Awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia uhai mpaka tukapata fursa ya kubadilishana mawazo juu ya umuhimu wa mkaa na athari zake kwa mazingira. Vilevile napongeza sana menejimenti ya Mwananchi Communications Limited na ITV/Radio One chini ya IPP Media; kubuni na kuandaa mjadala juu ya “Biashara ya Mkaa na Mazingira”. Hongereni sana.
Vilevile namshukuru Mheshimiwa Januari Makamba, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais –Mazingira, kwa takwimu na maelezo mazuri. Kwa kufanya hivyo aliweka msingi mzuri wa majadiliano kwa wachangiaji waliofuata.
Mkaa ndicho chanzo kikuu cha nishati ya kupikia katika miji nchini Tanzania. Zipo sababu kadhaa ikiwemo: urahisi wa kupata mkaa kutokana na kusambazwa kirahisi hadi sehemu zisizofikika kirahisi ambako vitendea kazi kama baiskeli, pikipiki pia mikokoteni hutumika.
Vilevile gharama za mkaa ni rafiki kwa mtumiaji ukilinganisha na umeme, gesi au mkaa mbadala (briquettes). Mathalani, kununua mkaa kwa matumizi ya kila siku ni njia rahisi kumudu maisha kuliko kununua nishati kama gesi ya LPG au kulipa gharama za umeme.
Inakuwa rahisi kubangaiza ukapata kiasi kidogo cha fedha ukilinganisha na kupata Sh 15,000 au zaidi na zote zikaishia kununua gesi.
Kwa mtazamo wetu inaonekana mkaa ni chanzo rahisi cha nishati ya kupikia, pia ni chanzo cha mapato kwa Watanzania mijini na vijijini, ukianzia na watengenezaji, wapakiaji, wasafirishaji, wapakuaji, wasambazaji wakubwa, wauzaji rejareja na watumiaji: hivyo wadau wengi wananufaika kupitia mnyororo huo.
Kulingana na mazingira ya biashara ya mkaa yalivyotunaweza kusema “ndiyo” mkaa ni nishati rahisi (cheap) ingawa kiuhalisia si kweli. MheshimiwaMakamba alijitahidi kulifafanua hili kwamba iwapo miti ya asili inayotumika kutengeneza mkaa ingelipiwa ipasavyo, mkaa usingeonekana ni wa bei rahisi ukilinganisha na vyanzo vingine vya nishati. Maeneo mengi ya misitu ya asili hayana usimamizi wa kutosha kiasi kwamba kila anayetaka kufanya apendavyo huingia na kujihudumia. Hivyo watengeneza mkaa wanakata miti yenye thamani kubwa (mfano, mininga, mipingo na miyombo) na kutengeneza mkaa bila kuigharimia, halafu tudai mkaa kuwa bei rahisi, je, ni sawa hiyo?
Serikali inatoza kiasi kidogo cha fedha kwa kila gunia la mkaa ambacho hakilingani na thamani ya miti iliyotumika kutengeneza mkaa. Iwapo miti ingelipiwa sawa sawa tusingethubutu kusema mkaa ni rahisi, maana ungepambana na vyanzo vingine vya nishati. Sheria ya Misitu (Sura 323 RE: 2002) inakataza kukata miti ya asili bila kuwa na kibali (harvesting permit), pia hairuhusiwi kuvuna miti kwenye eneo ambalo halina Mpango wa Usimamizi (Management Plan). Kwa misingi hiyo ya kisheria, karibu mkaa mwingi unaotumika nchini ni biashara Haramu, maana sheria na taratibu havifuatwi. Wadau wanafanya hivyo wakijua usimamizi wa misitu ya asili ni hafifu. Watumishi wa umma kupitia Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) na Serikali za Mitaa ni wachache sana na vitendea kazi havitoshelezi. Hivyo wengi wanakata miti bila kuulizwa wala kudhibitiwa inavyotakiwa kisheria na udhaifu huu unachangia kuuona mkaa kama ni bidhaa rahisi sana kupata na kutumia.
