Rais wa Marekani Joe Biden amempa mwanawe Hunter Biden msamaha wa rais na kumuepushia kifungo jela kutokana na makosa ya umiliki wa bunduki kinyume cha sheria na madai ya kukwepa kulipa kodi.
Kwa hatua hiyo, Rais Biden amekwenda kinyume na ahadi yake ya awali ya kutotumia nguvu zake za urais kwa manufaa ya familia yake.
Katika taarifa iliyotolewa jioni ya Jumapili, Biden alisema, “nauamini mfumo wa sheria, ila kwa kuwa nimepambana na hili, naamini pia kwamba siasa zimeingia kati katika kesi hii na zimepelekea kutopatikana kwa haki.”
“Madai katika kesi yake yametokea tu baada ya wapinzani wangu kadhaa wa kisiasa katika Congress kuyatumia kunishambulia na kupinga kuchaguliwa kwangu,” aliongeza Biden. “Hakuna mtu yeyote mwenye busara atakayeutazama ukweli katika kesi ya Hunter, atakayefikia maamuzi mengine mbali na kuwa Hunter alilengwa kwa kuwa ni mwanangu.”
“Natumai raia wa Marekani wataelewa kwanini baba na rais atafikia uamuzi huu,” aliongeza Biden.