Nianze kwa kumshukuru Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Abdalom Kibanda, Katibu wa TEF, Neville Meena, Mwanachama wa TEF, Jane Mihanji na wanachama wa Jukwaa la Wahariri Tanzania ambao kwa mshikamano mkuu mwezi Agosti tumefanya uamuzi utakaokuwa nguzo ya ustawi wa tasnia ya uandishi wa habari nchini.

Sitanii, naamini Watanzania mtakuwa mnaufahamu mchakato wa kutungwa kwa sheria ya uhuru wa vyombo vya habari nchini. Mchakato huu umekuwa wa muda mrefu sasa. Ni mchakato huu uliozaa Baraza la Habari Tanzania (MCT) mwaka 1995. Itakumbukwa kuwa harakati za kudai uhuru wa vyombo vya habari zilianza sawia na vuguvugu la mageuzi mwaka 1992.

Wadau waliwasilisha mawazo yao bila unafiki kwa Serikali na wananchi kwa ujumla, wananchi wakaelewa wadau wanataka nini. Wadau wamefanikiwa kuiondoa hofu jamii kuwa uhuru wa vyombo vya habari si kwa manufaa ya vyombo vya habari pekee, bali wananchi kwa ujumla wake.

Uhuru wa vyombo vya habari ni haki ya msingi inayowezesha haki nyingine kupatikana. Mfano huu nimeutoa mara kadhaa na ni vyema nikaurudia kuwa ikitokea mwananchi akaenda katika hospitali ya mkoa fulani au Muhimbili akadaiwa rushwa, mwananchi huyo akishindwa kupata huduma akaenda kueleza malalamiko yake kupitia vyombo vya habari, mara moja atarejeshewa haki hii kwa watendaji wa hospitali husika kutaka kuthibitisha kuwa hawaendeshi hospitali husika kwa njia ya rushwa.

Duniani kote, nchi zimeendelea kwa vyombo vya habari kuandika ukweli wa kila kinachotendwa ndani ya Serikali, watu binafsi au mashirika. Hii imepunguza uhalifu, imeongeza makusanyo ya kodi na imeboresha huduma za jamii. Kwa mfano zikitolewa ruzuku (fedha) za madawati, watendaji wakazitafuna ikitangazwa habari hii, polisi na mahakama wanapata pa kuanzia kuwawajibisha wahusika na mara nyingi fedha hizo hurejeshwa.

Kutokana na umuhimu huu, wadau wa vyombo vya habari waliamua kuunda umoja wa kudai haki ya msingi ya kupata habari unaohusisha mashirika 11. Umoja huu unafahamika kama Muungano wa Wadau wa Haki ya Kupata Habari (Coalition of the Right to Information – CORI). CORI inajumuisha taasisi 11, ila kwa bahati mbaya MCT wametaka kuuteka umoja huu.

CORI inajumuisha Tanzania Citizen Information Bureau (TCIB), the Media Institute of Southern Africa Tanzania Chapter (MISA-Tan), the Media Owners Association of Tanzania (MOAT), Sikika, the National Organization for Legal Assistance (NOLA), The Legal and Human Rights Centre (LHRC), Tanganyika Law Society (TLS), Tanzania Editors’ Forum (TEF), Tanzania Media Women Association (TAMWA) and MCT. Kwa bahati mbaya, MCT mara zote wamekuwa wakisema MCT na wadau, bila kutaja wadau wengine katika mchakato huu.

Ni wadau hawa walioisukuma Serikali kuandika Sera ya Habari ya mwaka 2003. Ni wadau hawa na wala si MCT peke yao kama wanavyotaka kuuaminisha umma walioishinikiza Serikali kuchapisha muswada iliouita Freedom of Information (FOI) mwaka 2006, kisha ikauondoa.

Ni wadau hawa mwaka 2007 walikusanya maoni ya wadau nchi nzima na kupendekeza miswada miwili wa kwanza ukiwa wa Haki ya Kupata Habari (RTI) na wa pili ukiwa wa Huduma kwa Vyombo vya Habari (MSB). Kwa muda wote huo wadau wamekuwa wakipambana kipatikane chombo huru kitakachoweza kuongoza vyombo vya habari.

Ukisoma kumbukumbu za kuanzishwa kwa MCT unaona nia ya wadau ilikuwa ni kuanzisha chombo chenye kusimamia vyombo  vya habari, ikiwamo kuanzishwa kwa Tume Huru ya Habari. Kadri mchakato ulivyoendelea MCT bila kushirikisha wadau, wakabadili mtazamo huu na kuanzisha mchakato mpya wa kujisimamia bila meno (self regulation).

Sitanii, mimi na wahariri wengi tumekuwa tukipigania mfumo huu wa kujisimamia wa kisheria (wenye meno) badala ya mfumo wa maadili ulioshindwa sehemu nyingi duniani. MCT wanasema mwandishi au gazeti likimkosea mtu, basi wakutanishwe wahusika na hata kama kuna aliyemkosea mwenzake wapeane mikono na kusameheana.