Matumizi ya mkaa yanaongezeka kila mwaka kutokana na ongezeko kubwa la watu wanaoishi mijini. Mwaka 2012 tani zaidi ya milioni 2.3 za mkaa zilitumika, ikiwa ni takriban thamani ya Sh bilioni 980 na wanufaika wa moja kwa moja wakifikia 225,000. Hii ni biashara kubwa, lakini pia ni njia kuu ya kuharibu misitu ya asili na kuhatarisha mazingira. Mathani, utaalamu na teknolojia ya kutengeneza mkaa ni duni na husababisha miti mingi kukatwa kupata mkaa kidogo (tani moja ya mkaa hutumika tano 10 mpaka tani 12 za miti).
Mwaka 2009 Benki ya Dunia ilikadiria kuwa biashara ya mkaa iliingiza dola milioni 650 za Marekani. CAMCO mwaka 2014 walikadiria biashara ya mkaa kufikia dola bilioni moja za Marekani.
Sehemu kubwa ya biashara hiyo ikifanyika Dar es Salaam na kwenye miji mikubwa kama Mwanza, Arusha na Mbeya.
Ukusanyaji tozo kwa mkaa unakabiliwa na changamoto nyingi, kuanzia unapotengenezwa na kusafirishwa bila kuzingatia taratibu na sheria. Kwa bahati mbaya masuala ya mkaa, kama chanzo muhimu cha nishati ya kupikia hayajapewa msukumo wa kutosha kitaifa. Watunga sera na wafanya uamuzi tumekuwa na mazoea kuuona mkaa mwingi pembeni mwa barabara zetu na wanunuzi wakifanya hivyo bika shida. Mwishowe watumiaji wanapata na hakuna anayelalamika, hivyo ikawa ni biashara ya kimazoea bila sera madhubuti ya kusimamia na kuhakikisha mkaa unanufaisha nchi bila kuathiri mazingira.
Kimsingi Wizara ya Nishati imeweka mkazo kwenye kuendeleza vyanzo vingine vya nishati: umeme; gesi na bidhaa za mafuta (petroleum products). Ni muhimu kuwapo na sera inayoeleweka kuhusu nishati ya kupikia na huu ni wajibu wa Wizara ya Nishati na si jukumu la Wizara ya Maliasili na Utalii. Kazi kuu ya wataalamu wa misitu ni kutunza na kusimamia rasilimali misitu ili bidhaa zitakazotokana nayo (mbao, magogo, kuni, mkaa, nguzo) ziwe endelevu bila kuathiri uwezo wa misitu kuhifadhi mazingira na kuendeleza huduma za kiikolojia; mfano, kutunza vyanzo vya maji.
Vilevile, miti iliyokomaa ndiyo inatakiwa kuvunwa, lakini kwa sababu uwezo wa TFS na Serikali za Mitaa kudhibiti hali hiyo ni mdogo; misitu ya asili mingi haina usimamizi, hivyo watu wanavuna miti bila ruhusa na hukata miti michanga. Isitoshe miti inayotengeneza mkaa hailipiwi, hivyo husababisha mkaa uonekane nafuu ukilinganisha na nishati nyingine.
Gharama halisi za mkaa zikijumlisha kulipia thamani ya miti ipasavyo, zitaufanya mkaa usiwe bei nafuu kama tunavyofirikia.
Mwisho, nashauri watunga sera na wafanya uamuzi (policy/decision makers) waone upatikanaji wa nishati ya kupikia kama ni jukumu la Wizara ya Nishati. Hivyo kuwapo sera na taratibu za kisheria na usimamizi madhubuti katika Wizara ya Nishati ili uwajibikaji juu ya nishati ya kupikia uwe wa uhakika.
Pili, mamlaka za kusimamia misitu kama TFS, Serikali za Mitaa naIdara ya Misitu ziwajibike kusimamia utekelezaji wa sera na sheria za misitu na kuzuia kukata miti michanga, pia kuhakikisha rasilimali-misitu inanufaisha taifa na mkaa ukiwa ni zao endelevu.
Usimamizi wa misitu uimarishwe ili yeyote atakayekata miti afuate taratibu za kisheria. Mkaa kutoka rasilimali-misitu utumike kupikia au kufanya kazi nyingine, hilo lisiwe jukumu la wanaosimamia misitu, bali kwa mamlaka zinazohusika na masuala ya nishati kama EWURA. Iwe hivyo kwa ubora wa mbao, mamlaka ya viwango ihusike na idhibiti ipasanyo.
Mwandishi wa makala hii, Dk. Felician Kilahama, ni Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania (TAFORI). Anapatikana kwa simu: 0756 007 400.