Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge, William Lukuvi, amesema Serikali inafanya uchunguzi ili kujiridhisha kama watu 19 waliokamatwa nchini China na dawa za kulevya ni Watanzania.

Waziri Lukuvi amesema uamuzi huo umefikiwa baada ya kuibuka kwa tabia ya baadhi ya watu wanaokamatwa na dawa za kulevya, kubainika kuwa wanaghushi hati za kusafiria ili waonekane kuwa ni raia wa Tanzania.

Sisi JAMHURI tunasema kuchukua hatua za kuwabaini wanaoghushi hati za kusafiria kwa lengo la kujihusisha na biashara haramu ya dawa za kulevya, hakuwezi kuleta ufumbuzi wowote wa tatizo hili. Kitendo cha kughushi hati hizo hakiwezi kufanywa na upande mmoja tu. Pasi shaka yoyote maofisa wa Serikali wasiokuwa waaminifu wanajihusisha kwa kuhakikisha wafanyabiashara wa dawa za kulevya wanaweza kusafirisha dawa hizo kwa urahisi zaidi.

Tatizo la dawa za kulevya nchini limekuzwa na propaganda za kisiasa zinazotolewa mara kwa mara, kwamba lengo ni kukomesha biashara hiyo huku mamia ya vijana wa Kitanzania wakiathiriwa na matumizi ya dawa hizo. Kwa kipindi cha Oktoba 23 hadi 29, mwaka huu, dawa za kulevya zilizokamatwa ni heroin kilo 82.297, cocaine gramu 894.28 na bangi magunia 267. Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa waathirika wa matumizi ya dawa za kulevya ni 1,805 wakiwamo wanawake 232.

JAMHURI tunasema biashara hii imekithiri nchini kwa muda mrefu huku baadhi ya viongozi wakiibuka na kudai wapelekewe majina ya vigogo wote wa dawa za kulevya ili wachuliwe hatua, lakini hadi sasa hakuna aliyethubutu hata kuwataja tu.

Tangu utawala wa Awamu ya Tatu chini ya Rais Benjamin Mkapa, majina hayo yamekaliwa Ikulu na hakuna aliyethubutu kutaja jina lolote na leo tunatafuta kuthibitisha majina ya wanaokamatwa na dawa hizo nchini China!

Biashara hii haramu inayoangamiza maelfu ya vijana haiwezi kumalizwa kwa propaganda za wanasiasa ambao hawana ujasiri wa kuchukua uamuzi mgumu wenye lengo la kuwanusuru vijana wanaoangamia.

Tunasema badala ya kubaini majina ya watu waliokamatwa na dawa hizo, Serikali inapaswa kutoa elimu kwa wananchi hususani vijana, ambao ndiyo watumiaji wakubwa wa dawa za kulevya.

Kupambana na biashara hii kisiasa hakuwezi kuleta ufumbuzi wowote wa tatizo, ni viongozi wa kweli, wenye ujasiri na huruma kwa wananchi wanaoangamia kwa dawa za kulevya, wanaoweza kupambana na uhalifu huu.