KILINDI

Na Bryceson Mathias

Ajuza mkazi wa Mgambo, Kwediboma wilayani Kilindi mwenye umri wa miaka 100, Fatuma Makame, ameapa kuwafikisha mahakamani maofisa wa serikali na wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi akiwatuhumu kwa kuhujumu chanzo chake cha kipato.

Bibi huyo anayefahamika pia kwa jina la Bibi Kidude II, amesema maofisa hao wamekata, kufyeka na kuteketeza kwa moto mazao yake.

Akizungumza na JAMHURI huku akitokwa machozi, Bibi Fatuma amesema mazao hayo ndiyo yaliyokuwa yakimpatia riziki.

“Hawa wanataka nife haraka. Katika kupigania haki yangu, nitawashitaki mahakamani kwa majina yao, kwa kuwa ni wao ndio wanaohusika,” amesema.

Bibi Fatuma amelionyesha gazeti hili nyaraka kadhaa za malalamiko ya kunyang’anywa ardhi ikiwamo barua yenye kumbukumbu namba KDC/E.10/13/23 ya Julai 13, 2015 (nakala tunayo).

Amesema tayari amekwisha kufikisha majina yao ofisi za Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya na kwa Rais Samia Suluhu Hassan. 

“Nimemuomba na kumlilia mwanangu (Rais Samia) nikimwambia kuwa watu aliowaamini na kuwapa vyeo, wamegeuka kuwa wanyama kwa masilahi yao.

“Hawatutetei tena, ila wanatunyang’anya haki zetu na kuteketeza mazao wakitusababishia umaskini tupate presha na tufe haraka. Kama ingekuwa ni ndugu zao, wasingefanya hivyo,” amesema.

Ameiomba serikali kuwahamisha vigogo hao kama ilivyofanya kwa maofisa wa polisi waliohusishwa na uzembe na kusababisha mauaji ya wakulima na wafugaji, akitaka wawajibishwe kwa ukatili wao.

Ameziomba taasisi za kiraia za kutetea haki za binadamu kumsaidia kupata haki na wenzake waliovunjiwa nyumba na kuteketezewa mazao.

“Huenda wanafanya hivyo kuficha ukweli ambao wananchi wa Mgambo tunahoji ziliko Sh milioni 16 kati ya Sh milioni 30 zilizotolewa na Papa Yohane Paulo II mwaka 1993,” amesema Bibi Kidude II.

Fedha hizo zilitolewa baada ya Papa kufurahishwa na uimbaji wa wanafunzi wa Mgambo na kuomba zitumike kujengea shule.

Amesema anaamini miongoni mwa fedha hizo zilipaswa kutumika kufidia wakazi wa Mgambo walionyang’anywa maeneo.

Serikali, kupitia barua yenye Kumb. EA.171/176/01 ya Mei 29, 2020 ya aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, ilimuagiza Mkuu wa Wilaya ya Kilindi, kushughulikia mgogoro huo kwa amani na si kuvunja nyumba za watu na kuteketeza mazao.

Akizungumzia suala hilo, Mkuu wa Wilaya ya Kilindi, Abel Busalama, amesema: “Siijui barua hiyo, ila malamiko haya nimeyakuta yakimhusu mtangulizi wangu.”

Busalama ni mmoja wa viongozi waliomo kwenye orodha ya kushitakiwa mahakamani na Bibi Fatuma.

Kinyume cha agizo la Lukuvi, mbali ya mmoja wa walalamikaji kushinda kesi mara zote, Mwenyekiti wa Baraza la Ardhi Kilindi, kwa mshangao wa wengi, alitoa amri ya kuvunja nyumba na kuteketeza mimea ya walalamikaji.

Uvunjaji huo ulifanyika Februari 21, 2022.

Mwanasheria na Wakili wa Mahakama Kuu, Jebra Kambole, amesema ipo sheria inayoruhusu mtu kumiliki ardhi baada ya kuishi hapo kwa miaka 12 bila kusumbuliwa na yeyote.