Hihitaji mamilioni kuzalisha mabilioni isipokuwa unahitaji wazo, taarifa, uwezo wa kuwasiliana na ujasiriamali vitakavyokuletea mabilioni.
Vile vile miaka ya hivi karibuni hapa nchini Tanzania kuna vijana wamebuni mfumo wa kukata tiketi kwa kutumia simu za mikononi.
Kinachofanyika ni kwamba unakata tiketi yako kwa kutumia simu yako katika basi unalolitaka.
Sitashangaa hata kidogo nitakapokuja kusikia kwamba kampuni hii ya kukatisha tiketi ina thamani kubwa kuliko makampuni ya mabasi!
Kuna mambo mawili ninataka uyabaini yaliyomo katika ulimwengu mpya wa biashara.
Mosi ni kwamba ukianzisha biashara leo; kuna urahisi mkubwa wa kusambaa dunia nzima ndani ya muda mfupi.
Hii ni kwa sababu huhitaji kufika mahali ambako bidhaa ama huduma zako zinafika. Mawasiliano yanaweza kukusambazia bidhaa na huduma zako kwa uharaka.
Pili; katika ulimwengu mpya wa biashara muda wa kupata faida na utajiri umepungua. Hauhitaji kusubiri miaka mingi ili utajirike.
AngloGold ilianzishwa makumi ya miaka huko nyuma, ikiwa imewekeza mabilioni ya dola katika miaka yote hiyo, lakini inafukuzwa kwa karibu sana na kampuni yenye umri wa miaka karibu mitano pekee tena ikiwa haijawekeza mabilioni ya dola!
Katika zama mpya uwekezaji wa mamilioni unaendelea lakini si lazima uwe na mabilioni ili uwekeze; bali unahitaji mawazo, taarifa, maono na ujasirimali.
Pengine mtaji mkubwa sana katika zama kama nilivyosema hapo juu ni ubongo (kufikiri kwa kina). Bahati mbaya ni kwamba kufikiri ndio kazi ngumu kuliko zote huku duniani ndio maana ni wachache wanaojihusisha nayo.
Dunia ya sasa inaongozwa na misukumo mikubwa mitatu; urahisi, uharaka na unafuu. Mtu ananunua bidhaa ama huduma kwa kuangalia Je, ni rahisi kiasi gani kupatikana? Je, ni kwa haraka kiasi gani ataipata na ni kwa unafuu(bei) kiasi gani ataipata? Kama uko kwenye biashara yeyote ni lazima ujiulize, Je, biashara yako inahimili misukumo hiyo mitatu inayotawala soko la zama hizi?
Mathalani; leo hii mtu akihitaji kupata wimbo, filamu ama rekodi fulani anafikiria harakaharaka kuingia mtandaoni kwa kutumia simu ama komyuta yake (urahisi).
Akiupata, ndani ya dakika chini ya tano anakuwa ameshaupakua na anausikiliza (uharaka), na kwa kutumia kifurushi cha inteneti pengine cha shilingi elfu mbili anaweza kupata nyimbo mia moja(unafuu).
Nyimbo mia moja ni sawa na wastani wa santuri 10 (CDs), ambazo zingemgharimu si chini ya 50,000! Hata kama wimbo huo unauzwa huko mtandaoni, bei yake inakuwa ni chini sana ukilinganisha na kununua CDs au kanda.
Kwa kuungalia mfano huu, unaweza kutabiri changamoto zinazowapata na zitakazoendelea kuwapata wafanyabiashara wa maduka ya kanda ambao hawajifunzi na kubadilika kutegemea mabadiliko haya.
Kubadilika hauhitaji fedha nyingi (na unaweza usihitaji hata shilingi kumi) ila unahitaji wazo na taarifa.
Ukiitazama misukumo hiyo mitatu inayoongoza wateja wa zama za kizazi cha taarifa utabaini kwamba inaegemea katika starehe (luxury style).
Ni kwamba wateja wa nyakati mpya hawataki shida, hawataki kuhangaika, wanataka kuishi na kuchukuliwa kifalme. Hili limepelekea wajasiriamali wengi kuwa wabunifu kila siku, wakiibuka na huduma na bidhaa mpya.
Hivyo ikiwa umo kwenye biashara yeyote na ukawa ‘mvivu’ wa kufikiri kivingine, ukawa mzito wa kubadilika kwa kubadilisha ama kuboresha biashara; uwe na uhakika kwamba zama mpya zitakuondoa sokoni ‘mchana kweupe’!
Badala ya kwenda mpaka stendi ya basi kukata tiketi mteja anataka kukata tiketi yake huku akiwa amekaa kwenye kochi lake sebuleni akiangalia runinga(Ole kwa wakatisha tiketi stendi!)
Badala ya kwenda benki kupanga foleni kwa ajili ya kutuma pesa, mteja anataka kufanya hilo kwa kutumia dakika chache na akiwa popote pale kupitia simu yake.
Misukumo hii mitatu inaweza kufanikishwa na uwepo wa huduma bora. Ndio maana nilikueleza kuwa uchumi wa taarifa (Information economics/Information age) unaendana sana na uchumi wa huduma (service economics/service age).
Biashara yeyote ni lazima ihakikishe inatimiza misukumo hii mitatu kwa wateja. Uchumi umebadilika, biashara zimeingia ulimwengu mpya na wateja nao wamebadilika.
Kama unaanzisha mgahawa leo ni lazima ujue wateja wanataka, kupata chakula kwa uharaka, kwa unafuu wa bei na kwa urahisi lakini pia mazingira yawe ‘luxury’.
Ndio maana badala ya kusubiri wateja waje mgahawani kwako unaweza kutengeneza utaratibu wa kuwapelekea vyakula, maofisini na hata majumbani mwao.
Kama ambavyo inachukua muda mfupi kufanikiwa na kutajirika katika zama mpya, vile vile inachukua muda mfupi kuanguka na kufilisika!
Hii ni kwa sababu sifa kubwa ya uchumi wa taarifa ni ushindani mkali usio kifani. Kukaa katika biashara yeyote siku hizi; ukizalisha faida mfululizo kwa miaka zaidi ya kumi; sio kazi nyepesi hata kidogo; ni lazima uwe mjanja sana, uwe unaebadilika haraka na uwe mtu unaetafuta taarifa, kuzichakata na kuzitumia kwa haraka sana. Biashara isiyouingia ulimwengu mpya, kufa na itakufa tu!
TAMATI
Whatsapp +255 688 726 442