Serikali imekusanya Shilingi bilioni 192.78 kutokana na biashara mtandaoni, ikiwemo michezo ya kubahatisha, kati ya Julai 2024 hadi Machi 2025, kutoka kwa kampuni 1,820 zilizosajiliwa rasmi.

Taarifa hiyo imetolewa bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe, alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Dk. Ritta Kabati, aliyetaka kufahamu hatua za serikali katika kusimamia na kudhibiti biashara hiyo.

Kigahe amesema, kutokana na ukuaji wa kasi wa biashara mtandaoni, serikali iko katika hatua za mwisho za utekelezaji wa Mkakati wa Kitaifa wa Biashara Mtandao (National Electronic Commerce Strategy), ambao unalenga kuhakikisha mfumo thabiti wa usimamizi wa biashara hiyo ili kuendana na mabadiliko ya kiteknolojia na kuongeza mapato ya taifa.

Ameeleza kuwa mkakati huo utahusisha maboresho katika maeneo mbalimbali ikiwemo miundombinu ya TEHAMA, sera, sheria, huduma za mawasiliano, usafirishaji, miamala ya mtandaoni, pamoja na kutoa elimu kwa umma kuhusu matumizi salama ya biashara za mtandao.

Akijibu swali la nyongeza la Dk. Kabati kuhusu udhibiti wa utapeli mtandaoni, Kigahe amesema serikali imeanzisha mkakati huo ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Biashara ya Mwaka 2003, Toleo la 2023. Pia, amebainisha uwepo wa sheria mbalimbali kama Sheria ya Usalama wa Taarifa Binafsi ya 2022 na Sheria ya Makosa ya Mtandao ya 2015.

Amesema pia serikali inaendelea kushirikiana na sekta binafsi kusaidia vijana wabunifu waliopo kwenye biashara hiyo. Mfano ni kampuni ya Fortune Technology inayomiliki app ya Swif Pack, inayoshirikiana na Shirika la Posta kuwezesha mfumo salama wa malipo ya bidhaa mtandaoni.