Biashara holela ya chuma chakavu inayofanyika bila vibali na leseni nchini, inapoteza mapato na kusababisha hasara kwa taasisi za umma ambazo miundombinu yake huibwa na wafanyabiashara hao.
Tangu taarifa zitolewe kwa mamlaka zinazohusika ikiwamo Ofisi ya Rais na ile ya Waziri Mkuu kwa kipindi cha miaka saba iliyopita, kuhusu biashara hiyo holela ya chuma chakavu na Kampuni ya Kenwood Enterprises Tanzania Limited ya Mlandizi, Kibaha Mkoa wa Pwani, kuwa ni moja ya uhalifu mkubwa unaolikosesha Taifa mapato hakuna hatua zozote zilizochuliwa.
Biashara ya chuma chakavu iliyoelezwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuwa haipaswi kutozwa kodi, imeendelea kuwanufaisha wafanyabiashara wa kigeni waliowekeza katika viwanda vya nondo na wengine wanaosafirisha holela nje ya nchi na kujipatia mabilioni ya shilingi yasiyolipiwa kodi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Kenwood Enterprises Tanzania Ltd, Henry Batamuzi, anasema tangu atoe taarifa kuhusu upotevu mkubwa wa mapato ya Serikali kutokana na biashara hiyo kuachwa ikifanyika holela, hakuna hatua zozote zilizochukuliwa na kwamba maisha yake yako hatarini.
Batamuzi anasema aliwasilisha taarifa ya biashara hiyo kufanyika holela kwa mara ya kwanza makao makuu ya Mamlaka ya Mapato Idara ya Uchunguzi wa Kodi, na pia kwa aliyekuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka hiyo, Harry Kitillya, aliyemjibu kwamba biashara ya chuma chakavu haina kodi.
Pamoja na madai hayo ya TRA kuwa haitozi kodi kwa biashara hiyo, miezi miwili iliyopita ilivamia viwanda vya kuzalisha nondo jijini Dar es Salaam na kudai kodi, jambo lililozua hofu kubwa kwa wafanyabiashara haramu wa chuma chakavu ambao wamekuwa wakiuza chuma katika viwanda hivyo na kwa wanunuzi wa chuma chakavu kinachosafirishwa nje ya nchi.
Anasema mfanyabiashara halali wa chuma chakavu ni lazima awe na cheti cha usajili wa kampuni kutoka Brela, namba ya utambuzi ya mlipa kodi (TIN), leseni ya biashara kununua chuma chakavu kutoka Halmashauri ya Wilaya, Manispaa au Jiji husika.
Pamoja na masharti hayo, anasema wafanyabiashara hao holela wa chuma chakavu wamekuwa wakihujumu miundombinu ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL), Shirika la Maji Safi na Maji Taka Dar es Salaam (DAWASCO), Shirika la Reli Tanzania (TRL), Mamlaka ya Reli Tanzania na Zambia (TAZARA) na Mamlaka zote za maji nchini.
Kuna jumla ya viwanda 14 vya kuzalisha nondo hapa nchini. Dar es Salaam vipo tisa, Pwani kimoja, Arusha viwili na Mwanza viwili.
“Sasa TRA wao wameingia katika kusaka kodi hiyo ya chuma chakavu, lakini wamekutana na kikwazo na wala hawawezi kupata kodi halisi kutokana na biashara hiyo kwani wafanyabiashara hao wanatumia risiti za biashara za gesi, vipuri vya magari, vifaa vya ujenzi na kuziacha kwenye viwanda vya kuzalisha nondo bila uthibitisho kama chuma hicho chakavu kimelipiwa kodi.
“Huu ni uhalifu mpya wa kupanga unaoendelea katika biashara ya chuma chakavu, unaopaswa kudhibitiwa kama TRA wana nia njema ya kukusanya kodi,’’ anasema Batamuzi.
