Wiki iliyopita wakati nikiangalia taarifa ya habari katika moja ya vituo vya televisheni hapa Tanzania, nilikutana na habari kuhusu wakulima wa mpunga walioandamana hadi Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa.

Walikuwa wakilalamikia ushuru mkubwa wanaotozwa na Manispaa hiyo. Katika kuwasilisha malalamiko yao, wakulima hao walidai kuwa ushuru mkubwa umekuwa ukiwapa hasara na wengi wao wanashindwa kumudu maisha, kukwama kurejesha mikopo yao na kushindwa na washindani wao.

 

Wakati nikiwafuatilia wakulima hao waliokuwa wakizungumza kwa uchungu mkubwa, nikakumbuka habari ya bei ya mchele ilivyotikisika hapa nchini. Itakumbukwa kuwa hivi karibuni Serikali iliruhusu uingizaji mchele kwa wingi kutoka nje ya nchi ili kukabili tishio la baa la njaa linaloweza kutokea.

 

Hadi naandika makala haya, uingizaji wa mchele kutoka nje ya nchi umeleta msiba mkubwa kwa wakulima na wafanyabiashara wa mchele katika maeneo mengi. Wale wakulima waliolima mpunga kwa gharama kubwa wanajikuta matatani kwa sababu watalazimika kuuza mchele wao kwa bei ndogo ili kushindana na ulioingizwa kutoka nje.

 

Ukiacha hilo, wapo wale wafanyabiashara ambao walihifadhi mpunga kwa matazamio ya kuuza kwa bei kubwa siku za baadaye; lakini sasa wanajikuta wakilazimika kuuza mchele kwa bei ndogo, tena wakati mwingine pungufu ya gharama walizonunulia!

 

Kilio cha wale walioandamana nikiunganisha na hili sekeseke la bei za mchele kwa sasa; ninapata funzo kubwa kuhusu hizi biashara. Biashara zinahitaji ramani, maono ya mbali, makadirio (timing), urahisi wa kubadilika na ubunifu wa hali ya juu sana. Vile vile biashara zinahitaji uwe mtu wa mibadala mingi sana. Yaani unapoendelea na biashara moja akili yako iwe inaperuzi huku na kule ili kujiweka tayari kwa ajili ya dharura yoyote.

 

Hakuna biashara inayodumu milele na hata zinazodumu milele, kuna wakati uwezo wa mjasiriamali unapungua na kujikuta unashindwa kuzimudu. Kibaya zaidi na ambacho ndicho tunachokiangalia katika makala haya ni mambo yanayojitoeza (external factors), yenye kuathiri biashara zako; lakini ambayo huna uwezo wa kuyadhibiti .

 

Na hizi, “external factors” ndiyo kama hizi za mamlaka za maeneo kupanga ushuru ama utaratibu fulani unaokubana ama Serikali kutengeneza sera au kufanya uamuzi (wenye kuwasaidia wananchi), lakini ambao unakuacha katika wakati mgumu kibiashara. Kwa kuwa biashara ndivyo zilivyo “wakati wote” ni lazima wafanyabiashara kujijengea uwezo na mbinu za kupambana na mambo haya “wakati wote”.

 

Hebu tutazame mifano kadhaa. Miaka michache nyuma kabla ya kuingia kwa bodaboda, biashara ya teksi ilikuwa inalipa sana. Wajasiriamali wengi “wakajipigapiga” na kuanzisha biashara ya teksi. Muda si muda ndugu zetu Wachina wakaleta bodaboda na Wahindi wakatumwagia bajaj, na “automatically” biashara ya teksi ikaanza kufifia. Hadi sasa ukipita maeneo mengi hapa nchini, wenye teksi wanalalamika kwa kudai kuwa biashara imekuwa ngumu ikilinganishwa na zamani.

 

Wajanja walioliona hilo mapema, wakaamua kuuza kabisa ama kupunguza teksi zao na kisha kununua bodaboda na bajaj. Wale waliojifungia na kudhani kuwa mabadiliko hayo hayawahusu wanapigwa na butwaa kuona kuwa “mambo hayaendi”.

 

Biashara zinahitaji akili za kijanja sana; unapoona kuna biashara inakupa faida leo, anza kuandaa biashara ya aina nyingine kesho. Miaka kadhaa nyuma kidogo kulikuwa na wafanyabiashara waliopata mafanikio kwa kuuza kanda, santuri na mikanda ya sauti na video.

