Kwa mara nyingine baadhi ya wanahabari wenzetu wamejikuta wakipigwa. Kama ilivyo ada, walioshiriki kufanya hivyo ni polisi.

Pengine wanahabari kadhaa hawatapenda hiki nitakachokisema hapa. Naomba wanisamehe. Wanisamehe kwa sababu mimi mwenyewe sifurahii kupigwa au kudhalilishwa; hasa ninapokuwa nikitekeleza dhima zangu halali.

Naomba wanisamehe kwa sababu hata mimi nimeshaonja adha ya nguvu na mabavu ya polisi wasiokuwa na maadili. Kwa hiyo, sishangilii kipigo. Wakati wenzangu wakipigwa, mimi nilishahukumiwa kwenda jela miezi mitatu kwa sababu niliandika habari za dhuluma za polisi zilizofanikisha askari zaidi ya 10 kuhamishwa katika moja ya vituo vyao mkoani Mara. Baada ya hapo, waliniwinda, wakanikamata na kunifungulia kesi ya kutungwa. Mfumo wa wakati huo ulikuwa mbaya. Hatukuwa na watetezi.

Tukio la pili ninalokumbuka ni la polisi kushambulia, mwanzoni mwa miaka ya 2000 wakati nikiripoti habari za Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Dunia, katika Hoteli ya Sheraton (sasa Hoteli ya Serena). ‘Kosa’ langu lilikuwa kuokota mabango kwa lengo la kusoma ujumbe uliokuwamo. Mabango hayo yaliandaliwa na wanaharakati kina Zitto Kabwe. Polisi walinijeruhi. Ulikuwa uonevu wa hali ya juu mno. Vyombo vya habari vya kitaifa na kimataifa pamoja na asasi mbalimbali viliripoti kwa nguvu kubwa na kulaani tukio hilo la uonevu.

Matukio yaliyonisibu nikiwa kwenye kazi hii ni mengi mno. Lakini jingine ambalo siwezi kulisahau ni lile la kung’atwa na mbwa nyumbani kwa Paul Bomani, kule Msasani jijini Dar es Salaam. Niling’atwa wakati nikienda nyumbani kwa aliyekuwa Waziri wa Fedha, Kilontsi Mporogomyi. Nilikuwa nasaka habari ya minofu ya samaki. Namshukuru Waziri wa Afya wa wakati huo, Mama Zakia Meghji, kwani baada ya kukosa sindano sehemu zote, alinipeleka Muhimbili ambako nilidungwa chanjo ya anti-rabies. Hii inazuia kichaa cha mbwa.

Lakini ni wakati huo huo ambao rafiki na dadangu, Rose, ambaye alikuwa Meneja wa Shirika la Bima la Taifa, Tawi la Kisutu, aliyeweza kunikatia bima ya maisha.

Nimeyasema haya kuonesha kwa ufupi kabisa kuwa wanahabari wanakabiliwa na mazingira magumu na ya hatari. Hapa sijagusa vitisho wanavyopata kutoka kwa watu wanaowaharibia mipango yao miovu. Wanawekewa mitego ya kila aina. Kama nilivyosema hapo awali, naomba wanahabari wanisamehe kwa hili tukio la juzi.

Kwanza, wanahabari si wamoja. Kwa kukosa umoja, ndiyo maana hawako pamoja yanapokuja masuala haya ya wao kupigwa au masuala ya kitaifa. Kwa wanahabari wa mataifa mengine, linapokuja suala lenye maslahi kwa jamii au taifa lao huungana na kuwa na msimamo mmoja. Tanzania mambo ni tofauti. Alipouawa Daudi Mwangosi, mwanahabari wa kituo cha Televisheni ya Channel Ten, Iringa, wanahabari hawakuonesha mshikamano wa dhati wa pamoja. Waliishia kuandamana na kumzomea Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi. Hata waliposema wanasusa kuandika habari za Polisi Iringa, baadhi ya vyombo vya habari vikawa mbele kupuuza msimamo huo.

Wanahabari walipopigwa hivi majuzi, sikushangaa. Sikushangaa kwa sababu hata polisi wenyewe wanajua baada ya hapo ungetolewa ‘mkwara mbuzi’ wa kususwa kwa habari zao, lakini baada ya muda watasoma na kusikiliza habari za Wiki ya Nenda kwa Usalama huku kina Kamanda Kova wakipamba televisheni na kwenye magazeti. Kweli, imekuwa hivyo.

Lakini nirejee kidogo kwenye sakata la kupigwa wanahabari wale. Wakati umefika kwa wanahabari kutojiaminisha kuwa wanajulikana kwa kila polisi. Nashukuru kuwa nimepata mafunzo ya kiasi chake ya kuripoti habari za vita na migogoro.

Jambo kubwa ambalo tunafunzwa kwenye eneo hilo ni la usalama wa mwanahabari kwanza. Mwandishi wa habari anatakiwa aende kuripoti habari za vurugu, vita au maandamano. Kitu cha kwanza anachopaswa kujiridhisha ni je, usalama wake utakuwa katika hali gani? Akishajua kwenda kufanya kazi hiyo katika mazingira hayo ni hatari kwa uhai wake, mara moja anapaswa aachane na mpango wa kwenda huko.

Pili, akishajua anakwenda kuripoti maandamano ambayo yana dalili za mvutano kati ya pande mbili, na kama kweli ana dhamira ya kuona kitakachotokea, ni wajibu wa mwanahabari kujiandalia mazingira ya kujilinda.

