Wizara ya Ujenzi, kama zilivyo wizara nyingine, ni miongoni mwa wizara chache ambazo ni mihimili ya maendeleo ya taifa letu.
Tanzania, tofauti na makoloni mengine, iliachwa na watawala dhalimu ikiwa haina barabara, si za lami tu, bali hata za changarawe.
Tangu Uhuru wa Tanganyika na baadaye Muungano wa Tanganyika na Zanzibar uliozaa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Serikali zote za Awamu Nne zimejitahidi kuhakikisha kuwa barabara za lami na changarawe zinajengwa.
Kazi hiyo licha ya kufanywa kwa miaka mingi, bado inakabiliwa na changamoto. Eneo kubwa la Tanzania bado halifikiki kirahisi kutokana na ubovu au kutokuwapo barabara.
Pamoja na hali hiyo, ukweli ni kwamba Serikali zote zimeendelea kuhakikisha kuwa Tanzania inaunganishwa kwa barabara, tena za lami. Mpango huo umefanikiwa kwa kiwango cha kutia matumaini.
Mathalani, Mtanzania aliyefariki mwaka 1990, kama angeweza kufufuka leo na kushuhudia Watanzania wakisafiri kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza kwa saa kadhaa, asingeweza kuamini. Pale ambako Serikali inajitahidi kufanya mambo ya maana hatuna budi kuipongeza.
Pamoja na kasi kubwa ya ujenzi huu, bado kuna dosari ambayo tumeona hatuna budi kuungana na wengine kuisema. Tatizo kubwa tunaloliona hapa ni kwamba barabara hizi zinaweza zisiwe na tija kubwa na kwa muda mrefu kutokana na kulemewa na shehena nzito zinazosafirishwa kwa kutumia malori.
Kwa bahati mbaya hatukuona jambo hili likipewa mtazamo mpya katika hotuba ya Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli. Barabara zimelemewa na shehena baada ya kuwapo juhudi za makusudi za kuzorotesha usafirishaji wa njia ya reli.
Kuna maneno yanazungumzwa kwamba wamiliki wengi wa malori haya ni vigogo. Kuna madai kwamba wafanyabiashara wanajitahidi kuhakikisha kuwa reli hairejei katika utendaji kazi ili vigogo wanasiasa na wafanyabiashara waendelee kufaidika.
Ndiyo maana tunasema kwamba pamoja na nia nzuri na kasi ya Serikali ya kujenga barabara za lami, hakika kinachofanyika sasa ni kama kutwanga maji kwenye kinu. Barabara hazitadumu.
Kama kweli tunataka barabara hizi zidumu na ziwe na tija ni lazima tuhakikishe kuwa shehena nzito za nondo, saruji, shaba na mizigo mingine ya aina hiyo inasafirishwa kwa kutumia reli na maji.
Hakuna nchi kubwa kama Tanzania iliyoweza kuendelea kwa kusafirisha shehena nzito kwa kutumia barabara. Hakuna. Barabara zikibaki kuwa za kusafirisha mizigo ya kawaida na abiria, kwa hakika barabara zitadumu.
Mwisho, tunaupongeza uongozi wote wa Wizara ya Ujenzi kwa kuziba mwanya mkubwa wa wizi uliokuwa kwenye ujenzi wa barabara za lami. Kufanikisha kushusha bei ya ujenzi wa kilomita moja ya lami kutoka Sh bilioni 1.8 hadi wastani wa Sh milioni 700 ni jambo linalostahili pongezi. Tuwe na utaratibu wa kupongeza pale viongozi wetu wanapofanya mambo ya maana kama haya. Hongereni sana.