Nilipata kusoma makala ya kiongozi wangu wa kitaaluma, Jenerali Ulimwengu, akikosoa Watanzania wenye matamanio ya kumpata ‘Kagame’ wao.
Mwenyekiti Ulimwengu alisema mengi, akahitimisha kuwa tatizo letu kubwa ni la mfumo. Anaamini kuwa kwa kupata mfumo mzuri, hasa kupitia Katiba mpya, mambo tunayoyaona sasa yakiwa yamekwama, yatakwamka. Makala hayo yalikuwa ya kufikirisha.

Kwa bahati nzuri kila ninapokutana na maandishi yanayomhusu Paul Kagame (Rais wa Rwanda), sisiti kuyasoma. Nampenda Kagame. Ana sifa za kumwezesha kuwa na mashabiki wengi. Katika ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati, Kagame amejipambanua kama kiongozi aliyedhamiria kuiweka juu kabisa nchi yake kimaendeleo.

Nimepata kusema huko nyuma kwamba mimi nitakuwa wa mwisho kuishabikia Katiba mpya. Msimamo wangu unatokana na ukweli kwamba hii Katiba tuliyonayo sasa haina matatizo makubwa kama wengi wetu tunavyoaminishwa. 

Ukiwasikia Watanzania wengi, hasa vijana, kwao Katiba mpya wanaiona kuwa ujio pekee wa maisha bora. Wanaona kuwa itafungua pepo ya neema. Wanaitamani Katiba mpya kwa imani kwamba itafukuza umasikini, ujinga, maradhi na huu ufisadi wote!

Kwa wale wa rika langu, na niliowapita umri, kwao Katiba mpya ni mwarobaini wa matatizo yetu yote! Wanajidanganya.

Bado naamini na nitaendelea kuamini kuwa Katiba mpya si suluhisho la matatizo yetu.

Kama waumini fulani wanalalamika kukosa elimu, Katiba mpya haiwezi kuwapa elimu endapo wataendelea kuamini kuwa madarasa pekee ndipo mahali sahihi kwa watoto wao kujifunzia. Wala Katiba mpya haitawafanya wasiotaka shule waweze kuwa wakurugenzi katika mashirika na kampuni au marubani!

Nimejaribu kuipitia Katiba ya sasa ili nishawishike kuamini kuwa ni mbaya kiasi kwamba haifai hata kutazamwa, nimekosa ibara ya kuniaminisha hivyo. Dosari nilizoziona ni za kawaida, ikiwamo inayosema kuwa nchi hii ni ya “Ujamaa na Kujitegemea”.

Nimeviona vipengele vinavyomtaka kila mwananchi kulinda rasilimali za nchi, nimeziona ibara zinazoelezea haki ya kila mmoja wetu mbele ya vyombo vya sheria, na pia haki za binadamu. Yamo mengi kwenye Katiba hii. Bahati mbaya ni kwamba wengi wetu tumeingia mkumbo wa kuikosoa bila hata kujua kilichomo.

Ninachojaribu kukisema hapa ni kwamba tatizo kubwa la nchi yetu ni uongozi, basi. Hili linathibitishwa na matukio ya mawaziri watatu baada ya kuapishwa hivi karibuni.

Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Abdallah Kigoda, amemsimamisha kazi Mkurugenzi wa TBS, Charles Ekelege. Huyu ni mmoja wa watuhumiwa wakuu walioweka rehani afya za Watanzania kwa kuruhusu vyakula na vifaa visivyofaa. Wananchi wameshangilia uamuzi wa Dk. Kigoda. Wameshangilia, si kwa sababu wanamchukia Ekelege. Wameshangilia kwa kukunwa na ujasiri wa waziri huyo ambao mtangulizi wake aliukosa.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki, naye amepitisha fagio katika wizara yake. Wakurugenzi sita na askari wanyamapori 28 wamesimamishwa kutokana na tuhuma kadhaa zikiwamo za usafirishaji wa wanyamapori hai, uuaji faru na utoaji vibali mbalimbali. Wananchi wamekunwa sana kwa uamuzi huo.

Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, alikesha Tazara akihakikisha kuwa abiria wanasafiri. Ameingia ATCL na kukuta kuna mambo mengi, mazito na machafu. Sare za wafanyakazi pekee zimegharimu zaidi ya Sh milioni 60! Amewasimamisha kazi vigogo kadhaa. Ameahidi kuwa moto huo huo unaendelea Bandari na kwingineko ndani ya wizara yake.

Kitu gani kinachoonekana hapa? Je, hawa viongozi wametoa wapi ujasiri huu wa kuwashughulikia vigogo hao? Kinachobainika haraka haraka hapa ni kwamba hawa mawaziri hawakusubiri Katiba mpya ili waweze kuwashughulikia watuhumiwa ndani ya wizara zao. Kadhalika, mawaziri watangulizi wao si kwamba walishindwa kuwaadabisha hao vigogo kwa sababu ya Katiba ya sasa (isiyofaa?), bali ni kwa kuwa waliendelea kuongoza wizara hizo kwa mazoea.

Ndiyo maana nasema, ukubwa wa tatizo la rushwa katika taifa letu, wizi wa mali za umma, uzembe, ukorofi, kutowajibika na mengine machafu ya aina hiyo, hayasababishwi na Katiba hii “mbaya”. Haya machafu tunayoyaona sasa ni matokeo ya viongozi legelege, viongozi wanaowaonea aibu wenzao wasiofaa, na ni matokeo ya kutowajibika kwa kila mmoja wetu katika nafasi yake.

Udhaifu wa uongozi umeonekana si katika wizara na idara pekee, bali hadi katika ngazi za juu kabisa za uongozi wa taifa letu. Huwezi kuwa na uongozi wa mazoea katika ngazi za juu halafu ukatarajia kuona miujiza kwa kunyooka yenyewe.

Kwa hoja hii, naungana kabisa na Watanzania wanaoamini kuwa Tanzania ilipofika sasa inamhitaji Kagame wake. Tunaweza kupata Katiba mpya nzuri sana, lakini kama hatuna rais, makamu wa rais, waziri mkuu na mawaziri wanaowajibika kwa dhati ya mioyo yao, kamwe tusitarajie mabadiliko ya maana.

Nitatoa mfano. Kwa sasa kuna ujenzi mkubwa unaendelea katika Jiji la Dar es Salaam. Ujenzi huu unasimamiwa na Waziri mwenye dhamana hiyo, Dk. John Magufuli. Mara kadhaa nimepingana na Magufuli katika mambo kadhaa, lakini kuna mambo hata kama humpendi, utalazimika kumpenda!

Ujenzi wa barabara za Dar es Salaam hasa ile ya Kimara unafanywa na Magufuli kwa ubabe wake! Ikumbukwe kuwa kabla ya kurejeshwa wizarani hapo, mradi wa mabasi yaendayo kasi ulikuwa kama umeshakufa!

Wavamizi wa barabara waligoma kuondoka, lakini siku alipozindua Kituo cha Mabasi Mbezi aliwaagiza viongozi wa Serikali Mkoa wa Dar es Salaam wawaondoe wavamizi hao ili ujenzi uanze. Kweli, wale waliodhani kwamba kuwaondoa wavamizi hao ingekuwa kazi isiyowezekana, sasa wanakiri kuwa walikosea. Wameondolewa na kazi inaendelea. Hii inatoa matumaini kuwa siku si nyingi, wananchi katika jiji hilo wataondokana na adha ya foleni.

Lakini jiulize, Dk. Magufuli amechukua uamuzi huo kwa ridhaa ya nani? Kwa Katiba mpya? Hapana. Bila shaka ni kwa jeuri yake mwenyewe na kwa kufuata sheria. Wengi tunakumbuka namna alivyopigwa kufuli na Waziri Mkuu kule jimboni kwake Chato, alipozuiwa kuwaondoa waliovamia hifadhi ya barabara. Kana kwamba haitoshi, Rais naye akapigilia msumari. Wengi wakadhani angekoma, la hasha! Ameendelea kuwa kichwa ngumu kwa sababu anaamini nchi haiwezi kuendeshwa kwa lelemama na kwa kuchekeana.