Silaha kubwa ya mwandishi wa habari katika mazingira kama hayo ni mavazi yake. Kwa mfano, anapaswa akumbuke kuvaa koti lisilopenya risasi na kofia ngumu vyenye maandishi yanayomtambulisha kuwa ni mwandishi wa habari. Mara kadhaa tumeona wanahabari wakiwa na mavazi hayo yenye maandishi ‘PRESS’.

Mavazi hayo yana faida nyingi, lakini kubwa ni ya kumfanya asiguswe, ama na polisi, au waandamanaji wakati pande hizo zikipambana. Hatua hiyo inampa fursa ya kwenda huku na kule akitekeleza wajibu wake bila kujikuta akishambuliwa, ama na polisi, au na waandamanaji. Ikitokea polisi au waandamanaji wamempiga mwanahabari aliyejitanabaisha kwa mavazi na vitendea kazi, basi hao watakuwa wakitenda kosa la jinai, na kwa kweli ni halali kuwashtaki.

Sasa tujiulize katika matukio mengi, likiwamo ya hivi karibuni, polisi wanawezaje kumtambua mwandishi wa habari kwa kumtazama usoni, au kwa kumuona akiwa na kalamu na kijitabu (notebook)?

Polisi gani aliyepewa amri (halali au haramu) ya kuwatawanya watu, ambaye anaweza kukagua vitambulisho ili kujua nani ni mwandishi na nani si mwandishi? Hapa ikumbukwe kuwa polisi anapoamriwa kushambulia, anachofanya ni kutekeleza amri, vinginevyo akianza kukagua vitambulisho, anaweza kuwajibishwa.

Rai yangu kwa viongozi wa vyumba vya habari na wamiliki wa vyombo vya habari nchini ni kuhakikisha wanabadilika na kujiandalia mazingira mazuri ya kuwawezesha wanahabari wanaotumwa kwenda sehemu za hatari, kufanya kazi zao vizuri.

Hapa namaanisha lazima mavazi maalum yawepo kwa wanahabari. Pili, ni lazima sasa kila mmiliki wa chombo cha habari akahakikisha wanahabari wake wanakuwa na bima za maisha. Kuendelea na mazoea ya kuwaona wanahabari wakiripoti habari kwenye vurugu na maandamano wakiwa hawatofautiani kwa kila hali na waandamanaji, maana yake ni kutaka waendelee kukumbana na virungu na mateke ya polisi.

Hata hivyo, ushauri huu hauna maana kwamba sasa polisi wajione wana haki ya kuwapiga raia, hasa waandamanaji ambao hufanya hivyo kwa amani. Kwa bahati mbaya katika nchi yetu wanachofunzwa polisi ni ukatili, amri za ajabu ajabu, kufokea raia na kuwapiga. Imekuwa ada sasa kuona polisi wakitumia nguvu hata mahali ambako hakustahili kabisa.

Hakuna mahali ambako polisi wanatakiwa wapige wananchi, hasa wananchi ambao madai na hoja zao vinaweza kumalizwa kwa njia ya majadiliano. Wananchi wengi wameshurutishwa kwa vipigo wakubali makosa, jambo ambalo ni kinyume kabisa na sheria za haki za binadamu. Wananchi wengi wamepata vilema kwa kupigwa wakiwa mikononi mwa polisi. Hilo haliwezi kukubalika.

Muhimu hapa ni kwa wanahabari kujua kuwa wana wajibu mkubwa mno wa kuwatetea na kuwasemea wananchi. Kama wao wanapigwa ilhali polisi wakitambua kuwa unyama wao unaweza kuanikwa kwa kalamu na picha, hali itakuwaje kwa wananchi wasiokuwa na uwezo huo?

Wananchi wanaonewa sana. Hapa nakumbuka tukio la mwaka 2000 wilayani Meatu ambako tukiwa kwenye mkutano wa kempeni na mgombea urais kupitia United Democratic Party (UDP), tukapata taarifa za viongozi na makada kadhaa wa chama hicho kuwekwa katika rumande ambayo ni ghala la kuhifadhia pamba.

Wale watu waliwekwa humo na uongozi wa kijiji na polisi kadhaa. Bahati nzuri kwenye mkutano huo tukawa na OCD wa Meatu wa wakati huo (simkumbuki jina, lakini alikuwa kijana msomi). Akaamuru wale watu wafunguliwe. Walipotoka, yule OCD nusura amwage chozi. Akawaona wale watu waliovyodhoofu, macho yakiwa yamepoteza nuru, lakini kibaya zaidi wakiwa wamebadilika hata rangi za ngozi zao na wakihema kwa shida kutokana na kuvuta hewa yenye vumbi la pamba. Akawauliza; nao wakasema walikuwamo mle ndani kwa siku nane hivi!

Yule OCD kwa masikitiko, akaamuru wale watendaji na polisi walioshiriki unyama huo, nao wafungiwe humo japo kwa saa 24 ili waonje adha za uonevu wanaowafanyia raia. Wananchi wakashangilia kwa kuona wamempata mkombozi.

Ninachojaribu kukisema hapa ni kwamba katika mazingira kama hayo, wanahabari lazima waandike matukio ya aina hiyo. Kuyaandika hakuwezi kuwafurahisha polisi na watendaji hao, na kwa sababu hiyo wanaweza kujikuta wakipigwa.

Vyovyote iwavyo, wajibu wa kuwasemea wananchi wasio na sauti unabaki kuwa wajibu mkuu wa wanahabari walioingia kwenye taaluma hiyo kwa wito.