Na Isri Mohamed
Imezoeleka siku ya harusi ni siku ya furaha, shangwe, nderemo na vifijo hasa kwa maharusi wenyewe, lakini imekuwa tofauti kwa Mr Emile ambaye ameshuhudia mke wake akifariki mbele yake na wageni wakiwa ukumbini kwenye sherehe yao, ikiwa ni saa chache tu baada ya kutoka kanisani kufunga ndoa .
Tukio hilo la kusikitisha limetokea katika ukumbi wa sherehe wa hoteli ya zamani ya Johannesburg huko Akwa North, Douala, Oktoba 26, 2024, ambapo Bibi harusi Sorelle Manuella, alishika maiki kumuimbia mumewe kipenzi wimbo maalum, lakini ghafla akaanguka na kukimbizwa katika hospitali ya Ad Lucem Sable, na walipomfikisha daktari akathibitisha kwamba ameshafariki.
Tuhuma mbalimbali zimeibuka kwenye mitandao ya kijamii baada ya kifo chake, ambapo inadaiwa Manuella alipewa sumu na mtu ambaye bado hajafahamika.
Manuella amemuacha mume wake kwenye huzuni na majonzi, pamoja na mabinti zake watatu, huku wa mwisho akiwa hajatimiza hata mwaka mmoja.