Na Daniel Limbe,Jamhuri Media,Biharamulo

IMEELEZWA kuwa serikali inakusudia kuongeza uzalishaji wa zao la kahawa kwenye wilaya ya Biharamulo mkoani Kagera ili kuinua uchumi wa jamii na kuchangia pato la taifa ukilinganisha na hali ilivyo sasa.

Wilaya hiyo ambayo ni miongoni mwa wilaya saba za mkoa wa Kagera imejiwekea mikakati madhubuti ya kuhakikisha uzalishaji wa kahawa unapanda kwa kasi ukilinganisha na mazao mengine ya biashara ambayo huzalishwa katika wilaya hiyo.

Kulia ni mkurugenzi wa Halamshauri ya Biharamulo, Innocent Mkandara,anayefuata ni Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya hiyo,Leo Rushahu,na wa tatu kutoka kulia ni Mwenyekiti wa kamati ya Uchumi, ujenzi na Mazingira, Philbert Rubula na wa kwanza kushoto, ni Ofisa kilimo wilaya hiyo, Dkt. Sospeter Mashamba.

Baadhi ya mazao hayo ni pamoja na Tumbaku,Pamba na Kahawa huku mazao ya chakula yakiwa ni maharage,mahindi,viazi vitamu na karanga.

Akitoa taarifa ya serikali kwenye uzinduzi wa hafra fupi ya ugawaji wa miche bora 800,000 ya kahawa kwa wakulima wa wilaya hiyo,Ofisa Kilimo wa wilaya hiyo,Dkt. Sospeter Mashamba,amesema mpango huo unakusudia kuinua pato la mwananchi mmoja mmoja,kaya na serikali kwa ujumla.

Kadhalika mpango huo umeanza kutekelezwa tangu mwaka 2020/21 ambapo miche ya kisasa 89,000 ilizalishwa na kusambazwa bure kwa wakulima,2021/22 jumla ya miche 670,000 iligawiwa kwa wananchi ambapo mwaka 2022/2023 miche 36,000 ilisambazwa.

Mwonekano wa kitalu cha miche bora ya kahawa

Pia mwaka 2023/24 takribani miche 593,912 ilizalishwa kupitia Bodi ya kahawa nchini (TCB) na kugawiwa wananchi bure ambapo zaidi ya miche 1,388,912 imepandwa kwenye mashamba mbalimbali ya wananchi wa wilaya hiyo.

Dkt. Mashamba amesema katika mpango mkakati wa mwaka 2024/25 halmashauri hiyo kwa kushirikiana na Bodi ya kahawa nchini, inakusudia kuzalisha jumla ya miche 1,150,000 kwenye vitalu vya Katoke,Rukaragata, Kalenge,na Nyakahura na kwamba ifikapo mwaka 2030 halmashauri hiyo itakuwa kinara wa uzalishaji wa kahawa nchini.

Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya hiyo, Innocent Mkandara,ametumia fursa hiyo kuwataka wananchi kutambua thamani ya miche hiyo kwa lengo la kuitunza ili baadaye iweze kuwatunza kwa kuinua vipato vyao na kuchochea uchumi wa taifa kutokana na tozo mbalimbali kupitia zao hilo.

Amesema upo uwezekano wa robo nzima ya bajeti ya halmashauri hiyo kubebwa na mapato ya kahawa iwapo wananchi wataitunza kwa kuzingatia ushauri wa wataalamu wa ugani waliopo kila kata.

Kulia ni Maxmilian Donard,mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Biharamulo,akimkabidhi miche ya kahawa Domisian Kahigi(mkulima wa kahawa)

“Niwaombe sana wananchi mnaokusudia kugawiwa miche hii leo,muone thamani ya fedha nyingi zilizowekezwa na serikali ya awamu ya sita kwaajili ya uzalishaji wa miche hii kuja kwenu,kama alivyotangulia kusema Ofisa kilimo wetu kila mche mmoja umegharamiwa takribani shilingi 300 mpaka kufikia hatua hii ya kwenda kupandwa shambani” amesema Mkandara.

Akizungumza na wananchi hao,mkuu wa wilaya ya Biharamulo, Kamishna mstaafu wa jeshi la polisi(SACP) Advera Bulimba, aliyewakilishwa na Ofisa tarafa ya Rusahunga, Maxmilian Donard,amesema serikali kwa kutambua kuwa kilimo ni uti wa mgongo wa taifa letu na kwamba aslimia 85 ya wakazi wa wilaya hiyo ni wakulima, ndiyo maana imeamua kuwasaidia wananchi kuinua uchumi wao.

“Hatua hii inakusudia kuongeza pato la wakulima kwa kuongeza jitihada za utoaji miche bora na mbegu mbalimbali,mbolea ya ruzuku,ugawaji wa matekta pamoja na kuwawezesha wagani wetu wote kupata usafiri ili kuwahudumia wakulima kwa haraka na kwa ukaribu zaidi”

“Aidha miche yote inayogawiwa leo na kuendelea ikapandwe kwa kuzingatia kanuni za kilimo bora na kutunzwa ikiwa ni pamoja na miche yote ya zamani ambayo imezeeka ikafanyiwe usafi na kutoa matawi yakiyozeheka ili yaweze kuchipua upya na kuongeza uzalishaji” amesema Bulimba.

Mwenyekiti wa halmashauri hiyo,Leo Rushahu, amesisitiza wataalamu wa ugani kuwasaidia wakulima hao kuitunza miche hiyo kwa ubora wa hali ya juu ili kupunguza idadi ya miche inayoweza kuharibika kutokana na gharama kubwa iliyowekezwa na serikali.

Kulia ni Maxmilian Donard,mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Biharamulo na wa mwanzo kushoto ni Ofisa Kilimo wa wilaya hiyo,Dkt. Sospeter Mashamba,wakikagua kitalu cha miche ya kahawa kabla ya uzinduzi wa ugawaji kwa wakulima.

Vile vile amesema maendeleo ya wananchi hao yataendelea kutekelezwa na serikali kutokana na ukusanyaji wa mapato kutoka vyanzo mbalimbali ikiwemo mazao ya chakula na biashara.

Baadhi ya wakulima hao akiwemo,Domisian Kahigi,na Paul Mkamu,mbali na kuipongeza serikali kwa kuwasaidia miche hiyo bure,wamesema wanamatumaini makubwa ya kuondoka kwenye lindi la umaskini kutokana na mapato yatakayotokana kupitia kahawa hiyo ambayo ni miongoni mwa mazao mkakati ya kibiashara nchi.

“Tunayo matumaini makubwa sana ya kuondoka kwenye lindi la umaskini kutokana na bei ya kahawa inavyozidi kupanda,maana kwa msimu wa mwaka jana baadhi ya wakulima wameuza kahawa yao kwa zaidi ya sh.5,000 kwa kila kilo moja,na huenda msimu huu inaweza kupanda zaidi na ifikapo miaka mitano ijayo tunaamini tunaweza kuuza kilo moja kwa sh. 8,000 hadi 10,000 kwa kilo” amesema Mkamu.