza swali hili la msingi: “Kiongozi asiyewajibika tufanyeje?” Mbona hapa Dar es Salaam maghorofa yanaporomoka na kuua watu, sisi wananchi tufanyaje? Ningali natafakari juu ya uwajibikaji.
Kwa mtazamo wangu, uwajibikaji ni moja ya sifa za maadili mema katika nchi.
Mwanadamu ukiwa mwajibikaji utafanya kila kitu kadiri ya sheria na kanuni zinavyoelekeza. Kule Ulaya, Marekani hata Japan, uwajibikaji unathaminiwa sana.
Wazungu wanasema “integrity of a nation”, yaani kama kusema “kioo cha utaifa”. Wengi tumechanganya “integrity” na neno “responsibility” mimi natafsiri “responsibility” kwa maana zaidi ya wadhifa na madaraka aliyonayo mtu lakini “integrity” natafsiri kama ni tabia za uaminifu, upole, uadilifu na kujali wengine anazokuwa nazo mtu. Ni zaidi ya heshima yako mtu.
Watu wenye maadili mema wenye integrity huwa na haiba ya utu. Taifa lenye watu wenye uadilifu wa hali ya juu huwa kwa kawaida linaheshimika sana. Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, alikuwa mtu wa integrity ya hali ya juu sana.
itaendelea