 

Leo hii tunavyozungumza, biashara hiyo ina changamoto kali ajabu. Mtu badala ya kwenda dukani kununua santuri anakaa kwenye mtandao na ku-download bure ama kununua rekodi husika. Hata wale waliotoka kwa kuuza vocha za kukwangua mambo si shwari kwao.

 

Kwa sababu siku hizi watu wananunua muda wa hewani kwa benki za simu (M-Banking). Kama ulibweteka na kibanda cha vocha, si unajikuta umefulia? Utalalamika kuwa biashara siku hizi imebadilika, kumbe tatizo ni wewe mwenyewe kuwa mgumu wa kubadilika.

 

Angalia na hili pia: Kwa sasa Serikali imekazana kweli kweli kuboresha viwanja vya ndege na kufanya mapinduzi makubwa katika usafiri wa anga maeneo mengi. Muda si muda watu watapunguza kusafiri kwa mabasi na kugeukia usafiri wa ndege.

 

Mfanyabiashara yeyote wa mabasi kwa sasa anatakiwa kuanza kulitazama hili kwa sababu muda utakuja (haupo mbali), ambapo biashara “itakuwa ngumu” kwani abiria watakuwa wakikwea pipa. Kwa anayeona mbali ataanza kujiandaa mapema ama kwa kuondokana na biashara ya usafirishaji, au kujipanga kwa ajili ya kununua walau ndege.

 

Hata kama itachukua miaka kumi, hata kama mfanyabiashara utakufa haya hayajatokea, lakini kama una maono ya muda mrefu, biashara yako itaishi hata baada ya kufa kwako; na kama una mipango na maono hayo; unaowaachia “hawatafilisika” hata kama mambo yakibadilika kiasi gani.

 

Hatari ya upepo wa biashara kubadilika haiwapati wajasiriamali na wafanyabiashara wadogo pekee; isipokuwa inazikumba hata kampuni kubwa duniani kote.

 

Hapa nchini tulikuwa na kampuni kubwa za vinywaji baridi ambazo kwa miaka nenda rudi; licha ya kuzalisha bidhaa bora lakini zilikosa ubunifu katika ufungashaji.

 

Mteja unaponunua kinywaji kutoka katika kampuni hizi ilikuwa ni lazima urudishe chupa zao. Usumbufu huu wa urudishaji chupa ulikuwa na kero kwa kiasi fulani kwa wateja wengi hasa hasa wale wasafiri. Kwa kuwa bidhaa zao zinapendwa, wateja wengi ama walikuwa wanalazimika kutembea na chupa za kubadilishia, au kulazimika kuzinunua chupa hizo.

 

Kampuni kadhaa nchini ziliusoma usumbufu huo na zikaamua kuutumia kama fursa. Hata hivyo, kampuni moja hapa hapa nchini ikafanikiwa kuingiza sokoni bidhaa zenye vionjo, ladha na mtindo unaolandana na hizi kampuni “ya chupa”.

 

Kubwa walilolifanikisha likawa na kuondoa usumbufu wa watu kutembea na chupa za kubadilishia, kwani kampuni hii (iliyotumia usumbufu kama fursa) ikaja na chupa za plastiki ambazo ukinunua bidhaa unakwenda nayo moja kwa moja. Bidhaa hizi zilichangamkiwa kupita kawaida kiasi kwamba zilitishia kabisa uhai wa mauzo ya kampuni kongwe.

 

Kitu kilichonifurahisha mno na ambacho ninazipongeza sana hizi kampuni kongwe ni uharaka wao wa kubadilika. Zilipoona kuwa wateja wanakimbia zikaibuka na ubunifu wa kufungasha bidhaa zao zilezile katika chupa za plastiki pia. Hata mimi nimekuwa mmoja ya wateja “waliorudi kundini” baada ya ubunifu wao.

 

Kwa mifano hiyo, utabaini kuwa bila kuangalia kulia na kushoto na kujua wenzio/washindani wanafanya nini sokoni, utajikuta unapitwa na wakati pasipo kujua. Ndivyo biashara zilivyo, zinahitaji akili inayoona mbali sana, zinahitaji wale walio tayari kubadilika haraka kukabili mabadiliko na zinahitaji “wagumu hasa”, wa kukomaa huku wakikua kibiashara wakati wote.

 

Wafanyabiashara Tanzania tunahitaji ushindi