Jamii na vyombo vya dola vimekuwa haviamini katika mfumo huu. Vinaamini, sawa na mimi ninavyoamini kuwa mtu anayetenda kosa lazima awajibishwe kisheria. Anapaswa kulipa gharama ya uovu wake yeye binafsi, bila kuumiza wasiohusika. MCT wamekuwa wakijitambulisha kama taasisi kiongozi wa vyombo vya habari hapa nchini. Kwa muda wote Serikali imekuwa ikiamini kuwa msimamo wa MCT ndio msimamo wa vyombo vya habari, kumbe sivyo.

Sitanii, msimamo huu wa kuwa na chombo cha kusimamia vyombo vya habari kisicho na meno, umeifanya jamii kwa muda mrefu kuona kama waandishi wa habari wanataka kuwa juu ya sheria. Mimi nasema waandishi wasionewe, ila wasitengenezewe mazingira ya kuwa raia daraja la kwanza. Kwa kujenga mazingira kuwa tusiguswe, tunajengewa misingi ya kuvunja sheria bila wasiwasi, hata kama haukuwapo ulazima wa kufanya hivyo.

Matokeo yake, msingi huu umetujengea usugu na kudhani kuwa sisi waandishi ni polisi, ni askari magereza na wakati huo huo ni watendaji wenye kuweza kutoa matamko na yakatekelezeka bila kuhojiwa. Matokeo ya kuendelea kushikilia msimamo huu, tumejikuta Serikali ikigoma kutunga sheria ya kuongoza vyombo vya habari na kubakiza madaraka mikononi mwa waziri mwenye dhamana.

Kwa madaraka kubaki mikononi mwa Waziri Mwenye dhamana, tumejikuta magazeti yakifungiwa, redio na televisheni ama zimefungiwa kabisa au baadhi ya vipindi vyake vimefungiwa na hii yote inatokana na kutokuwapo chombo chenye nguvu za kisheria kinachoweza kuisimamia taaluma ya habari.

Hii imeifanya taaluma ya habari isiheshimike katika jamii yetu. Nchi hii inavyo vyama vya kitaaluma kama Chama cha Madaktari Tanzania, Chama cha Wahasibu, wagavi, wanasheria, wakadiriaji majenzi, makandarasi na wengine wengi vilivyoanzishwa kwa Sheria ya Bunge. Maana yake ni kwamba ikitokea mwanataaluma mwenzao ametenda kosa, vyombo hivi vinamwita, vinamuonya na ikibidi kama hajajirekebisha vinamfungia kwa muda kumtumikia taaluma husika kwa maelezo kuwa hawezi kuumiza jamii wakabaki bila kumchukulia hatua.

Vyama vya kitaaluma vilivyoanzishwa kwa mujibu wa sheria vinayo faida ya msingi. Moja na ya msingi, mkosaji hajawajibika yeye binafsi na kuiacha jamii ikiendelea kupata huduma inayotolewa chombo chake, huku watumishi katika taasisi aliyoitumia mtu kama kichaka kutenda makosa ikiendelea kufanya kazi na watumishi wasiohusika na makosa hayo wakiendelea kupata mishahara na kuitumikia jamii.

Sitanii, naomba kutoa mfano linganishi hapa nchini niweze kueleweka vyema. Daktari aliyepasua mgonjwa wa kichwa goti na wa goti akampasua kichwa, alipewa adhabu na Chama cha Madaktari Tanzania. Lakini kutokana na kosa hilo, hatukuiona Hospitali ya Taifa Muhimbili inafungiwa.

Hii ina maana kuwa wananchi waliendelea kupata tiba pale Muhimbili, madaktari na manesi walioajiriwa pale Muhimbili waliendelea kufanya kazi na kulipwa mishahara. Utaratibu kama huu ndio tunaoutaka kwa waandishi wa habari. Kwa mfano ikiwa kweli mtu aliyechapisha habari ya gazeti la Mwanahalisi alikosea, gazeti halikupaswa kufungiwa kama ambavyo Muhimbili haikufungiwa.

Chama cha Kitaaluma au Tume ya Habari yenye nguvu ya kisheria, ilipaswa kumwita Mhariri wa Gazeti la Mwanahalisi, ikaichunguza habari hiyo iwapo ilikuwa na upungufu wa kitaaluma  au la na baada ya kujiridhisha ama ingemuonya au ingemchukulia hatua za kitaaluma aliyeandika habari hiyo, ikiwamo kusitisha leseni yake ya kazi kama alikiuka maadili, lakini gazeti la Mwanahalisi lingeendelea kuwa sokoni, wananchi wangeendelea kupata huduma ya habari kutoka Mwanahalisi na waandishi walioajiriwa wangeendelea kupata mishahara kama ilivyotokea kwa Muhimbili.

Baada ya wahariri nchini kuyabaina haya, wakaona MCT inawapeleka chaka. Januari 10, 2013 wakawasilisha maoni yao kwa Tume ya Jaji Joseph Warioba wakiomba mambo manne. Haki ya Kupata Habari, Uhuru wa Vyombo vya Habari, Uhuru wa Kutoa Mawazo na kuanzishwa kwa Baraza Huru au Tume Huru ya Habari.

