Bidhaa mbalimbali zenye thamani ya sh bilioni 3.8 zimeuzwa wakati wa Maonesho ya 47 ya Biashara ya Kimataifa ‘Sabasaba 2023’ ikilinganishwa na sh bilioni 3.6 zilizopatikana katika maonesho ya mwaka jana.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (Tantrade), Latifa Khamis akizungumza katika hafla ya kufunga maonyesho hayo amesema kupitia wafanyabaishara wa ndani na wafanyabiashara wa nje (B2B) waliweza kujadiliana na kusaini Mkataba wa Makubaliano ya awali (MOU) na kutoa oda ya bidhaa za zenye thamani ya sh bilioni 16.98 .
Amesema pia jumla ya mikataba tisa ya awali (MOU) imesainiwa katika sekta na maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na ununuzi wa pamba uliosainiwa kati ya Bodi ya Pamba ya Tanzania na Algeria kununua tani 30,000 kwa mwaka, na ununuzi wa Mkonge kati ya Bodi ya Mkonge Tanzania na kampuni kutoka India.
Pia, katika maonesho ya mwaka huu yamewezesha kusainiwa MOU katika sekta ya kilimo na elimu.
Aidha, amesema MOU nyingine ni kati ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) na Chuo Kikuu cha Kilimo cha Chaudhary Charan Singh Haryana, India kuhusu programu mbalimbali za biashara ya Kilimo, Bioteknolojia, Sayansi ya Chakula na kadhalika.
Latifa amesema, zaidi ya wageni milioni tatu wa ndani na nje ya nchi ni zaidi ya 267 na nchi 17 walitembelea maonesho hayo kupata mahitaji mbalimbali ikilinganishwa na miaka ya nyuma ambapo mwaka jana kulikuwa na wageni 265,957.
Pia amesema kupitia maonesho hayo waliweza kutoa ajira za muda zipatazo 11,687.