RAIS wa zamani wa Marekani Joe Biden ameikosoa vikali serikali ya Donald Trump kwa kile alichokiita “uharibifu wa haraka” wa mashirika ya kijamii akisema hatua hiyo itaathiri zaidi ya Wamarekani milioni 65.
Katika hotuba yake ya kwanza kubwa tangu aondoke Ikulu, Rais wa zamani wa Marekani Joe Biden alishambulia vikali mabadiliko ya haraka ya serikali yanayoendeshwa na Donald Trump, akidai kuwa juhudi hizo zimeathiri vibaya shirika la usalama wa jamii na kuweka hatarini mafao ya uzeeni na ulemavu kwa mamilioni ya Wamarekani.
Akizungumza katika kongamano la haki za watu wenye ulemavu mjini Chicago, Biden alisema wafanyakazi 7,000 wa Idara ya Usalama wa Jamii tayari wameondolewa kazi, huku huduma muhimu kama tovuti ya shirika hilo zikiathirika vibaya.
Biden, ambaye aliacha kuwania urais kutokana na umri na wasiasi wa kiafya, alionekana kukumbwa na changamoto ya kutamka baadhi ya sentensi, hali iliyotumiwa na Trump kumkejeli kwa kuchapisha video ya hotuba hiyo mitandaoni.
Akilenga kushinikiza mabadiliko, Biden alisema mamilioni ya Wamarekani hutegemea mafao hayo kwa maisha ya kila siku na kuonya kuwa kuyakata kutasababisha madhara makubwa kwa familia zisizo na msaada wa kifedha.