Hapa ndipo msigishano ulipoanza rasmi na MCT. MCT imepigania mfumo wa vyombo vya habari kutoongozwa na sheria kwa miaka 20 sasa bila mafanikio. Vyombo vya habari vimeendelea kufungiwa kama Mwanahalisi, waandishi wa habari wameendelea kupigwa na hakuna maendeleo yoyote tunayopata kitaaluma zaidi ya kuendelea kutujengea usugu.

Katika kikao cha Agosti, 2014 wahariri waliamua kuchukua mkondo tofauti. Katika kikao cha TEF tuliunda timu ya watu wanne, iliyoongozwa na mimi Deodatus Balile, na wajumbe Absalom Kibanda, Jane Mihanji na Neville Meena kwenda Dodoma kuangalia uwezekano wa Katiba inayopendelezwa kuwa na Ibara inayoruhusu kuanzishwa kwa Tume au Baraza Huru la Vyombo vya Habari Tanzania.

Tulikwenda Dodoma tukazungumza na Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba, Samuel Sitta tukazungumza na wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba wasiopungua 150, ambalo waliona mantiki ya kuanzishwa kwa Baraza au Tume Huru ya Habari kwa nia ya kuondoa misuguano na Serikali, kuipa jamii fursa ya kupata habari bila mizengwe na kurahisisha ushughulikiaji wa matatizo ya kiutendaji yanayojitokeza sasa ndani ya vyombo vya habari.

Baada ya hoja hii kukubalika, mtu mmoja akajipendekeza na kwenda kwenye Kamati ya Uandishi, akasema uongo kuwa ametumwa na vyombo vya habari nchini, kuondoa pendekezo la Baraza Huru la Habari, na kwamba tumekubaliana, wakati si kweli na hatujawahi kukubaliana jambo la aina hiyo.

Rasimu ya Kwanza ya Katiba inayopendekezwa iliposomwa, tukaduwaa pamoja na kwamba tulihakikishiwa kuwa chombo hiki kingekuwamo. Kwa ujinga, mtu huyu akapita mitaani anatamba kuwa ameliondoa pendekezo hili. Ni katika hatua hii, wahariri tulijisikia maumivu makubwa. Tukajiuliza mtu huyu anazungumza kwa mamlaka yapi?

Tukajiuliza, mbona tunapopelekwa mahakamani hatupati msaada kutoka kwake zaidi ya yeye kutoa matamko ya kulaani vipigo? Uvumilivu ulituishia, tukaamua kuzitumia vilivyo siku mbili na kwa ushawishi mkubwa wa wahariri tukafanikiwa kuingiza Ibara mpya ya 208A inahosema: “Kutakuwa na Tume mbalimbali za kisekta zitakazoanzishwa kwa mujibu wa sheria zitakazotungwa na Bunge kwa ajili ya usimamizi, uratibu na utoaji wa huduma za jamii.”

Sitanii, najua msomaji unaweza kujiuliza wahariri wamekuwaje kwenda kuomba Tume hii kwa rasimu ambayo UKAWA wameikataa inayoonekana ni ya CCM? Tulilijadili sana hili, na ukiacha faida tulizozitaja hapo juu, busara ilituonyesha kuwa CCM ndio chama tawala. Rasimu inayopendekezwa tukiipuuza inaweza kupita miaka mingine 50 bila kuuona uhuru wa vyombo vya habari hapa nchini.

Hapa tulichagua msemo wa wahenga kuwa heri nusu shari kuliko shari kamili. Tuliona dirisha hili lililojitokeza, tulitumie kuingiza uhuru wa vyombo vya habari, uhuru wa kutoa mawazo, haki ya kupata habari na Tume Huru ya Vyombo vya Habari, itakayosimia, kuratibu na kuweka viwago vya huduma ya vyombo nchini kwa ustawi wa taifa letu.

Hii itakuwa ni kwa manufaa ya taifa zima, wakiwamo UKAWA, CCM na hata wasioshiriki siasa zinazoendelea Dodoma. Wiki ijayo, nitaeleza kwa ufasaha mvutano uliojitokeza baada ya pendekezo hili kukubaliwa, MCT ikionyesha kukejeli wahariri kupitia Katibu Mtendaji, Kajubi Mkajanga na matarajio na mwelekeo wetu kama waandishi wa habari.

Nahitimisha leo kwa kusema kuwa kwangu, ukweli ni zaidi ya maslahi ya tumbo langu. Tunapaswa kuijenga taaluma ya uandishi wa habari kwa faida ya wanahabari na taifa kwa ujumla, bila kuhofia kuwa pengine kwa kufanya hivyo tutawaudhi wafadhili. Tanzania ni nchi yenye mamlaka kamili, na kamwe tusikubali kuendeshwa na wafadhili. Tukutane wiki iiayo.