Anasema, biashara ya chuma chakavu imekosa msimamizi, hivyo Serikali inatakiwa kukagua chuma hicho katika viwanda vya kuzalisha nondo na maghala ya wasafirishaji ili kujiridhisha kama mnunuzi na muuzaji wana nyaraka halali, vibali vya NEMC (Trucking form) fomu tano za SW/WM/3 zinazotakiwa kujazwa kwa mujibu wa Tangazo la Serikali namba 198 la Juni, 2013.
Anasema iwapo wanunuzi watabainika kukosa vibali vya NEMC waitwe na kutozwa faini kwa mujibu wa sheria za Baraza hilo. Pia TRA itoze kodi ya mapato kwa malipo yote yaliyolipwa kwa wafanyabiashara wa chuma chakavu, kwa kuwabana wanunuzi wanaosafirisha nje ya nchi na orodha ya waliolipwa fedha taslimu na hundi kwa biashara hiyo iwasilishwe Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).
Katika taarifa yake aliyoitoa miaka michache iliyopita kwa Idara ya Uchunguzi ya Kanda TRA Makao Makuu, kuhusu ukwepaji wa kodi uliofanywa na mfanyabiashara mmoja wa chuma chakavu, anasema maofisa wa Mamlaka hiyo walivamia kiwanda kimoja cha Dar es Salaam cha kuzalisha nondo na kukamata kompyuta mpakato, na baada ya uchunguzi walibaini ukwepaji mkubwa wa kodi unaofikia shilingi milioni 900.
Kwa upande mwingine anasema Serikali inapaswa kubeba lawama kwa kushindwa kwake kusimamia na kudhibiti biashara hiyo inayofanyika holela nchini, pia kufa kwa karakana za Mang’ula na Karakana ya Taifa ya Uhandisi wa Vipuri vya Mitambo ya Kilimanjaro (KMMT).
Hata hivyo, anasema kutokana uholela huo, Taifa limekubali kuua uhandisi wa mitambo ya chuma aina mild steel ambayo inatumika kwa ajili ya uzalishaji wa nondo.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, January Makamba, alipohojiwa na JAMHURI, kuhusu biashara ya chuma chakavu kufanyika holela nchini na kusababisha uharibifu wa miundombinu ya mashirika na taasisi za umma, anakiri kwamba kuna uzembe mkubwa unaofanyika katika usimamizi.
Makamba anasema NEMC jukumu lake ni kudhibiti biashara hiyo yenye wadau wengi, na kuhusu ulinzi wa miundombinu ni kazi ya wadau hao.
‘‘JAMHURI mko sahihi kabisa kwamba biashara hiyo imekosa usimamizi, hivyo tumeitisha mkutano wa wadau wote wiki mbili zijazo na kwamba NEMC tuna vifungu 300 vya sheria ya mazingira ambazo tunataka kuzitengenezea kanuni zitakazotumika kudhibiti biashara holela ya chuma chakavu,’’ anasema Makamba.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Pwani, Bonavientura Mushongi, ambaye ndiye pekee aliyefanikiwa kuyakamata malori matano yaliyokuwa na shehena ya chuma chakavu mkoani humo, iliyokuwa inasafirishwa bila vibali halali, ameieleza JAMHURI kwamba NEMC wameshindwa kutoa ushirikiano kwa jeshi hilo.
‘‘Tangu tukamate malori hayo, na kuwatafuta maofisa wa NEMC hatuelewi kilichoendelea, hata faini iliyotozwa na tumejaribu kuwaandikia barua kuomba ufafanuzi lakini hatupati majibu.
Nashauri NEMC watoe elimu kwa wananchi ili kupambana na biashara hiyo haramu ya chuma chakavu, ili Serikali ipate mapato yake na pia kudhibiti uharibifu wa miundombinu,’’ anasema.
Naye Ofisa habari wa NEMC, Ruth Mgwaza, anasema Baraza hilo limepokea taarifa hizo na kwamba wanazifanyia kazi na watazitolea ufafanuzi wiki hii.