Rais mteule wa Marekani Donald Trump jana Jumatano alifika Ikulu ya White House kwa mara ya kwanza tangu aliposhinda uchaguzi wa wiki iliyopita. Mazungumzo yao yalidumu kwa muda wa saa mbili.

Trump na Rais Joe Biden anayemaliza muda wake, ambao ni mahasimu wa muda mrefu wa kisiasa, walijadili mizozo ya Ukraine na Mashariki ya Kati, sambamba na makabidhiano ya amani ya madaraka.

Biden amempongeza Trump kwa ushindi wake, wakati alimpokaribisha katika ofisi ya rais na kusalimiana naye kwa kushikana mkono, akimuahidi mchakato mzuri wa kumkabidhi mamlaka. Miaka minne iliyopita, baada ya kushindwa katika uchaguzi, Trump mwenyewe alikataa kushiriki katika utaratibu huo wa kukabidhi madaraka.

Msemaji wa Ikulu ya White House Karine Jean-Pierre, aliwaeleza waandishi wa habari kwamba viongozi hao wawili wamejadili masuala muhimu kuhusu usalama wa kitaifa na sera za ndani zinazolikabili taifa hilo na ulimwengu. Mazungumzo yao yalidumu kwa muda wa saa mbili.Rais mteule Donald Trump awateua wapambe wake

Naye mshauri wa usalama wa kitaifa Jake Sullivan alisema Biden alitoa msisitizo kwa Trump kwamba ni muhimu kuendeleza uungaji mkono wa Marekani kwa Ukraine dhidi ya Urusi. Kulingana na Sullivan, Biden amesema uungaji mkono kwa Ukraine ni bora kwa usalama wa taifa wa Marekani kwasababu Ulaya imara na thabiti itazuia nchi hiyo kujiingiza katika vita.