Tunamhitaji Kagame wetu hapa ili pamoja na hiyo Katiba mpya, aweze kusimamia sheria na kanuni. Tunaweza kuwa na Katiba nzuri sana, lakini bila kuwa na wasimamizi imara, tutajuta kutumia muda na fedha nyingi kwa kitu kisichokuwa na tija kwetu.

Hapa tulipofika sasa tunahitaji msukumo mpya wa uongozi. Chama Cha Mapinduzi kinapoteza mvuto si kwa sababu kimechokwa kwa bahati mbaya, bali ni kwa kutokana na kupoteza maana halisi ya kuwapo kwake. Wananchi wamepoteza matumaini. Hawaamini tena wanachoambiwa na viongozi wa chama hicho.

Serikali inachukiwa si kwa sababu ni ya CCM, bali ni kutokana na kuonekana kushindwa kusimamia misingi ya uongozi wa nchi. Kwa mfano, kama tungekuwa na viongozi makini, mgogoro wa Muungano huu wa leo usingekuwapo. Viongozi wenye dhamana wanajua kuna kero, lakini wameshindwa kuzitatua, matokeo yake sasa nchi inaelekea kusambaratika.

Udini unazungumzwa kama sifa sasa. Unasikia watu wanataka Wakristo wawe nusu, na Waislamu nusu katika nafasi mbalimbali za uongozi. Tutafika mahali tuwe na mawaziri nusu kwa nusu, Bunge nusu kwa nusu, makarani nusu kwa nusu, marubani nusu kwa nusu, madaktari nusu kwa nusu, wauguzi vivyo hivyo. Hatutaangalia sifa tena. 

Sokoni Kariakoo tutaanza kuuliza Waislamu wamo wangapi, na meza ngapi ni za Wakristo! Barabarani tutahoji kwanini hawa wa imani fulani wana magari mengi, ilhali wa imani ile wana magari machache! Tunakaribia huko kwa sababu ya udhaifu wa viongozi wetu. Hakuna anayekemea kwa dhati. Mchana wanakemea, usiku wanachochea!

Tumefika mahali tunapohitaji kuwa na “Kagame wetu” ambaye akisema barabara ijengwe, kweli itajengwa. Tufike mahali tuwe na Kagame anayeweza kukataa kuwa yai moja haliwezi kuuzwa kwa Sh 900! Tuwe na Kagame anayeweza kuthubutu kupiga marufuku ununuzi wa mashangingi. Tuwe na Kagame ambaye hatasubiri shinikizo la wabunge na wananchi ndipo awang’oe mawaziri waliofeli.

Tuwe na Kagame atakayehoji kwanini halmashauri hii au ile haina madawati katika shule zake. Tuwe na Kagame ambaye hatakubali kuona dawa za Sh bilioni tano zikioza ilhali watu wakifa. Tuwe na Kagame ambaye atamfukuza waziri anayekaa akitazama Muhimbili (hospitali namba moja katika taifa) ikikosa mashine, ilhali zahanati binafsi ya Tandale ikiwa nazo!

Tuwe na Kagame ambaye msafirisha dawa za kulevya akiiona picha yake uwanja wa ndege, ataahirisha safari! Tuwe na Kagame wetu ambaye hatakubali kuona wakulima wakinyonywa kwa kizingizio cha soko huria. Tuwe na Kagame wetu ambaye hatakuwa mwepesi wa kuuza ardhi kwa wageni kwa kivuli cha uwekezaji! Tuwe na Kagame ambaye hatakubali kuiona nchi yenye tanzanite, almasi, dhahabu, wanyamapori, mapori, mito, maziwa, milima mirefu, bahari, mafuta, gesi, samaki, ulani na utajiri wa kila aina, ikiwa ndani ya “Kumi Bora Duniani” kwa kuhemea. Hakika tunamhitaji Kagame wetu ambaye hataunda wizara ya viwanda ilhali akiwa ameuza viwanda na mashirika zaidi ya 400! Na kama ikishindikana kuwa na Kagame wetu, bali tumpate japo wa kukodi! Kiu ya Watanzania ni kuona wanapata kiongozi/viongozi jasiri.