Rais wa Marekani Joe Biden anayetarajia kukabidhi madaraka kwa rais mteule Donald Trump Januari 20, ametoa Jumatano jioni hotuba ya kuaga na kuelezea wasiwasi wake kwa utawala ujao.

Katika hotuba hiyo, Biden amesema Marekani inaangukia mikononi mwa matajiri wachache ambao matokeo yake ni hatari ikiwa hawatodhibitiwa.

Bila kuwataja, Biden aliwakusudia mabilionea ambao wameonekana kumuunga mkono Trump ikiwa ni pamoja na Mmiliki wa kampuni ya Tesla Elon Musk, mmiliki wa kampuni ya Amazon Jeff Bezos na Mark Zuckerberg anayemiliki kampuni ya Meta inayojumuisha mitandao ya kijamii ya Facebook na Instagram.

Biden amesema utawala wa matajiri hao unachora sura mpya ya Marekani na unatishia demokrasia, haki za msingi pamoja na uhuru. Rais huyo wa 46 wa Marekani ametaja kusikitishwa na kitendo cha kusambazwa kwa msururu wa taarifa potofu akitaka mitandao ya kijamii kuwajibishwa na kuwepo sheria ya kudhibiti matumizi ya akili mnemba (AI).