Wakati baba yangu mzazi akifariki katikati ya miaka ya 1990, alikuwa mmoja wa wafanyabiashara waliokuwa wakipanda kwa kasi kubwa kibiashara. Akiwa ameshakusanya uzoefu wa kusafiri kibiashara hadi nchi jirani ikiwamo Malawi, alifariki dunia na kuacha biashara zilizokuwa zimestawi kweli kweli.
Baada ya kuondoka kwake, mama yangu alijaribu kuvaa viatu vyake, lakini mambo yalimwendea kombo. Alipambana kuzisuka upya biashara zile, akabadilisha jina na kutafuta masoko mapya. Ni kama alikuwa akianza upya kabisa kwa sababu mtangulizi wake (mume wake) hakuacha urithi kamili wa kimfumo.
Haikupita miaka mingi kabla ya mama yangu kuyumba kutokana na kuzidiwa na changamoto na ushindani wa kibiashara. Sababu kubwa ya mama kushindwa kuhimili mikiki ya biashara zile ni baba (wakati wa uhai wake) kutomshirikisha mama kwa asilimia 100 kuhusu uendeshaji wa biashara zile.
Ingawa mama alikuwa akisimamia maduka kwa maana ya kuuza, hakuwa akijua mali zinachukuliwa wapi, hakuwahi kusafiri naye kufuata bidhaa, hakujua biashara zina madeni kiasi gani na pia hakuwa anaelewa kikamilifu mfumo kamili wa biashara zile kwa jumla.
Ndugu zangu Wakinga (na mimi ni Mkinga pia) wengi wao wana tatizo hili. Licha ya kuwa wana mafanikio makubwa katika tasnia ya biashara, ni wachache wanaowashirikisha wake zao kwa asilimia 100 kwenye biashara zao.
Ninao jamaa zangu Wakinga wanaotamba na maduka ya nguo maeneo ya Kariakoo wakiwa wanafuata bidhaa China, Uingereza na Dubai, lakini wengi wao wake zao hawajui hata tiketi ya ndege inavyofanana. Ndiyo maana kumekuwa na uvumi (myths) mwingi kuwa Wakinga wengi wanapofariki biashara huwa zinawafuata makaburini.
Uvumi huo husemwa kuwa ni kwa sababu ya kutumia ushirikina. ‘Stori’ za Wakinga na ‘janja’ yao ya biashara za kishirikina zimetapakaa sana hasa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini ambako ndiko wanakotamba kibiashara. Hata hivyo, kuna sababu ya kisayansi zaidi ya huo uvumi kutokana na suala la mtu kufariki dunia na kisha biashara zake kumfuata kaburini. Hili la ushirikina nitalichambua katika makala inayojitegemea huko mbele.
Kwa bahati mbaya ni kuwa si Wakinga pekee, bali biashara nyingi za Watanzania ndivyo zilivyo. Ni biashara chache sana zinazofanikiwa kuhimili au kukua ndani ya miaka 10 mara baada ya mmiliki wake kufariki dunia. Ni kwa nini mambo haya hutukia?
Nimetoa kisa cha wanaofariki dunia na biashara kuwafuata, lakini ngoja niongezee kitu kingine ili nishushe vizuri mantiki ya biashara za kisasa na u-kisasa. Katika makala mbili zilizotangulia niliwaeleza namna nilivyojikwamua kiuchumi hadi kufungua chuo cha mafunzo ya kompyuta na biashara.
Nasikitika kuripoti kuwa biashara hiyo iliyumba na nikajikuta nimefilisika kabisa. Kufilisika huko ndiko chimbuko la leo kuiandika makala hii. Nilipochora jedwali la kibiashara kutoka marehemu baba yangu, baadaye mama yangu na hatimaye mimi mwenyewe, nikagundua mambo mengi yaliyokuwa ni somo mwanana nilipokuja kuanza upya katika biashara nyingine.
Watanzania wengi tunaendesha biashara kienyeji. Hatuna mifumo ya kibiashara, hatuna malengo ya biashara na wala hatuna mwelekeo wa kibiashara. Wengi wetu tunategemea kudra za Mwenyezi Mungu kutufikisha mwakani, hatuna uhakika na tunakokwenda wala hatujui tutafika lini! Tuna macho ya kuitazama leo tu ila hatuna malengo angalau hata ya muongo mmoja.
Watanzania wenzetu wenye asili ya Kihindi na Kiarabu wametuzidi sana katika hili. Wenzetu hawa wana tamaduni imara za kibiashara kiasi ambacho matajiri wengi tunaowasikia sasa wenye asili hii, mali hizo wamerithi – ama kutoka kwa baba au babu zao. Mhindi au Mwarabu hawezi kuanzisha biashara halafu ikafa kirahisi!
Pengine tofauti na zamani, nyakati za sasa zinahitaji biashara kuendeshwa katika mifumo ya kisasa. Utunzaji wa hesabu, utafutaji wa masoko, kuhimili ushindani sokoni, kubadilisha bidhaa kuendana na mahitaji ya soko; yote haya ni mambo yanayohitaji u-kisasa. Biashara za kuuza samaki miaka nenda rudi bila kubadilika, au kufanya biashara za magari bila kuboresha huduma, si rafiki tena kwa sasa.